DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Maalumu
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) iliyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu aina mbalimbali za chanjo za Covid – 19 (corona).
Ufuatao ni ufafanuzi/majibu ya TMDA kuhusu chanjo za corona.
1. Chanjo za Covid – 19 ni nini?
Chanjo za Covid – 19 ni bidhaa za kibaiolojia zilizotengenezwa ili kukinga mwili dhidi ya virusi vya ugonjwa wa homa kali inayoathiri mfumo wa upumuaji aina ya SARS – CoV-2 ambavyo husababisha ugonjwa wa virusi vya corona unaojulikana kama Covid-19.
2. Ni aina ngapi za chanjo za Covid-19 na zinafanyaje kazi?
Chanjo za Covid – 19 zimetengenezwa ili kuufundisha mwili kujikinga, kutambua na kuzuia maradhi yanayosababishwa na virusi vya Covid – 19. Hadi sasa kuna aina kuu nne za chanjo za Covid-19 ambazo zimegundulika na kuanza kutumika duniani:
• Chanjo ambazo virusi vya Covid-19 vimeondolewa makali au kudhoofishwa. Hizi hutumia virusi vya corona ambavyo vimedhoofishwa na kutosababisha magonjwa lakini zinaweka kinga kwa mtumiaji.
• Chanjo zitokanazo na protini. Hizi hutumia vipande vya protini visivyo na madhara au ganda la protini ambalo hufanana na virusi vya Covid-19 ili kutoa kinga ya mwili.
• Chanjo za vekta za virusi. Hizi hutumia virusi salama ambavyo haviwezi kusababisha magonjwa lakini hutumika kama sehemu ya kutengenezea protini za virusi vya corona ili kutoa kinga.
• Chanjo zitokanazo na vinasaba (RNA na DNA). Hizi hutumia RNA au DNA iliyoundwa na vinasaba kutoa protini ambayo husababisha kinga ya mwili.
3. Kuna chanjo ngapi za Covid-19 zilizoidhinishwa kutumika hadi sasa?
Kuna chanjo 20 zilizoidhinishwa na angalau mamlaka moja ya udhibiti duniani kwa ajili ya matumizi kama ifuatavyo:
• Chanjo mbili za aina itokanayo na vinasaba (RNA) (Pfizer–BioNTech na Moderna).
• Chanjo tisa za virusi ambavyo vimeondolewa makali au kudhoofishwa (BBIBP-CorV, Chinese Academy of Medical Sciences, CoronaVac, Covaxin, CoviVac, COVIran Barakat, Minhai-Kangtai, QazVac, and WIBP-CorV).
• Chanjo tano za aina ya vekta za virusi (Sputnik Light, Sputnik V, Oxford–AstraZeneca, Convidecia na Janssen).
• Chanjo nne zitokanazo na protini (Abdala, EpiVacCorona, MVC-COV1901, Soberana 02 na ZF2001).
Kwa ujumla hadi sasa, kuna chanjo 330 ambazo ziko katika hatua mbalimbali za uvumbuzi ikiwa ni pamoja na 102 zilizo katika hatua ya utafiti, 30 katika majaribio ya awamu ya kwanza, 30 katika majaribio ya awamu ya pili, 25 katika majaribio ya awamu ya tatu na nane katika majaribio ya awamu ya nne.
4. Aina gani za chanjo zimeorodheshwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa matumizi ya dharura?
Hadi sasa WHO limeorodhesha aina nane tofauti za chanjo kwa matumizi ya dharura (EUL) kama ifuatavyo:
1. Pfizer/BioNtech – BNT162b2/COMIRNATY Tozinameran mtengenezaji akiwa ni Pfizer/BioNtech – Marekani/Ujerumani.
2. Astra Zeneca – AZD1222 mtengenezaji akiwa AstraZeneca –Uingereza.
3. Astra Zeneca – AZD1222 mtengenezaji akiwa ni AstraZeneca (MFDS KOREA) – Uingereza na Korea.
4. Covishield (ChAdOx1_nCoV-19) mtengenezaji ni Serum Institute of India Pvt. Ltd – India.
5. Janssen – Ad26.COV2.S mtengenezaji akiwa ni Janssen – subsidiary of Johnson & Johnson – Marekani.
6. Moderna – mRNA-1273 mtengenezaji akiwa ni Moderna – Marekani.
7. Sinopharm – SARS-CoV-2 Vaccine (Vero cell), inactivated (InCoV) Beijing mtengenezaji ni Bio-Institute of Biological Products Co Ltd – subsidiary of China National Biotec Group (CNBG)-China.
