ZANZIBAR
Na Masoud Msellem
Karibu miezi miwili imepita sasa tangu kuachiwa huru kwa waliokuwa mahabusu; masheikh wa Jumuiya ya Uamsho Tanzania.
Hawa waliswekwa kizuizini kwa zaidi ya miaka saba wakituhumiwa kutenda vitendo vya kigaidi kati ya Januari 2013 na Juni 2014, kinyume cha Kifungu cha 27 cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
Kuachiwa kwao huru katikati ya Juni mwaka huu kunatokana na uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwafutia mashitaka na kutokuwa na nia ya kuendeleza kesi.
Tangu walipoachiwa huru, kwa sababu baadhi tunafahamiana na tuna uhusiano kwa muda mrefu, nilichofanya kwanza ni kuwasiliana nao kwa simu, kwani baada ya kuachiwa sikupata fursa kuwatembelea hadi wiki mbili zilizopita.
Hapo ndipo nilipofanya ziara kwa baadhi yao, hususan wale tuliokuwa na ukaribu zaidi.
Ziara hizo zililenga kuonana nao ana kwa ana, kuwasalimu, kuwafariji kwa masaibu makubwa waliyopitia, kuwatia moyo na hima mpya, kubadilishana nao mawazo na kusikia changamoto zao katika kukabiliana tena na mazingira ya uraiani.
Nilimtembelea Ustadh Abdallah Said (Madawa) aliyekuwa Katibu wa Jumuiya ya Uamsho anayeishi Misufini, mjini Zanzibar.
Uhusiano wetu mwema ni wa muda mrefu, pia mkewe ni jamaa yangu wa damu. Nilimfariji Ustadh Madawa na kumpa pole kwa mitihani mikubwa iliyomsibu, si tu kwa kuwa mahabusu kwa miaka mingi, bali pia kwa kufiwa na dada na mama yake mzazi, yeye akiwa kizuizini!
Msiba wa mama yake aliyekuwa mgonjwa kwa muda, ulitokea kama siku 40 tu kabla hajaachiwa huru.
Tulizungumza mengi kwa kina. Nikasikiliza kwa makini changamoto zake na hali tete inayomkabili baada ya kuwa kizuizini kwa kipindi kirefu.
Nilichogundua ni mkwamo na kugota kwa baadhi ya shughuli zake za kiuchumi, ikiwamo kufunga duka lake la dawa za mitishamba eneo la Mtendeni, hatua chache kutoka barabara kuu ya Darajani.
Nilimshauri ajikaze na kuanza upya, japo nilihisi uzito wa namna ya kujipanga upya, hususan upande wa mtaji.
Baada ya hapo nikaelekea Kwarara, Fuoni, nje kidogo ya kitovu cha mji, kumtembelea Ustadh Said Amour.
Huyu tumejuana kitambo, na zaidi tumewahi kuwa waajiriwa pamoja wa Kampuni ya Kuhudumia Ndege Zanzibar (ZAT).
Ustadh Said alinieleza kuwa wakati akiwekwa mahabusu miaka saba iliyopita, alikuwa bado katika ajira na kwa ‘maumbile’ ya ajira za kampuni binafsi, sasa hana kazi!
Mkasa wa kuwekwa kwake kizuizini ulikuwa na machungu ya aina yake tofauti na wengine, kwani ulimhusisha pia ndugu yake wa tumbo moja, Salum Amour; wao wakiwa ndio wanaume wakubwa katika familia yao.
Awali walikuwa na faraja kiasi kwani baba yao alikuwa hai. Lakini wakiwa mahabusu, walianza kugubikwa majonzi mutawalia (yenye mfuatano).
Kwanza, kwa kufariki dunia mama yao mzazi mwaka 2018, kisha baba yao mwaka jana. Hawakupata fursa adhimu ya kuwauguza na kuwazika wazazi wao.
Lakini pia hawakupata nafasi ya kuwapa malezi na kuwasimamia watoto wao wa kuwazaa (Ustadh Said aliwaita mbele yangu), ambao wakati wakikamatwa wengine walikuwa wadogo kabisa, wenye kuhitaji usimamizi wa karibu wa baba na mama.
Ustadh Said Amour anasema kuwa kwake kizuizini pia kulisitisha masomo yake ya shahada ya biashara Kampala International University (KIU).
Kwa upande wa mdogo wake, Salum Amour, msomi mwenye shahada ya uzamili katika fani ya biashara aliyekuwa mwajiriwa wa kampuni moja binafsi, hapana shaka ajira yake ilitoweka kama ilivyokuwa kwa kaka yake.
Licha ya majonzi ya kuondokewa na wazazi wao wote wawili, kibarua kizito kilicho mbele yao ni namna ya kujipanga upya kimaisha ili kusimamia ndugu na familia zao, wao wakiwa wanaume wakubwa katika familia.
Mwishowe nikamtembeleaAntar Hamoud nyumbani kwake, Maungani, kama nyumbani kwa Ustadh Said, nako ni kando na mji kidogo.
Mimi naAntar tumekulia eneo moja. Ni kama ndugu kwangu, na kimsingi alisoma shule na ndugu yangu.
