LUSAKA, ZAMBIA

Na Kennedy Gondwe, BBC


Baada ya kushindwa mara tano mfululizo katika Uchaguzi Mkuu wa Zambia, hatimaye bahati imemuangukia Hakainde Hichilema, na sasa amefanikiwa kuwa Rais wa taifa hilo. 

Hichilema amemwangusha mpinzani wake mkuu, aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu, kwa kura zaidi ya milioni moja.

Hichilema mwenye umri wa miaka 59, anajitambulisha kama mwananchi wa kawaida ambaye wakati akiwa mdogo alikuwa mchungaji wa mifugo ya wazazi wake kabla ya kupambana na hatimaye kuwa mmoja kati ya matajiri wakubwa nchini Zambia.

Rais huyo mteule na kiongozi  wa United Party for National Development (UPND), anafahamika zaidi kwa kifupi kama HH. Alizaliwa katika familia ya kawaida na baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Zambia, kisha akahitimu shahada ya Uzamili ya Biashara (MBA) katika Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza.

Baadaye akijitengenezea utajiri kupitia masuala ya fedha, majengo, mifugo, afya na utalii.

Katika kampeni zake, ametumia historia zake zote mbili kuwaomba kura wananchi wa Zambia.

Amewaambia wapiga kura kuwa wanahitaji mtu tajiri na mwenye mafanikio katika biashara ili waelewe namna hasa ya kuupeleka mbele uchumi wa taifa hilo tajiri kwa madini ya shaba, huku likiwa na uhaba mkubwa wa ajira. 

Pia ametumia historia yake katika kilimo kuwaomba kura wakulima, akidai kuwa ataigeuza Zambia kuwa ‘kapu’ la chakula katika ukanda wa kusini mwa Afrika. 

Lakini kitu ambacho huenda ndicho kilichompa mafanikio makubwa zaidi katika uchaguzi huo ni namna alivyojichanganya na wapiga kura vijana. Zaidi ya nusu ya raia milioni saba waliojiandikisha kupiga kura ni vijana wenye umri chini ya miaka 35. Na kijana mmoja kati ya watano hana ajira. 

Kilichokuwa Chama tawala, Patriotic Front (PF), kiliingia madarakani mwaka 2011 kikiwaahidi wananchi ‘punguzo la kodi, fedha mifukoni mwao na ajira zaidi’. Kwa bahati mbaya hayo yote hayakutimia kwa vijana wengi na mamilioni yao wakahamishia nguvu kwa Hichilema.

Njia mojawapo iliyomuunganisha na ulimwengu wa vijana ni kupitia mitandao ya kijamii. Huu haukuwa uchaguzi wa kwanza kwa Hichilema kutumia mitandao kama ‘Facebook’ na ‘Twitter’ kuwa karibu na wapiga kura, lakini safari hii akaongeza kasi zaidi. Alikuwa pia tayari hakucheza rafu!

Mwaka jana HH alitoa video iliyoitwa ‘The tale of two professionals…’, ikimwonyesha yeye kama mfanyabiashara makini, mjanja na mwajibikaji, huku Lungu akionyeshwa kama mtu anayetumia fedha zake zote kwa ulevi, kwenye klabu za usiku. “Kati ya hawa wawili nani anayefaa zaidi?” inahoji video hiyo. 

Mbali na siasa, Hichilema amekuwa akichangia maoni, hasa ya masuala ya soka, kwenye mitandao ya kijamii – njia ya uhakika kabisa ya kuungana na wapiga kura. Kuna nyakati huwatania na kuwarushia madongo mashabiki wa Manchester United na Arsenal pale timu zao zinapopoteza mchezo.

Pia amewahi kuwapongeza wanasoka wa Zambia kama Patson Daka aliyejiunga hivi karibuni na Leicester City na Fashion Sakala wa Rangers ya Scotland, wanaovuna fedha nyingi Ulaya. Wakati klabu zao zikiwa kwenye maandalizi ya msimu mpya, HH ameonekana kufuatili michezo ya kirafiki na kutoa maoni yake, ishara inayoonyesha kuvutiwa na maendeleo yao. Lungu amewahi kujaribu mbinu kama hizo, lakini wengi wanaamini kuwa alifanya kwa kulazimishwa.

Kwenye mitandao ya kijamii, Hichilema amekuwa akitumia lugha za mitaani, kama vile neno ‘bally’ (kwa Kiswahili cha mtaani ‘dingi’), linalotumika kumtambulisha mtu kama baba yako. Matumizu ya ‘hashtag’ kama ‘#BallyWillFixIt’ (#DingiAtarekebisha) ametumia katika juhudi za kuzungumza lugha ya kawaida masokoni na mitaani, si kwa wafanyabiashara wakubwa wenzake. 

Matumizi hayo ya lugha ya mitaani yalimsogeza zaidi kwa jamii. 

Baada ya ushindi wa Hichilema, mashabiki wake waliingia kwenye mitaa ya Lusaka wakishangilia kwa furaha na kuimba “Twende zetu dingi!”

Kwa hakika Hichilema ameonyesha uvumilivu mkubwa katika siasa. Pamoja na kushindwa kwake mara tano kwenye uchaguzi mkuu, siku zote huwakumbusha watu kuwa amewahi kukamatwa mara 15 tangu alipoingia katika anga za siasa.

Mwaka 2016, alishitakiwa kwa makosa ya uhaini akidaiwa kushindwa au kukataa kuupisha msafara wa Rais. Alikaa rumande kwa miezi minne kabla ya kufutiwa mashitaka.

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya ushindi, Rais mteule HH, alimwelekezea mkono wa upendo na amani mtangulizi wake, Lungu, akisema:

“Usiwe na hofu kabisa, mambo yatakuwa mazuri. Hatutalipa kisasi wala hautapigwa mabomu ya machozi.” 

Wakati wa utawala wa Lungu, Hichilema alikuwa akidai mara kwa mara kupewa vitisho na kukamatwa kwa lengo la kumnyamazisha yeye binafsi na kama kiongozi wa upinzani.

Baada ya hatimaye kupata nafasi hiyo ya juu kabisa nchini Zambia, bila shaka Hichilema atakuwa na furaha kubwa. Lakini rais huyo mteule anapaswa kuanza kazi mara moja katika taifa hilo lenye matatizo lukuki. 

Pamoja na kuwapo kwa ukosefu mkubwa wa ajira, gharama za maisha zimepanda kwa kasi kubwa.

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998, mwaka jana Zambia ilikumbwa na mdororo mkubwa wa uchumi kutokana na janga la corona lililoikumba dunia.

Zambia inadaiwa na wakopeshaji wa nje takriban dola za Marekani bilioni 12. Kwa mujibu wa taasisi moja ya masuala ya fedha, S&P Global, hii maana yake ni kuwa walau asilimia 30 ya mapato ya nchi hii hutumika kulipa riba.

Mwaka jana Zambia ilishindwa kulipa riba yake na kuifanya kuwa taifa la kwanza la Afrika kushindwa kufanya hivyo wakati wa janga la corona. Lakini pia inapitia wakati mgumu katika kulipa mikoipo mingine.

Kama atashindwa kuanza kurekebisha haraka sana baadhi ya matatizo haya, bila shaka umaarufu wake utashuka.