8. Sinovac – COVID-19 Vaccine (Vero Cell),
Inactivated/ CoronavacTM mtengezaj ni Sinovac -China
5. Ni chanjo zipi zimeidhinishwa na TMDA kwa matumizi nchini?
TMDA huidhinisha chanjo ambazo zimependekezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutumika nchini. Chanjo ambazo sasa zinaruhusiwa kutumika nchini Tanzania ni pamoja na:
i. Janssen – Ad26.COV2.S mtengenezaji akiwa ni Janssen – subsidiary of Johnson & Johnson–Marekani.
ii. Pfizer/BioNtech – BNT162b2/COMIRNATY Tozinameran mtengenezaji akiwa ni Pfizer/BioNtech – Marekani/Ujerumani.
iii. Moderna – mRNA-1273 mtengenezaji ni Moderna – Marekani.
iv. Sinopharm – SARS-CoV-2 Vaccine (Vero cell), inactivated (InCoV) mtengenezaji akiwa ni Beijing Bio-Institute of Biological Products Co Ltd – subsidiary of China National Biotec Group (CNBG)-China
v. Sinovac – COVID-19 Vaccine (Vero Cell), Inactivated/ CoronavacTM mtengenezaji akiwa ni Sinovac – China.
6. Idhini ya matumizi ya dharura (EUL) inamaanisha nini?
Idhini ya matumizi ya dharura (EUL) ni utaratibu uliowekwa na WHO wa kutathmini kama bidhaa mpya za afya zinafaa kwa matumizi wakati wa dharura.
Lengo ni kufanya dawa, chanjo na vitendanishi vipatikane kwa haraka iwezekanavyo ili kushughulikia dharura iliyojitokeza bila kuathiri ubora, usalama na ufanisi wake. Tathmini hupima uzito wa tishio linalosababishwa na dharura na faida inayoweza kupatikana kutokana na matumizi ya bidhaa hiyo dhidi ya athari zozote zinazoweza kujitokeza.
Njia ya EUL inajumuisha tathmini ya kina ya taarifa za majaribio ya bidhaa husika hasa katika hatua ya II na III na vilevile taarifa nyingine za ziada juu ya usalama, ufanisi, ubora na vihatarishi vyovyote kwa kuzingatia mahitaji ya nchi za kipato cha chini na cha kati. Takwimu hizi hupitiwa na wataalamu wa WHO wasiofungamana na upande wowote wanaozingatia ushahidi wa sasa juu ya chanjo inayotathminiwa, mipango ya ufuatiliaji wa matumizi yake na mipango ya tafiti au uchunguzi zaidi.
Kama sehemu ya mchakato wa EUL, kampuni inayozalisha chanjo husika ni lazima ikubali kuendelea kutoa taarifa zaidi kuwezesha kupitishwa na WHO. Mchakato wa uthibitishaji wa WHO unatathmini pia taarifa za ziada zitokanazo na majaribio ya chanjo na msingi wake ili kuhakikisha chanjo husika inakidhi viwango muhimu vya ubora, usalama na ufanisi kwa watumiaji.
7. Kuna faida gani za kupata chanjo?
Chanjo za Covid-19 hutengeneza kinga dhidi ya virusi vya SARS-CoV-2, hivyo kulinda mwili dhidi ya maradhi yanayosababishwa na ugonjwa wa Covid -19.
Kutumia chanjo hii kunapunguza uwezekano wa kupata ugonjwa na kusaidia kupambana na virusi na madhara yanayoweza kusababishwa navyo.
