TUNDURU
Na Mwandishi Wetu
Wananchi zaidi ya 400 wa Tunduru mkoani Ruvuma wanaulaumu Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma kwa kuhujumu fidia walizostahili kulipwa baada ya kupisha mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.
Wananchi hao wanawalaumu pia viongozi wa wilaya na mkoa kwa kushindwa kuwapigania wapate fidia hizo, badala yake wanashirikiana na Wakala kuendeleza kile wanachoamini kuwa ni hujuma dhidi yao, ikiwamo hofu kwamba fedha zilizotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), zimetafunwa na vigogo kadhaa.
Awali wananchi wa vijiji vya Sautimoja, Tunduma mjini, Nakapanya, Muhwesi, Mkwela, Songambele, Namakambale, Mtonga, Majimaji, Chingulungulu na Msagula walilieleza JAMHURI kuwa walihisi kuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ndiyo iliyokwamisha wao kulipwa fidia za kupisha mradi huo.
“Kuna watu wamevuruga makusudi mchakato wa ulipaji fidia ili wajinufaishe wao wenyewe, haiwezekani mwaka 2018 Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itujibu kwamba hatustahili kulipwa fidia ilhali mwaka 2013 ilishirikiana na TANROADS pamoja na viongozi wa Serikali ya Mkoa kuweka wazi kuwa tunastahili kulipwa kwa mujibu wa sheria,” anasema Gerald Haule, mkazi wa Nakapanya, ambaye ni miongoni mwa waathirika walioharibiwa mali wakati wa kupisha mradi huo.
Ikumbukwe kuwa mradi wa ujenzi wa barabra ya Mangaka – Tunduru ulianza kutekelezwa mwaka 2011, ambapo serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) waliingia makubaliano ya kujenga kilomita 137 za barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Benki ya AfDB walitoa dola za Marekani milioni 210 sawa na asilimia 64.79 huku JICA wakichangia asilimia 32.83 na Tanzania asilimia 2.38 ambavyo katika fedha hizo pia yanatajwa kuwamo malipo ya fidia kwa wananchi kupisha mradi.
Wakazi wa vijiji hivyo wanasema kasoro za mwanzo zilianza kujitokeza baada ya TANROADS Mkoa, Novemba 4, 2011 kutoa notisi ya siku 21 ikiwataka waliojenga kwenye hifadhi ya barabara kuvunja nyumba zao kwa hiari na kwamba ambaye angekiuka agizo hilo angevunjiwa kwa nguvu na kuilipa serikali.
Notisi yenye Kumb. Na. TANROADS.RUV.R1/101 iliitikiwa kwa nguvu ambapo baadhi ya wananchi walivunja nyumba zao kwa hiari bila hata kusubiri kufanyiwa tathmini.
Hata hivyo, kuna notisi nyingine ilitolewa Januari 21, 2013 ikiwataka wananchi kusitisha ubomoaji ili tathmini ya mali ifanyike.
Notisi yenye kumb. Na. TANROADS/RUV/R1/86/ VOL.II / 87 ilibainisha kuwa TANROADS wanafanya upya tathmini ya mali za wananchi kubaini ni wananchi wangapi watakaoguswa na mradi wa barabara.
Akizungumzia chanzo cha wao kutolipwa fidia, mkazi wa Kijiji cha Muhwesi, Fakii Kayombo, anasema: “Walikuja maofisa kutoka TANROADS Taifa wakafanya vipimo kutoka katikati mwa barabara hadi kwenye maeneo ya wananchi.
“Baadhi yetu ambao hatukuwa tumebomoa na kuondoa mali zetu kwa hiari tulipigwa picha tukiwa kwenye nyumba na vibanda vyetu vya biashara.
“Tulielezwa kwamba wale waliobomoa kwa hiari wasingelipwa fidia kwa sababu hawakufanyiwa tathmini lakini kwa ambao hatukuwa tumebomoa tulielezwa kuwa lazima tungelipwa.”
Anasema shida ilianza baada ya TANROADS Taifa kurudisha idadi ya majina ya wananchi waliotakiwa kulipwa fidia huku wengi wakishindwa kuyaona majina yao katika orodha iliyopelekwa.
Kayombo anasema majina ya waliobandikwa kwenye mbao za matangazo katika ofisi za vijiji na majina ambayo hayakubandikwa yalikuwa na vigezo sawa vya kulipwa.
Anasema kitendo hicho kilisababisha wao kuanza kuhoji ndipo waliambiwa waandike barua za malalamiko na zifikishwe kwa mkuu wa wilaya wapate majibu.
“Tuliofikisha malalamiko yetu kwa DC ni wale tuliokuwa tumefanyiwa tathmini tu! Lakini tulishangazwa na Katibu Tawala wa Wilaya, naye alipita vijijini akihimiza hata ambao walibomoa kwa hiari yao nao wapeleke malalamiko kwake,” anasema Kayombo.
Twalibu Alabi wa Kijiji cha Nakapanya, anasema mwaka 2016 wakati wanafuatilia kwa DC suala la wao kulipwa fidia walikutana na mwakilishi kutoka AfDB akawaeleza kuwa fedha iliyotolewa na benki hiyo ilijumuisha suala la ulipaji fidia, hivyo wasiwe na wasiwasi; watalipwa.
