Anuani ya makala yetu leo inatudai fasili ya maneno mawili ya Kiswahili: Kazi na Ukupe. Kazi kwa fasili inayozingatia sheria ni “shughuli yoyote halali inayompatia mtu kipato au masilahi fulani halali yaliyokubaliwa,” wakati kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Toleo la Pili) iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili – TUKI (sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili – TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2004, ukurasa wa 432, ukupe ni “hali ya kutegemea watu wengine ili kupata mahitaji ya maisha.”

Mtume  Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Ni bora kwa mtu kuchukua kamba, akaenda mlimani na kuleta mzigo wa kuni mgongoni mwake na kuziuza ili Allaah Ailinde heshima yake, kuliko yeye kuomba kutoka kwa watu bila kujali kama watampatia au watamnyima.”

Mafundisho ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) yanatuonyesha uwepo wa aina mbili za watu katika suala la kutafuta chumo la kukidhi mahitaji ya mtu katika maisha yake hapa duniani; aina ya kwanza, ni mtu afanyaye kazi na kupata pato lake, hivyo kulinda heshima yake, na aina ya pili, ni yule aliyefanya kuomba kutoka kwa watu wengine ndiyo kazi yake; mtu anayepata mapato bila ya kutumia jasho lake; mtu mwenye nguvu, asiyekabiliwa na kikwazo chochote cha kufanya kazi, lakini ameamua kuishi kwa kuwategemea wengine, na huyu ndiye aliyeuridhia udhalili katika maisha yake.   

Katika Uislamu, kazi inamaanisha juhudi anazozifanya mtu katika shughuli yake binafsi au ya kuajiriwa ili  kupata pato halali na katika mipaka ya maagizo ya Mwenyeezi Mungu na kanuni zake.

Kufanya kazi na kupata pato halali linalomuwezesha mtu kuendesha maisha yake akitafuta radhi za Mola wake na kuyaandaa maisha yake ya kesho Akhera ndiyo utekelezaji wa mafunzo ya Uislamu kama tunavyosoma katika Qur’aan Sura ya 28 (Surat Al-Qas’as’) Aya ya 77 kuwa:

“Na utafute, kwa Aliyokupa Mwenyeezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyeezi Mungu alivyokufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyeezi Mungu hawapendi mafisadi.”

Aya hii inatuzindua juu ya wajibu wetu wa kulishughulikia fungu la dunia kwa kufanya kazi halali zikazotuwezesha kujenga nguvu ya kiuchumi ya kuendesha maisha yetu, kukidhi mahitaji yetu mbalimbali na kujiandalia vema nyumba ya Akhera.

Ni dhahiri kuna ibada kadhaa ambazo bila ya nguvu ya kiuchumi huwezi kuzitekeleza kama vile ibada za Hijja, Zaka, Sadaka na kadhalika. Katika utekelezaji wa haya, mwenye mali ndiye mwenye fursa zaidi ya kuzifanya ibada hizi kuliko yule ambaye hana mali.

Kufanya kazi na kupata chumo halali linalotokana na jasho lako ndiyo njia bora ya kujenga uchumi wako kama anavyotufundisha Bwana Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akisema: “Hakika bora ya chumo ni chumo la mtu linalotokana na mkono wake (kazi yake).”

Akafafanua zaidi Bwana Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akisema: “Mwenye ezi Mungu anampenda mja mwenye kufanya kazi na yeyote mwenye kuhangaikia familia yake anakuwa ni kama anayepigana jihadi katika Dini ya Mwenyeezi Mungu.”

Kufanya kazi kwa nia safi na kumtanguliza mbele Mwenyeezi Mungu kunahesebiwa ni ibada inayompa mfanyakazi huyo thawabu mbali ya malipo anayopokea kutokana na kazi hiyo. Kama hilo halitoshi, yapo madhambi ambayo hayafutwi na ibada nyingine yoyote zaidi ya kufanya kazi kama Bwana Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) anavyotufundisha akisema: “Hakika katika madhambi, kuna madhambi ambayo hayafutwi na Swala wala Swadaka wala Hijja na inayafuta madhambi hayo ile tabu anayoipata mja katika kutafuta maisha yake.”

Kutokana na umuhimu huo wa kufanya kazi ili kila mja apate riziki yake ya halali, Bwana Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akatufundisha akituambia: “Mkimaliza kuswali alfajiri msilale mkaacha kwenda kutafuta riziki zenu.”

Uislamu haukuishia tu kuelekeza na kufundisha umuhimu na ulazima wa kufanya kazi bali pia umeelekeza umuhimu wa ujira wa kazi fulani kujulikana kabla ya  kazi hiyo kufanyika. 

Bwana Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amekataza kumpa mtu kazi yoyote mpaka kwanza ujira wake uwe wazi. Habari ya kwamba mtu afanye kazi halafu mapatano ya ujira wake yawe baada ya kazi, hilo halikubaliwi na Uislamu.

Uislamu umemuelekeza mwajiri pia kwamba baada ya kukamilika kazi ule ujira waliokubaliana na mfanyakazi usicheleweshwe na ulipwe kwa mujibu wa makubaliano yao yalivyokuwa. Bwana Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Watu watatu mimi ni mgomvi wao siku ya Kiyama (mmoja wao) ni mtu aliyempa mtu kazi kisha hakumlipa ujira wake.”