Kupata chanjo pia kunalinda watu walio karibu, kwa sababu ikiwa una kinga dhidi ya maambukizi kuna uwezekano mdogo wa kuambukiza mtu mwingine. Ni muhimu kulinda watu walio katika hatari kubwa ya kuugua ugonjwa wa UVIKO-19, kama watoa huduma za afya, watu wazima au wazee na watu wenye magonjwa sugu.
8. Mtu anaweza kupewa chanjo akiwa amekwisha kuambukizwa corona?
Hata ukiwa tayari uliwahi kuambukizwa Covid -19, unapaswa kuchanjwa kama chanjo inapatikana. Ulinzi ambao mtu anapata kutokana na kuwa na Covid-19 unatofautiana kati ya mtu na mtu, pia bado haifahamiki kinga ya asili inaweza kudumu kwa muda gani.
9. Ufanisi wa chanjo maana yake nini?
Ufanisi maana yake ni uwezo wa chanjo kupunguza ugonjwa kwenye kundi la watu waliochanjwa ukilinganisha na kundi la wasiochanjwa. Ufanisi hupimwa kwa kutumia majaribio yaliyofanywa kisayansi na kusimamiwa kwa karibu. Ufanisi ni tofauti na uwezo wa chanjo kuzuia magonjwa baada ya majaribio kukamilika kwa kuwa katika kipindi hiki chanjo huonyesha inavyofanya kazi inapotumiwa na idadi kubwa zaidi ya watu. Ufanisi hupimwa tu wakati chanjo inafanya kazi katika hali fulani ambayo pia hudhibitiwa sana. Ufanisi hutumika pia kupima mashambulizi ya magonjwa, watu waliolazwa, idadi ya wanaoumwa na gharama za afya.
10. Chanjo za Covid-19 zimeharakishwa na kuanza kutumika, je, kuna hatua zilizorukwa wakati wa kutengeneza chanjo hizi?
Hakukuwa na njia fupi wala kuharakisha matumizi ya chanjo hizi. Tafiti za kisayansi kwa wanyama na binadamu zimefanyika ili kuthibitisha usalama na ufanisi wake. Kwa ujumla angalau awamu tatu za tafiti zinapaswa kufanyika kwa watu weusi na matokeo yanapaswa kuonyesha usalama na ufanisi kabla chanjo haijaruhusiwa kutumika nchini Tanzania. Taarifa zilizowasilishwa na watengenezaji zimethibitisha kwamba tafiti hizo zilifanyika. Vilevile, TMDA ilishiriki katika tathmini ya pamoja ya chanjo hizi kupitia Muungano wa Mamlaka za Udhibiti wa Chanjo – Afrika (AVAREF) ulioandaa vikao kazi vya tathmini ya chanjo husika chini ya uratibu wa WHO.
11. Kuna haja ya kuchoma dozi zaidi ya moja na kwa nini?
Kwa mujibu wa matokeo ya tafiti yaliyopatikana hadi sasa, chanjo ya Janssen pekee ndio hutolewa kwa dozi moja wakati nyingine zinahitaji dozi mbili zinazotakiwa kutumika kati ya siku 21 au 28 kutegemeana na aina ya chanjo. Watafiti bado wanachunguza kama kinga inapungua baada ya kuchoma dozi zilizothibitishwa hadi sasa na kama kuna haja ya kuongeza tena. Mara tu tafiti zitakapokamilika, taarifa itatolewa kuhusu dozi ngapi zinatosha.
12. Mtu anaweza kupata tena corona baada ya kuchanjwa?
Mtu anaweza kupata tena corona baada ya kuchanjwa. Hii ni kwa sababu chanjo hizi hazina kinga ya asilimia 100 na bado utafiti unaendelea juu ya uwezo wa kuleta kinga ya muda mrefu na kupunguza maambukizi. Ndiyo maana tunapaswa kuendelea kujikinga na maambukizi sisi wenyewe na walio karibu yetu.
