DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan Ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana huku ikiambatanisha mapendekezo kadhaa ili kuimarisha ufanisi wa shughulu zake.
Katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa wa kitaifa akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, anapendekeza kufanyika kwa marekebisho kadhaa ikiwamo kutungwa kwa sheria mpya.
Baadhi ya wanasiasa wameonyesha kukubaliana na mapendekezo hayo, wakiamini yataboresha uendeshaji wa shughuli za Uchaguzi Mkuu kwa siku zijazo.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wanasiasa hao wanasema mapendekezo ya NEC ni hatua muhimu ya kuboresha utendaji wa tume na yanajibu maswali kadhaa ya vyama vya siasa hasa vya upinzani wanayoyaibua mara kwa mara.
Endapo mapendekezo hayo yatakubaliwa na serikali, wanasema yatajibu hoja za kutaka Uchaguzi Mkuu, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa au wa marudio kuwa huru, wa haki na wa kuaminika.
“Vyama vya siasa vimekuwa vikilalamika kila kukicha kwamba kuna baadhi ya mambo katika utendaji wa NEC hayako sawa, sasa ukiniuliza mimi nitakujibu kwamba mapendekezo hayo ni hatua ya awali ya kuelekea katika maboresho ya utendaji kazi wa NEC,” anasema kiongozi mmoja wa chama cha siasa, akiomba hifadhi ya jina lake.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa Ikulu mbele ya Rais na Jaji (mstaafu) Kaijage, wakati akikabidhi Taarifa ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 25, 2020, ni kutungwa kwa sheria itakayoiwezesha NEC kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Mapendekezo mengine ni kuwe na watendaji wa NEC kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi ya halmashauri; pia mamlaka husika ziangalie uwezekano wa kuunganisha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 ili kurahisisha utekelezaji wa sheria hizo.
Pia NEC inapendekeza sheria za uchaguzi zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili na serikali iangalie uwezekano wa kuziwezesha kifedha asasi na taasisi zinazotoa elimu ya mpiga kura katika hatua mbalimbali za mchakato wa uchaguzi.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Samia amesema mapendekezo ya NEC ni ya msingi na amewataka wadau mbalimbali kuyajadili na kuyawasilisha serikalini huku akiyatilia shaka baadhi, kwamba yataipa mzigo mkubwa serikali katika kuyatekeleza.
“Mapendekezo yote ni ya msingi, wadau wayajadili kwa maana kila jambo linaloanzishwa lina msingi wake. Nawaomba wadau wakakae waangalie mapendekezo yaliyotolewa na watuletee serikalini na sisi tutaona tutakavyoyafanyia kazi.
“Pia changamoto ninayoiona ni serikali tutakapotakiwa kuwa na wasimamizi wa kudumu hadi ngazi ya halmashauri na itasababisha kuwa na bajeti kubwa na lile pendekezo la kuzisaidia taasisi za kiraia nalo litasababisha mzigo mkubwa wa fedha serikalini na yote hayo yanazungumzika, yanaweza kufanyiwa kazi,” anasema Samia.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wengine wa vyama vya siasa, akiwamo Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, wanatofautiana na Jaji Kaijage, wakisema mapendekezo hayo hayalazimishi uwapo wa hitaji la Katiba mpya.
“Wanachokifanya NEC ni kutoa mapendekezo ya kuboresha utendaji wao. Mapendekezo yao ni muhimu kwa maana ya kuboresha ufanisi wao kwa kuwa yamejikita katika sheria za uchaguzi, ingawa hayagusi hitaji la sasa la Katiba mpya. Sisi kama chama kipaumbele chetu ni kutaka NEC iwe huru,” anasema Shaibu na kuongeza:
“Kwamba viongozi wa NEC kuanzia kwa mwenyekiti wake, mkurugenzi hadi makamishina wasipatikane kutokana na mchakato wa vyama vya siasa, kwa maana wasiteuliwe na Rais na hapo itakuwa huru lakini kinyume chake ni vigumu kuwa huru.
“Kwa mfano, yule Ramadhani Mapuri, amewahi kuwa na cheo kikubwa ndani ya CCM (Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi) lakini leo ni Kamishina! Kwa hiyo lazima kuwepo na marufuku ya kuwapo kwa watu kama hao. Sasa sisi kama chama (ACT – Wazalendo), tunatafuta nakala ya taarifa ya NEC kisha tutaichambua na kutoa taarifa rasmi kwa wananchi.”
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Martha Chiomba, anaungana na mawazo ya Shaibu, akisema kabla ya kuzungumza kwa kina, kwanza wataisoma taarifa ya NEC ndipo watakapotoa maoni yao.
“Hatuwezi kukurupuka. Tutakaa chini na sisi tuje na mapendekezo yetu,” anasema Martha.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa, anasema hawezi kutoa maoni kuhusu taarifa ya NEC kwa sababu wanaamini mwaka jana hakukuwa na Uchaguzi Mkuu.
“CUF tulialikwa Ikulu kushuhudia kukabidhiwa kwa taarifa hiyo, lakini hatukwenda. Hatukwenda kwa sababu Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa na kasoro chungu nzima ndiyo maana hatutaki hata kuijadili taarifa hiyo,” anasema Ngulangwa.