Na Pawa Lufunga

Utawala bora unaoheshimu haki, uhuru wa wote, haki sawa na furaha kwa wote hutokana na siasa safi inayosimamiwa na jamii chini ya mifumo safi ya kisheria kupitia katiba iliyoandaliwa kwa ushiriki wa jamii.

Ni wazi kuwa kila binadamu anatamani kuiona jamii ikiishi namna hiyo, na hili halipingwi kwa misingi ya chama, dini wala mihemko ya mtu kwa masilahi yake. 

Kila mtu anatamani kuishi na kuona jamii ikiishi katika amani, furaha, haki na kushikamana vema huku ikisonga mbele katika ujenzi wa nyenzo muhimu za mahitaji ya maisha yao kama njia za uchukuzi, elimu, maji, afya na umeme.

Ili hayo yajengwe vema, jamii inahitaji katiba safi inayotaja wazi uhuru wa watu, haki za watu, utawala wa kisheria na misingi ya kidemokrasia kwa ujumla.

Rais wa zamani wa Marekani, Abraham Lincoln, aliamini kuwa ili jamii iishi kwa furaha, amani na upendo na iweze kuendelea na kuishi kwa haki na usawa inahitaji serikali safi, iliyotokana na jamii na itimize majukumu yake kwa kufuata matakwa ya jamii husika. 

Serikali ya kidemokrasia inatakiwa kutokana na watu na watawala waongoze watu kwa kuwarahisishia upatikanaji wa mahitaji yao na si wachache kupeana fursa za uongozi wa jamii nzima na wachache hao kujipa nafasi ya kuamua maisha ya jamii nzima.

“Demokrasia ni mfumo wa serikali ya watu, inayotokana na watu kwa ajili ya watu hao,” anasema Rais huyo wa 16 wa Marekani, akisisitiza kuwa msingi mkubwa wa serikali ya kidemokrasia ni watu.

Watu wa jamii husika ndio wanaotakiwa kuwa na mamlaka, miongoni mwao watokee wagombea wa nafasi za uongozi zinazohitajika, na jamii yao ichague wale wanaowataka na watakaochaguliwa waongoze kwa masilahi na matakwa ya jamii.

Kinachoumiza jamii nyingi duniani ni pale ambapo maneno ya falsafa hii yanaishi vinywani mwa wanaotafuta fursa za uongozi; wanapoupata hujiona hawawezi kuwajibishwa kutokana na upungufu wa kikatiba katika nchi husika na mara hugeuka na kuwa watawala wa mambo yao (wabinafsi).

Si ajabu sana hasa kwa Afrika (hili lipo sana), mtu anayesimama na kujinadi kuwa mtetezi wa wenye mahitaji, anatambua udhaifu wote wa kisheria na anasimama kudai marekebisho lakini pindi atakapokuwa kwenye mamlaka, inakuwa mwisho wa madai hayo.

Anakwenda kuungana na aliokuwa akiwalalamikia kuwa hawatendi sawasawa, naye anaanza kutenda kama wao na pengine zaidi ya pale wanapoishia wao katika yale aliyosimama kuyapinga awali hadi akaaminiwa kupewa nafasi hiyo ili atakayatekeleze.

Mwalimu Julius Nyerere katika moja ya nukuu zake, amewahi kunukuliwa akisema kuwa jamii ndiyo yenye wajibu wa kuwadhibiti viongozi na viongozi wana wajibu wa kuheshimu haki za watu.

“Jamii inatakiwa kutokuwaogopa watawala, iwakosoe kwani jamii mkiwa waoga mtazalisha watawala madikteta,” anasema Mwalimu Julius Nyerere huku akiwaonya watawala wenye tabia za kuonea watu, kupuuza watu na kulazimisha yale wanayoyaamini waliopo madarakani pekee kuwa ndiyo mawazo sahihi.