13. Kuna taarifa zimesambaa kwamba chanjo hizi zimewekewa sumaku na vifaa vya kuzuia mtu kupata mimba, je, taarifa hizi ni za kweli?
Taarifa hizi si za kweli na ni uzushi unaoenezwa pasipokuwa na ushahidi wowote. Haiwezekani chanjo zikawekewa sumaku au kifaa chochote cha kuzuia mtu kupata mimba. Chanjo ni kemikali za majimaji zinazoonekana kwa macho na haiwezekani kufanya hivyo. Taarifa hizo zinapaswa kupuuzwa na kuzuiwa zisienee ili kuwezesha chanjo ziweze kutumika kwa walio wengi, hivyo kuleta kinga ya ugonjwa wa corona.
14. Inawezekana mtu aliyepata chanjo kuweza kuambukizwa kwa mara nyingine?
Pamoja na kwamba chanjo za Covid-19 zimethibitika kuwa na usalama na ufanisi wa kuweza kuzuia watu kuugua sana na kulazwa hospitalini, bado hazijafikia asilimia 100 ya kinga. Hivyo basi, bado kuna asilimia ndogo ya watu waliopewa chanjo lakini wanaweza kupata corona.
Hii inasababishwa na mambo mbalimbali kama vile tabia ya chanjo yenyewe, umri wa mtu, hali ya kiafya, kama aliwahi kuugua Covid-19, maambukizi mapya au aina ya virusi vilivyoko nchini. Bado haijulikani kinga ya muda mrefu ya chanjo tofauti za Covid-19 itadumu kwa muda gani?
Kwa mantiki hii, hata kama chanjo za Covid-19 zinatolewa, lazima tuendelee kutumia mbinu zote za kiafya zinazofanya kazi kupunguza hatari ya maambukizi, kama vile kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu, kuvaa barakoa na kunawa mikono na maji tiririka.
Kwa siku 14 za kwanza baada ya kupata chanjo, kinga ndiyo inaanza kuongezeka taratibu. Kwa chanjo ya dozi moja, ulinzi kwa kawaida hutokea wiki mbili baada ya chanjo. Kwa chanjo za dozi mbili, dozi zote zinahitajika kufikia kiwango cha juu cha kinga inayokusudiwa.
Pamoja na kwamba chanjo hizi zimeonyesha ufanisi, bado TMDA inajifunza juu ya uwezo wa chanjo kuzuia maambukizi na kuleta kinga ya muda mrefu.
Kusaidia kujiweka salama wewe na wengine, endelea kuzingatia kukaa umbali wa mita moja kutoka kwa wengine, kufunika kwa kiwiko wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kusafisha mikono mara kwa mara kwa maji tiririka, kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko ya watu wengi na kukaa eneo lenye mzunguko mzuri wa hewa, pia hakikisha unasoma miongozo inayotolewa mara kwa mara na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
15. Ninaweza kutumia chanjo tofauti kutoka kwa wazalishaji tofauti kwa wakati mmoja?
Bado hakuna taarifa za kutosha kupendekeza mchanganyiko huu. Tafiti zinaendelea kufanyika kuangalia kama mtu anaweza kuchomwa dozi ya chanjo moja, kisha kuchomwa dozi ya chanjo nyingine.
16. Chanjo hizi zinaweza kuwalinda watu dhidi ya aina zote za virusi vya corona?
Utafiti zaidi unahitajika kufanyika ili kutathmini ufanisi wa chanjo za sasa za corona dhidi ya mabadiliko ya virusi. Kwa taarifa zilizopo, inaonekana chanjo nyingi huleta kinga ya kutosha dhidi ya aina za virusi vilivyoko, hasa katika kupunguza makali ya ugonjwa, kulazwa hospitalini na vifo.
Tafiti bado zinaendelea kuangalia aina ya virusi na namna vinavyojibadilisha ili kufanya mabadiliko ya chanjo kuweza kuendelea kuleta kinga kwa watu wengi. Kwa hali ilivyo sasa, idadi kubwa ya aina za virusi vilivyoko vinaweza kuzuiwa na chanjo zilizoko kusababisha ugonjwa mkali.