Anaonekana kufarijika kwa kuwa huru kama wengine, na akanieleza kuwa siku walipofutiwa mashitaka, hakuamini mpaka walipotolewa nje!
Lakini kwa hakika Antar ana mzigo wa maumivu makubwa uliosababishwa na kuwekwa kwake mahabusu kwa miaka mingi.
Yeye alikuwa mfanyabiashara mwenye hima, mjasiriamali na wakala wa wawekezaji. Mpaka anawekwa kizuizini miaka saba iliyopita, alikuwa mbioni kushirikiana na kampuni za nje kuwekeza katika miradi muhimu Zanzibar. Nitaeleza baadaye.
Kuwekwa kwake kizuizini kulisambaratisha biashara, uwekezaji, familia na kubwa zaidi kupoteza faraja na maliwazo ya mama yake ambaye licha ya udhaifu wa afya yake, alikuwa ‘kiguu na njia’ kwenda gerezani kumjulia hali mwanawe.
Alifanya hivyo mara kwa mara hadi alipofariki dunia mwanzoni mwa Aprili mwaka huu, akiondoka duniani na donge (kinyongo) la kumkosa mwanawe na kukosa fursa ya kushuhudia kuachiwa kwake huru.
Kufahamu hasara na maumivu makubwa aliyopata na yanayoendelea kumkabili Antar upande wa kiuchumi hakutaki mahojiano makubwa naye, bali kwa kila aliyekuwa mfuatiliaji wa mwenendo wa kesi ya Uamsho atakumbuka waraka muhimu aliouandika mama yake, marehemu Bi Aziza Muhammed mwaka 2018 kwa DPP, Wizara ya Sheria na Tume ya Haki za Binadamu uliokuwa na anuani: ‘Huzuni na Malalamiko ya Mama Mzazi wa Mtuhumiwa wa Ugaidi, Antar Hamoud.’
Katika waraka ule Bi Aziza anaeleza kinagaubaga namna mwanaye anavyoishi katika mazingira magumu gerezani, kuathirika kisaikolojia na kuharibika kwa kazi na biashara zake, ikiwamo kukwama kwa miradi miwili anayoisimamia chini ya Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).
Mradi mmoja ulihusisha ujenzi wa kiwanda cha mafuta ya kupikia aina ya ‘Sunflower’ uliotarajiwa kuwekeza dola za Marekani milioni 12 kutoka Kampuni ya Blue Horizon Investment Co. Ltd ya Kenya, ambayo Antar alikuwa mwakilishi wake na meneja mkuu.
Mradi wa pili ni wa Sinbad Company Ltd., kiwanda cha kutengeneza sabuni nyeupe ya unga na sabuni ya maji, uliotarajiwa kuwekeza dola za Marekani 990,000, Antar akiwa mkurugenzi.
Miradi hiyo iliyokuwa ikisimamiwa na Antar na biashara zake nyingine si tu zilikwama na kusambaratika, bali tuhuma alizopachikwa za ugaidi pia zimeharibu haiba na uhusiano wake na wawekezaji na washirika wake kibiashara.
Antar kama wenzake (huenda yeye ni zaidi), kuwa kwake mahabusu kumeangamiza kila kitu chake, anakabiliwa na mustakabali wenye giza totoro kiuchumi katika kuhuisha biashara na miradi iliyokwama kwa kipindi kirefu.
Sura niliyoipata kwa ziara hizi kwa hao wachache miongoni mwa waliokuwa mahabusu, inaakisi na kuwakilisha wengine ambao japokuwa kwa sasa wako huru, lakini wameathirika kiuchumi, kijamii na kisaikolojia.
Haya yanadhihirishwa kwa kauli za mapema za Sheikh Farid Had baada ya kuachiwa huru, kwamba madhara waliyoyapata ni makubwa, akitolea mfano kuangamia kwa biashara zake, ikiwamo daladala.
Haya ndiyo matokeo mabaya ya Sheria ya Ugaidi kwa watuhumiwa wa Uamsho ambao ni wachache miongoni mwa waathirika wengi wanaoendelea kusota mahabusu.
Ni sheria yenye sura ya wazi ya uonevu inayogongana moja kwa moja na misingi ya utu.
Watuhumiwa mara nyingi hutiwa nguvuni kwa kutekwa, huteswa na hakuna dhamana. Zaidi ya yote hakuna namna ya kudai fidia baada ya mahakama kuwaona hawana hatia!
Hakuna fidia kwa muda uliopotezwa, uchumi uliosambaratika, familia zao zilizovurugika na kupigwa kwao chapa ya milele ya sifa mbaya ya ‘ugaidi’ inayoacha jeraha litakalowaathiri daima katika uhusiano wao.
Kwa ufupi, uchungu, maumivu na majonzi yanayoletwa na Sheria ya Ugaidi huanza kuumiza kuanzia kizuizini na kuendelea madhila yake hata ukiwa huru.
Watu makini katika vyombo husika wanapaswa kuliangalia jambo hili kwa kufungua mlango na si kuchungulia kwenye tundu la ufunguo.