MAPUTO, Msumbiji
Bataliani ya jeshi la Rwanda inaripotiwa kutinga kaskazini mwa Msumbiji na kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya kikundi cha kigaidi kinachoua hovyo raia.
Ndani ya wiki mbili tu, kikosi hicho cha kwanza kutoka nje ya nchi kupelekwa kupambana na magaidi – tayari kimeteka na kudhibiti maeneo muhimu yaliyokuwa yakikaliwa na magaidi kwa mwaka mzima; na kimefika katika mji wa Bandari ya Mocímboa da Praia.
Kwa miaka minne waasi hao wamekuwa wakidhibiti eneo kubwa la wilaya tano za Jimbo la Cabo Delgado, kaskazini mashariki mwa Msumbiji.
Hadi sasa walau watu 3,100 wameuawa na wengine 820,000 wameyakimbia makazi yao – ikiwa ni zaidi ya wakazi wa eneo hilo.
Wakati waasi hao walipouteka mji wa Palma mwezi Machi mwaka huu, eneo ambalo Kampuni ya Total imewekeza mabilioni ya fedha kulifanya kuwa la pili Afrika kwa uchimbaji wa gesi asilia, kampuni hiyo kubwa Ufaransa ilisitisha shughuli zake.
Jeshi la Msumbiji linachukuliwa kuwa dhaifu, lililojaa ufisadi, likiwa na mafunzo duni bila zana muhimu za kivita, hivyo kushindwa kuwadhibiti waasi hao.
Pamoja na upinzani kutoka ndani ya chama chake, Rais Filipe Nyusi ameamua kuomba msaada Rwanda.
Inadaiwa kuwa uasi huo umeanzishwa na vijana wasio na kazi wakipinga kuongezeka kwa umaskini na kukosekana kwa usawa, pamoja na kutopata chochote kitokanacho na rasilimali za madini ya rubi na gesi.
Yote hayo yanajumuishwa katika ukandamizaji unaofanywa na maofisa wa serikali, polisi na wanajeshi.
Mgogoro ulianza kwa shambulio la mwaka 2017 katika mji wa Mocímboa da Praia na ukapamba moto baada ya vijana kuwanyang’anya silaha wanajeshi na kuungwa mkono na wananchi.
Kuna uhusiano na IS?
Waasi hawa wanajiita ‘al-Shabaab’, maana yake ‘vijana’, ingawa kwa kweli hawana uhusiano na kundi la Somalia lenye jina kama hilo.
Wakazi wengi wa eneo hilo kaskazini mwa Msumbiji ni Waislamu, na mwaka 2019 waasi walifanya mawasiliano na kundi la kigaidi la Islamic State (IS).
Marekani inawaita ‘IS wa Msumbiji’ na wanatambulika kama kundi la kigaidi.
Lakini waasi hawa hawana uhusiano wowote wa dini na wanachodai wao ni kwamba wanapigania taifa lao; na zana wanazotumia katika mapambano ni zile walizoteka kutoka majeshi ya Msumbiji.
Taasisi ya Kimataifa ya Migogoro (IGC) inasema waasi hao wana uhusiano mdogo sana na IS na kwamba kichocheo kikubwa katika mgogoro huo ni maudhi na malalamiko ya wenyeji.
“Hakuna atakayepeleka askari Msumbiji kupambana na wenyeji wenye njaa, lakini wengi wapo tayari kupeleka majeshi kupambana na IS,” wanasema IGC.
Askari wa Ureno, wakoloni wa zamani wa Msumbiji na Marekani wamo nchini humo wakitoa mafunzo kwa jeshi jinsi ya kupambana na waasi.
Jirani mkubwa wa Msumbiji, Afrika Kusini, wamo katika shinikizo la SADC kupeleka majeshi nchini humo.
Lakini Msumbiji ina historia tofauti na mataifa hayo matatu na isingependa kushirikiana nayo.
Kimbilio pekee ni Rwanda, yenye jeshi lenye weledi mkubwa.
Siku 10 tu baada ya Rais Nyusi kukutana na Paul Kagame wa Rwanda Aprili – timu ya mashushushu wa jeshi la Rwanda wakatua Cabo Delgado.
Taarifa za kidiplomasia zinasema kwamba Marekani inaunga mkono suala hilo. Rwanda ina uhusiano imara na Israel, ambao wataunga mkono operesheni dhidi ya IS.
Mara baada ya majeshi ya Rwanda kuanzisha mapambano, maofisa maalumu wa SADC nao wameruhusiwa.
Meli na ndege za Afrika Kusini zimewasili Pemba karibu na uwanja wa mapambano huku bataliani ya askari 1,500 wa Afrika Kusini yenye zana za kisasa za kivita zikielekea Msumbiji.
Bataliani hiyo ina askari kutoka kikosi maalumu, ‘43 Brigade’. Magari ya kivita na askari 300 wa Botswana tayari yameshavuka mpaka kuingia Msumbiji.
Hofu ya wadunguaji
Rwanda inasema majeshi yake yataendelea kuwapo Msumbiji kwa muda mrefu kadiri itakavyohitajika, na wanatarajia kutengeneza eneo salama kuzunguka Palma na maeneo yenye mitambo ya gesi.
Kwa kufanya hivyo kutarejesha imani kwa Total na kurejea kazini mwaka kesho.
Kwa kuanzia, majeshi ya Afrika Kusini yatakuwapo Msumbiji kwa miezi mitatu tu. Wanajeshi 3,000 wakisaidiwa na majeshi ya anga na majini yatafanya kazi ya haraka kukomboa barabara, miji na Bandari ya Mocímboa da Praia.
Lakini tayari waasi wameshaziacha ngome zao na sasa wapo katika vikundi vidogo vidogo, kama ambavyo hufanyika mara nyingi kwa wapiganaji wa vita ya kuvizia wanapojikuta kwenye mbinyo. Maeneo mengi ya uwanja wa mapambani ni mapori makubwa yanayotoa nafasi nzuri kujificha.
Pia eneo hilo lina barabara ndefu zenye upweke zinawapa wadunguaji nafasi nzuri sana, na kwa miaka saba iliyopita, Renamo – kundi la upinzani lenye jeshi na uwakilishi bungeni – limethibitisha namna wadunguaji wachache wanavyoweza kusababisha vurugu kwa kufunga barabara kuu mara kwa mara.
Na iwapo ni kweli waasi wana uhusiano na IS, basi wanaweza kutuma fedha, silaha na wanaojitoa mhanga, hivyo kusababisha mapambano kuongezeka. Vita hii haitamalizika kwa sasa.
Mapema mwaka huu, Amnesty International iliwalaumu waasi pamoja na serikali kwa ‘uhalifu wa kivita’, hivyo watu wengi watapatwa na hofu wakati jeshi na Polisi wa Msumbiji watakaporejea. Waasi ni wenyeji wa maeneo hayo wanaofahamika kwa jamii.
Mwaka jana walifanikiwa kuiteka miji ya Palma na Mocímboa da Praia kwa kupeleka watu wanaofahamika katika miji hiyo kuishi na familia zao au wanaowaunga mkono.
Ni nadra sana kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe kumalizwa kijeshi. Ni lazima kwanza malalamiko yapatiwe ufumbuzi.
Mahojiano na watu waliokamatwa na waasi na baadaye kuachiwa huru yanathibitisha kwamba wengi wako huko kutafuta fedha na kuiba, na kwamba wangeweza kuachana na uasi iwapo watapewa kazi nzuri.
Maelfu kidogo tu ya nafasi za kazi yatamaliza vita.