Akaongeza tena kwa kusema: “Kumdhulumu mfanyakazi malipo yake ni miongoni mwa madhambi makubwa.”

Akamalizia Bwana Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kwa kusema: “Mpeni mfanyakazi ujira wake kabla halijakauka jasho lake.” 

Kupitia mafunzo haya ya Uislamu tumeona kuwa Uislamu unawataka watu wafanye kazi iwe ya kujiajiri, kuajiriwa au biashara na kufanya hivyo ndiyo kulinda hadhi na heshima zao na wajiweke mbali na tabia za mtu kupe ambaye pamoja na nguvu na uwezo wa kufanya kazi alionao ameamua, bila ya haya wala soni, kuwa ombaomba na kuishi kwa kuwategemea wengine.

Wakati wa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kuna Swahaba aliyezoea kuja kumtaka msaada Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani), siku moja Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alimuuliza kama ana akiba yoyote nyumbani kwake. 

Yule bwana akamwambia anacho kitambaa. Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alimwagizia akilete, na kilipoletwa alikinadi nacho kikanunuliwa kwa dinari mbili. Moja kati ya hizo dinari mbili Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alimwambia anunulie chakula na akiache nyumbani. Ya pili Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) mwenyewe alikwenda sokoni na kununua kile chuma cha shoka na kumtilia mpini kwa mkono wake. Kisha alimwambia asionekane pale mpaka baada ya muda fulani. 

Swahaba huyo alielekea msituni ili kukata kuni. Baada ya muda Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alikutana na huyo bwana kukiwa na sauti ya pesa zikilia mfukoni kwake. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alimwambia: Hii ni bora kabisa kuliko kuomba omba. 

Mfano mzuri wa wajibu wa kila mtu kufanya kazi wakiwamo viongozi wa dini tunaupata kupitia mitume na manabii (Allaah Awape Amani) ambao kwetu ni ruwaza (kiigizo) njema kwamba walifanikiwa katika kazi zao kwa kiasi kikubwa ambapo Nabii Daawud alikuwa mtengenezaji makoti ya chuma na ngao zake, Nabii Adam alikuwa mkulima, Nabii Nuuh alikuwa seremala, Nabii Idriis alikuwa mshonaji na Nabii Muusa alikuwa mchungaji.

Kwa upande wake Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Allaah Hakumtuma Mtume bila ya yeye kuchunga kondoo.” Wakamuuliza Maswahaba: “Hata wewe, ewe Mtume wa Allaah?” Akajibu: “Hata mimi, nilikuwa nikichunga kondoo wa watu wa Makkah kwa ujira.” 

Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) aliwaambia Maswahaba zake hivi ili kuwafunza kuwa heshima inakuwa kwa wale wanaofanya kazi, na si wale wenye kukaa na kuzembea na kuwa kupe kwa kuwanyonya wengine. 

Uislamu mbali ya kuchunga haki za mfanyakazi pia umeweka wazi wajibu wake. Kwamba mfanyakazi (mtumishi) anapaswa kuwa mwadilifu na mkweli kwa muajiri wake na ajue kwamba kwa dhuluma yoyote anayomfanyia muajiri wake, hayo hayataishia hapa duniani, kwani kwa hakika kesho (Siku ya Hukumu) ataulizwa mbele za Mwenyeezi Mungu na atapoteza thawabu nyingi atakazonyang’anywa na Mwenyeezi Mungu kama fidia ili kumlipa mwajiri aliyedhulumiwa na mwajiriwa.

Amesema Bwana Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani): “Na mtumishi (mfanyakazi) ni mchunga katika mali ya mwajiri wake na yeye ataulizwa juu ya uchungaji wake.”

Mafunzo yote haya yametuonyesha kuwa kufanya kazi ni wajibu kwani ndiyo njia ya kupata kipato ambacho kitamsaidia mtu kujikimu, kuikimu familia yake na kutenda mema yanayomridhisha Mola Muumba ambayo yanahitaji mali na bila ya mali hayatendeki kama vile kutoa Zaka na Sadaka.

Nihitimishe makala hii kwa kumkumbusha kila mfanyakazi kuwa changamoto  kubwa iliyo mbele yake ni kuhakikisha kuwa malipo anayolipwa na mwajiri wake yalingane na kazi aliyofanya kwa mujibu wa makubaliano yao. Kutumia wakati wa kazi, vifaa na nyezo za mwajiri wako kwa masilahi yako binafsi ni dhuluma na utakwenda kuulizwa na kuhukumiwa mbele ya Mwenyeezi Mungu. 

Kila mmoja wetu afanye kazi na hususan za kujiajiri kama Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alivyomwelekeza yule Swahaba kwenda kukata kuni, kuzibeba mgongoni na kuja kuziuza. Na kwa waajiri na waajiriwa watendeane uadilifu ili kuepuka kinachoitwa “ waajiri wanajidai (pretend) kulipa mishahara na waajiriwa wanajidai kufanya kazi.

Haya tukutane Jumanne ijayo!

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania. Simu: 0713603050/0754603050