17. Baada ya kuchanjwa tunapaswa kuendelea kujitenga, kusafisha mikono na kuvaa barakoa tena, kwa nini?
Chanjo zimekuja kusaidia katika mapambano dhidi ya corona. Pamoja na kwamba chanjo hizi zipo kwa sasa, tunapaswa kuendelea kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka, kukaa eneo lenye hewa nzuri, kuzingatia umbali na kujiepusha na mikusanyiko.
18. Kinga ni ya muda gani baada ya kuchanjwa?
Si chanjo zitakazodhibiti ugonjwa bali uchanjaji. Wizara kupitia IVD inafanya kazi kuhakikisha upatikanaji wa chanjo kwa haki na usawa, na kuhakikisha kila mtu anapata kinga kwa kuanzia na walio hatarini zaidi. Hata hivyo, ikumbukwe kuwa kupata chanjo si lazima, ni hiari kwa watu ambao wako tayari kuchanjwa.
Kwa sababu chanjo za corona zimetengenezwa hivi karibuni tu, ni mapema kujua muda wake wa kinga. Utafiti unaendelea kujibu swali hili. Hata hivyo, inatia moyo kwamba taarifa zinazopatikana zinaonyesha kuwa watu wengi wanaopona corona hutengeneza kinga ambayo hutoa angalau kipindi fulani cha ulinzi dhidi ya kuambukizwa tena, ingawa wanasayansi bado wanajifunza jinsi ulinzi huu ulivyo, nguvu yake na inachukua muda gani.
19. Chanjo za corona ni salama kwa matumizi ya binadamu?
Kama chanjo yoyote ilivyo, chanjo za corona zinaweza kusababisha athari chache, za muda mfupi, kama vile homa ya kiwango cha chini, maumivu au ngozi kuwa nyekundu eneo ulipochomwa sindano. Athari hizi ni za kawaida na huisha baada ya siku chache. Madhara makubwa au ya kudumu ya chanjo yanawezekana lakini ni nadra sana kutokea. TMDA inaendelea kufuatilia usalama wa chanjo hizi ili kuangalia madhara yanayoweza kujitokeza baada ya matumizi ya muda mrefu kwa lengo la kulinda afya ya jamii.
Madhara yaliyoripotiwa hadi sasa ni ya wastani na yanajumuisha homa, uchovu, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, baridi, kuhara na maumivu kwenye sehemu palipochomwa sindano. Madhara haya yanatofautiana na aina ya chanjo.
Madhara haya yanatibika kwa kupumzika, kunywa maji mengi na kutumia dawa zenye paracetamol au acetaminophen. Ikiwa madhara yatazidi saa 24, watumiaji wawaone wataalamu wa afya kwa uchunguzi zaidi.
Endapo mtu atapata shida ya kupumua, maumivu ya kifua, kuchanganyikiwa, kushindwa kuongea au kushindwa kutembea, ni vema kuwahi kituo cha afya kilicho karibu kwa msaada zaidi.
20. Chanjo za mRNA ni salama? Ikiwa zinatengenezwa kwa teknolojia mpya, tunawezaje kuwa na uhakika?
Chanjo za corona za mRNA zimechunguzwa kwa teknolojia ya hali ya juu na kuthibitika kuwa na ufanisi wa kuzuia ugonjwa wa Covid-19.
Teknolojia ya kutengeneza chanjo za mRNA imetumika miaka mingi na imehusisha pia uvumbuzi wa chanjo nyingine kama za ugonjwa wa zika, kichaa cha mbwa na mafua. Chanjo za
mRNA hazina virusi vya corona na haziingiliani na DNA ya binadamu.
21. TMDA itafuatiliaje usalama wa chanjo hizi?
TMDA ina mifumo miwili ya ufuatiliaji wa bidhaa kwa ajili ya kuhakikisha usalama wake. Hii ni pamoja na ufuatiliaji wa hiari na ule wa karibu.