Wanaharakati wengi Afrika na baadhi ya mataifa ya Asia na yale yenye tawala za kifalme hukoUlaya, wamekuwa wakipuuza demokrasia kwa kuendelea na katiba zisizoendana na matakwa yajamii.

Tawala za kurithishana, yaani kizazi kilichotoa kiongozi mwanzoni mwa ujenzi wa mifumo kinadumu katika mamlaka vizazi na vizazi bila kujali uwezo na wingi wa rasilimali watu waliomo katika taifa husika. Inakera sana.

Watawala wengi wamefeli katika suala la utendaji wa haki kwenye mamlaka za utawala, kusimamia matakwa ya jamii nje ya matakwa ya wenye mamlaka na kuheshimu haki za binadamu.

Wengi wamekuwa watamu mioyoni mwa watu katika siku zao za awali madarakani kutokana na kauli zenye matumaini, lakini siku chache baadaye hujikuta wakipoteza wafuasi na kukimbilia kufunga ndoana vyombo vya dola ili kulinda tawala zao.

Watawala wengi wenye sifa hizi huamini kuwa kwa kutumia polisi wenye bunduki kutisha watu, magereza kuwaumiza wakosoaji wenye wafuasi wengi na mamlaka za mapato kuwatengenezea kashfa na kesi za kukwepa kodi na kuhujumu uchumi; huamini kuwa watadhoofisha upinzani ili waweze kupiga dili zao bila vikwazo na kushinikiza matakwa yao kwa nguvu watu watake wasitake yawezekane.

Kwa bahati mbaya huwa wanashindwa kuuamini ukweli ulio wazi kuwa upinzani si mtu wala si watu,  upinzani ni moyo utokanao na kutokuridhishwa na mifumo au vitendo vinavyofanyika katika jamii.

Hivyo, kuwaua wapinzani na hata kuwafunga gerezani wote wanaoonyesha mawazo kinzani na mfumo uliopo bila kuzishughulikia kero au madai wanayoyasimamia, hakujawahi kumaliza upinzani mahali popote duniani.

Wakosoaji wanaosimama na kusema hadharani wanakuwa kama mitume tu wateule wa Mungu ambao wanatumika kufikisha ujumbe wa wengi wanaosononeka mioyoni na wasiweze kusema, kumbe njia sahihi ya kumaliza upinzani ni kumaliza masuala yanayoibuliwa.

‘Amani ni tunda la haki na bunduki ni silaha ya kupigana vita ya silaha.’ Falsafa hii ni muhimu kwa wote wanaopata neema ya kuteuliwa na Mwenyezi Mungu kuziongoza jamii za watu kwani bila haki hakuna amani na kutumia bunduki hakumalizi tatizo husika.

Maneno matakatifu kutoka katika vitabu vitakatifu vyote yanaeleza kuwa binadamu si mkamilifu bali Mungu pekee ndiye amekamilika.

Kwa kutambua ukuu huu wa Mungu ni vema jamii ikatambua kuwa, kuwa na cheo fulani hakumfanyi mtu kuwa na akili kuliko wengine; kuwa kiongozi hakumaanishi mawazo yako pekee ndiyo yanatakiwa kuamua nchi au jamii iishije, bali kwa kuheshimu sheria za jamii husika (Katiba).

Kutii na kutimiza mahitaji ya watu unaowaongoza na kusimamia misingi ya haki na juhudi zenye lengo la kupunguza kero za watu na kurahisisha maisha yao ni tunu pekee ambayo mwanasiasa au mtawala anaweza kushinda hila zote na mapambano dhidi ya wakosoaji wake.

Matumizi ya nguvu, makaripio, magereza, vipigo na kutesa wakosoaji kama ambavyo watawala wengi wamekuwa wakiamini na kutenda ni makosa ambayo baadaye husababisha watawala wa aina hii kujikuta wakiongoza kwa misukosuko na kusahaulika mara tu wanapomaliza muda wao madarakani. 

Viongozi andikeni ‘legacy’ (alama) kwa wema.

0689990248