Taarifa za uongo za hivi karibuni zilizosambaa kueleza kuwa Mama Maria Nyerere ameaga dunia zimeibua maswali kuhusu wajibu na umakini wa baadhi ya watu wanaotumia teknolojia ya habari na mawasiliano.
Aliyeanzisha uongo huo ni dhahiri alifahamu kuwa anaandika uongo kwa sababu hakujitambulisha, na tunafahamu kuwa waongo siku zote hupendelea kujificha. Alichofanikiwa kufanya ni kuwapa hofu ndugu, jamaa, marafiki, na watu wengine wengi ambao waliamini kuwa ni taarifa za kweli.
Moja ya mbinu za kufundisha waandishi wa habari wa uchunguzi kupata ukweli wa habari na kubainisha nani anaweza kuwa mhusika mkuu wa tukio fulani ni kuorodhesha watu au taasisi zinazoweza kufaidikia kimapato na tukio hilo.
Ingekuwa kampuni za simu zina shida kubwa ya pesa tungeweza kusema kuwa kampuni za simu zingeweza kuzusha habari hizi za uongo kwa kutarajia kuwa habari hizo zingesababisha watu wengi waanzishe mawasiliano baina yao na, kwa gharama zile za mawasiliano, kampuni zingeongeza mapato. Lakini siamini hata kidogo kuwa kampuni za simu zinaweza kuwa na shida kubwa kiasi hicho cha pesa mpaka kumzushia mtu kifo ilimradi waongeze mauzo yao.
Kama hayajakutokea, huwezi kuona kama ni tatizo. Miezi kadhaa iliyopita nilisoma uzushi mwingine wa aina hii ukimhusisha kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu, na sikulichukulia uzito sana hadi lilipotokea hili la Mama Maria. Lakini kama ambavyo nilisema kwenye mahojiano na kituo kimojawapo cha redio wakati wa tukio la hivi karibuni, mtu au watu wanaotuma ujumbe wa aina hii hawakumbuki au hawajali kuwa wanaemzushia uongo huu ni mtu ambaye ana watoto, wajukuu, marafiki, ndugu zake, na watu wengine wengi ambao watapata mshituko kusikia habari hizo, kama ambavyo mzushi huyo angepata mshituko kusikia taarifa za msiba wa mtu aliye karibu naye.
Nimewahi kufanya utafiti mdogo kwenye jukwaa moja la mtandao na kuuliza umri wa wale ambao wakati ule walikuwa wanatumia jukwaa lile. Wengi wao walikuwa vijana wa chini ya umri ya miaka 20, lakini umri wa wastani kwa sehemu kubwa zaidi ulikuwa miaka 15.
Niliamini wakati huo na sasa hivi kuwa watumiaji wengi wa mtandao ni vijana ambao uzoefu mfupi wa maisha unawatuma kuchukua uamuzi ambao hawaoni athari zake.
Naandika makala hii nikiamini kuwa nazungumzia tukio la uzushi ambalo yawezekana limesababishwa na mtu mzima, lakini natambua pia kuwa inawezekana sana kuwa ni tukio ambalo limeibuka kwa kijana ambaye hajafikisha umri wa kutambua tofauti ya utoto na utu uzima, tofauti ya busara na upuuzi, tofauti ya uungwana na ufedhuli. Kama ni mtu mzima aliyezusha haya, basi naye tunamweka kwenye kundi la utoto.
Mtu mwenye akili timamu akijiuliza kwa nini habari za aina hii zinaweza kutolewa hawezi kupata jibu la kuridhisha. Lakini tunaweza kupata jibu kwenye masuala matatu: kuenea kwa uwezo wa kila mtu kutoa habari kutokana na kutapakaa kwa teknolojia ya mawasiliano kwa njia ya simu za kiganja, uwezekano wa mtumiaji wa teknolojia hii kutoa taarifa bila kufahamika utambulisho wake mara moja, na utambuzi wa baadhi ya watumiaji wa teknolojia hii kuwa simu ya kiganja ina uwezo mkubwa wa kutoa taarifa kwa ulimwengu.
Kuwapo kwa masuala haya matatu, pasipo kuwapo pia uadilifu na busara za mtumiaji; ndiyo kunasababisha taarifa za aina hii.
Njia rahisi ya kusisitiza ukubwa wa tatizo hili ni kutamka kuwa ulimwengu wa zamani ulikuwa na waandishi wa habari ambao wamepitia mafunzo ya uandishi yaliyosisitiza kufuata maadili ya uandishi na walifanya hivyo kwa kiwango kikubwa. Lakini ulimwengu wa sasa una mabilioni ya raia wa kawaida ambao teknolojia ya mawasiliano imewapa uwezo wa kuandika wanachotaka – hata uongo – bila kuwa wamepitia mafunzo yanayoweka bayana umuhimu wa kuheshimu maadili ya uandishi.
Ni sawa sawa na kumpa silaha mtu ambaye hajaenda mafunzo ya kijeshi. Akiona jani linatikiswa na upepo, anaweza kulifyatulia risasi.
Kibaya zaidi kwenye hali hii ya hatua hii kubwa ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni kuwa mtu anaweza kuzusha habari bila yeye mwenyewe kujulikana kwa urahisi, ingawa tunaambiwa kuwa Tume ya Mawasiliano inao uwezo wa kufanya uchunguzi na kubaini ujumbe kama ule ulianza kwa nani hadi ukasambaa kwa watu wengine.
Nadiriki kuongeza kuwa mtu ambaye analazimika kutumia muda wake mrefu kufanya kazi hawezi kuwa na muda wa kutunga uongo kama huu. Kazi ya kweli inafanya mwanadamu atumie akili yake kujiletea maendeleo yeye mwenyewe na jamii inayomzunguka na mtu huyo huyo anakuwa na kiwango kikubwa zaidi cha uwajibikaji kuliko mtu ambaye hana kazi ya uhakika. Uwepo wa ajira hautamaliza tatizo hili, lakini unaweza kulipunguza kwa kiasi fulani.
Naunga mkono jitihada zote zinazozuia matumizi mabaya ya teknolojia ya habari na mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika. Sidhani kama naweza kumshawishi Mama Maria kulalamika kwa vyombo husika ili hatua hizo kali zichukuliwe dhidi ya wale waliozusha habari hizi juu yake. Hata hivyo, tukio hili lituamshe kuchukua tahadhari na habari zote tunazozipata, na kuchunguza taarifa tunazopokea kwa sababu mitandao ya mawasiliano inatoa mwanya wa kusambaza habari ambazo siyo za kweli.
Hatuna uwezo wa kubaini kuwa huko tuendako ni uongo wa aina gani ambao tutausikia tena na ambao una uwezo mkubwa kiasi gani kutuathiri kama Taifa. Inawezekana mtu au watu kuzusha taarifa zenye uwezo wa kuhatarisha amani na usalama wetu kama raia, na hata kuchonganisha makundi ya Watanzania na kuwajengea uhasama baina yao.
Sababu hii peke yake inatosha kupiga vita kwa nguvu zote tabia hii ambayo inao uwezo mkubwa wa kubomoa badala ya kujenga. Tunao wajibu mkubwa, kama raia, kushawishi matumizi bora ya teknolojia ya habari na mawasiliano.