Mfumo wa ufuatiliaji usalama wa hiari hutumia fomu za njano (kwa watoa huduma za afya) na fomu za kijani (kwa wagonjwa) kuripoti madhara ya dawa na chanjo (ADRs).
Njia ya ufuatiliaji wa karibu (CEM) hutumia fomu maalumu zilizoandaliwa kutegemeana na aina ya ugonjwa na dawa inayotumika. Njia ya CEM hutumiwa kwa dawa na chanjo mpya zilizoingizwa ikiwa ni pamoja na zile zinazotumiwa na watu wengi.
TMDA itatumia njia ya CEM kufuatilia usalama wa chanjo za UVIKO-19 ili kurekodi matukio yote pamoja na madhara ya muda mrefu ya chanjo.
Pamoja na hayo, mfumo wa kuripoti madhara kwa hiari pia utatumika ili kutambua madhara mengine yote yanayoweza kujitokeza wakati chanjo hizi zinatumika hapa nchini. Ufuatiliaji utafanywa kwa kushirikiana na Mpango wa Chanjo wa Taifa (IVD) ambao uko chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
22. Mtu anapaswa kuripoti madhara ya kiafya yanayotokea baada ya chanjo na nini kitatokea ikiwa tukio baya litaripotiwa?
Kama ilivyo kwa chanjo nyingine, TMDA inafuatilia kwa karibu usalama na ufanisi wa chanjo zote zinazotumika katika programu za chanjo. Ikiwa shida ya kiafya itaripotiwa kufuatia matumizi ya chanjo, uchunguzi wa kina hufanywa na TMDA kwa kushirikiana na IVD. Fomu za CEM za kukusanya taarifa za usalama wa chanjo za Covid – 19 zitatumika (zinapatikana www.tmda.go.tz).
Hata hivyo, ni nadra kukuta shida za kiafya zinazotokea baada ya kuchanjwa kuthibitika kuwa kweli husababishwa na chanjo yenyewe. Shida za kiafya kufuatia chanjo mara nyingi hutokea kwa bahati mbaya na mara nyingi hazihusiani moja kwa moja na chanjo.
Wakati mwingine zinahusiana na jinsi ambavyo chanjo husika imehifadhiwa, kusafirishwa au kusambazwa.
Makosa yanayohusiana na utoaji wa chanjo yanapaswa kuzuiwa kwa kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya pamoja na kuimarisha mnyororo wa usambazaji. Hata hivyo, endapo madhara ya chanjo yatatokea, TMDA itachukua hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Uchunguzi zaidi utafanyika pia ili kubaini ni nini hasa kilichosababisha madhara hayo na hatua za kurekebisha zitawekwa.
23. Kuna tahadhari zozote za kuchukua kabla ya kutumia chanjo hizi?
Chanjo za corona ziko salama kwa watu wengi wenye umri wa miaka 18 na zaidi, ikiwa ni pamoja na wenye magonjwa mengine kama vile shinikizo la damu, kisukari, pumu, mapafu, homa ya ini na ugonjwa wa figo.
Pamoja na hilo, mtumiaji atapaswa kuchukua tahadhari ikiwa ana upungufu wa kinga mwilini, mtu ana ujauzito au kunyonyesha, ana historia ya mzio, hasa kwa chanjo husika au viambata vyake au ana udhoofu wa mwili.
24. Tunaweza kuacha kuchukua tahadhari baada ya chanjo?
Chanjo inatoa kinga dhidi ya kupata maambukizi makali na kifo. Kwa siku 14 za mwanzo baada ya kupata chanjo, mtu hatakuwa na kiwango kikubwa cha ulinzi, kwa kuwa huongezeka taratibu. Kwa chanjo za dozi moja, kinga kwa kawaida itatokea wiki mbili baada ya chanjo. Kwa chanjo za dozi mbili, dozi zote zitahitajika ili kufikia kiwango cha juu cha kinga inayotakiwa.
Wakati chanjo ya corona itakukinga na maambukizi makali na kifo, bado tunajifunza juu ya kiwango gani kitakuzuia kuambukizwa na kusambaza virusi kwa wengine. Takwimu kutoka nchi nyingine zinaonyesha kuwa chanjo zinazotumika sasa zinalinda dhidi ya hali ya ugonjwa mkali na kulazwa hospitalini. Hata hivyo, hakuna chanjo yenye ufanisi wa asilimia 100.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na TMDA bado tunaendelea kufuatilia mabadiliko ya aina ya virusi vilivyopo nchini na uwezo wa muda mrefu wa chanjo zilizovumbuliwa. Kwa sababu hizi, na kwa kuwa wengi katika jamii bado hawataweza kupata chanjo, kuendeleza hatua nyingine za kuzuia ni muhimu hasa katika jamii ambazo mzunguko wa virusi ni mkubwa.
Ili kukusaidia wewe na wengine kuwa salama, na wakati juhudi zinaendelea kupunguza maambukizi ya virusi na kuongeza chanjo, unapaswa kuendelea kuzingatia kukaa umbali wa mita 1 kutoka kwa wengine, kukohoa au kupiga chafya kwenye kiwiko chako, kusafisha mikono yako mara kwa mara, kuvaa barakoa, kuepuka misongamano na kukaa maeneo yenye mzunguko mzuri wa hewa. Wakati wote fuata miongozo inayotolewa na Wizara na IVD kulingana na hali na hatari ya mahali unapoishi.
25. Chanjo ya corona inatolewa kwa watoto wa umri gani?
Chanjo ya corona haitolewi kwa watoto bali kwa wenye umri unaoanzia miaka 16. Umri huu ndio imethibitika kuna maambukizi mengi ya ugonjwa wa Covid-19 na tafiti za usalama na ufanisi wake zimefanyika kuanzia kundi hili hadi miaka zaidi ya 60.
26. Mtu akiwa na Covid -19 anaweza kuchangia damu?
Mtu mwenye UVIKO-19 anayetaka kuchangia damu ni vema kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanya hivyo.
27. Watu wa vijijini watapataje chanjo?
Chanjo ya UVIKO-19 imeanza kutolewa kwenye vituo ambavyo vimeainishwa kupitia IVD iliyoko chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Ni vema kufika vituo vya kutolea huduma za afya ili kufahamu mahali chanjo inapotolewa.
28. Chanjo ni njia inayotumiwa na mataifa makubwa kupunguza idadi ya watu na ilitengenezwa kwa ajili ya kupunguza watu duniani?
Chanjo ya Covid -19 imetengenezwa kwa lengo la kuleta kinga dhidi ya corona, si kuangamiza watu. Kuna chanjo nyingi pia zilizotengenezwa na mataifa hayo hayo makubwa na hadi leo haziui watu bali zinakinga watu dhidi ya magonjwa mbalimbali kama vile surua, tetekuwanga, polio, tetenasi, kichaa cha mbwa, saratani ya shingo ya kizazi, homa ya ini na kadharika. Huu ni uvumi tunaopaswa kuuacha ili tuweze kuwalinda Watanzania wasipate maambukizi ya ugonjwa mkali wa Covid-19.
29. Kama unatarajia kupata ujauzito bado unaweza kupata chanjo?
Kwa tafiti ambazo zimefanyika hadi sasa, chanjo ya Covid-19 haijaonekana kuleta madhara kwa mjamzito wala mtu anayetarajia kubeba ujauzito. Hata hivyo tafiti zinaendelea kufanyika kuona kama zinaleta madhara kwa wajawazito baada ya matumizi ya muda mrefu.
30. Nani anadhibiti chanjo Tanzania?
Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura 219 imeipa mamlaka TMDA kudhibiti chanjo za binadamu na mifugo pamoja na chanjo za Covid-19. Udhibiti unahusisha usajili wa chanjo, udhibiti wa uingizaji nchini na usafirishaji nje ya nchi, ufuatiliaji ubora na usalama katika soko, ukaguzi, utoaji leseni za majengo yanayojihusisha na masuala ya chanjo, uchunguzi wa kimaabara na udhibiti wa majaribio ya chanjo.