Alabi anaongeza kuwa Machi 3, 2016 aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Edwin Ngonyani, alifanya mkutano Nakapanya na kuwaagiza viongozi wa Wilaya ya Tunduru kuhakikisha wananchi wanaodai fidia wanalipwa.
Hata hivyo, anasema agizo la naibu waziri huyo halikufanyiwa kazi hadi Oktoba 2016 waliporudi maofisa kutoka TANROADS Taifa na kufanya mkutano na wananchi wa Nakapanya na kuwaeleza kuwa waathirika wa mradi huo wamegawanyika katika makundi manne.
Walieleza kuwa kundi la kwanza ni waliobomolewa na kuondoa mali zao bila kupata notisi na kufanyiwa uthamini na kwamba watu hao hawatalipwa fidia yoyote.
Kundi la pili, maofisa hao walisema ni kundi la waliopewa notisi lakini walivunja nyumba zao na kuondoa mali zao na kwamba watu hao wangefikiriwa kupata japo kifuta machozi.
Kundi la tatu lilitajwa kuwa la waliofanyiwa uthamini na wamelipwa fidia lakini wakazidi kulalamika kulipwa fedha chache, kundi hilo lilielezwa wazi kuwa hawatalipwa tena.
Na kundi la nne walilitaja kuwa kundi la wenye haki ya kulipwa, ambao walielezwa kuwa fedha zao zipo lakini kompyuta iliruka majina yao baada ya kuukosea mfumo wakati wa kuandaa malipo.
Alabi anasema hata baada ya ufafanuzi huo hakuna kilichofanyika, hali iliyowalazimu baadhi ya wananchi kufunga safari hadi Dar es Salaam kupata majibu stahiki.
“Tulifika wizarani lakini tukaambiwa twende TANROADS ndio wenye majibu sahihi. Tulipofika TANROADS walitueleza wako tayari kulipa na wanawajua wanaostahili kulipwa, tatizo wizara haijawapa fedha za malipo ya fidia hizo,” anasema Alabi.
Alabi anasema walishangazwa na timu ya wataalamu kutoka wizarani iliyofika Tunduru Julai 31, 2017 wakidai kwenda kuhakiki majina ya wanaodai fidia.
Anasema timu hiyo iliyoongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru ilikuwa na watu wanane ambao ni Mhandisi Martin Mtemo, Mhandisi Hashim Kabanda, Veronica Najima na Daniel Kipagile, wote kutoka Wizara ya Ujenzi.
Wengine ni Julius Luhuro kutoka TANROADS Dar es Salaam, Mhandisi Fanuel Msangi kutoka TANROADS Ruvuma, Amos Malemula kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma pamoja na Geofrey Mgode; Mthamini wa Wilaya ya Tunduru.
Anasema timu hiyo ilifanya mikutano katika vijiji vyote na wanaodai fidia waliitwa majina na kusainishwa nyaraka ambazo zilikuwa na majina yao.
“Tulihoji kwanini wamekuja kutusainisha majina wakati hatujapokea malipo, wao wakatujibu kuwa wanafanya hivyo kufahamu idadi ya wanaodai, pia kupata uhakika kwani wanaogopa kufanya malipo hewa,” anasema Alabi na kuongeza kuwa baada ya hapo waliambiwa kuwa majina yao yangefikishwa Ofisi ya Rais ili Rais aidhinishe fedha walipwe.
Baada ya kusaini, Alabi anasema walishangaa baada ya siku kadhaa kupokea taarifa kutoka Ofisi ya DC kwamba hawapaswi kulipwa.
Anasema walivyofuatilia taarifa hiyo kwa DC aliyekuwapo kipindi hicho naye aliwaambia kuwa hiyo ni taarifa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Wananchi kadhaa walilazimika kufika kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambapo naye aliwaeleza kuwa barua ya wao kutolipwa imetoka wizarani.
“Tulimuomba RC atupatie nakala ya barua inayoeleza kwamba hatustahili kulipwa, akatujibu ikiwa hatujaridhishwa na uamuzi wa wizara, twende mahakamani tukatafute haki,” anasema Alabi.
Baada ya majibu hayo wananchi hao walifanya mkutano na kuchagua viongozi watakaosaidia kufuatilia suala hilo kwa undani ambapo watu kadhaa walichaguliwa, akiwamo Abdallah Kitona, ambaye amekuwa mfuatiliaji wa mara kwa mara wa suala hilo katika idara zinazohusika.
Kitona na wenzake wanasema walifika wizarani na kukutana na William Mshama aliyekuwa amekaimishwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa wizara na kumueleza suala hilo.
“Tukiwa ofisini kwake alimuita Mhandisi Mtemo na kumhoji juu ya suala letu akamjibu kuwa tunastahili kulipwa na kwamba ripoti ipo kwa Katibu Mkuu.
“Mtemo alisema kilichoamuliwa na wizara yeye hakijui lakini wizara inaogopa kuwalipa watu wa Tunduru kwa kuhofia kuamsha mgogoro wa watu waliovunjiwa nyumba Kimara,” anasema Kitona.
Kwa upande mwingine wanapingana na barua ya Novemba 2, 2017, yenye kumb. Na. CDA 87/99/01C/148 iliyoandikwa na wizara kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ikibainisha kuwa anayefaa kulipwa ni mtu mmoja tu.
“Leo tunashangaa tunapoambiwa kwamba tulikuwa ndani ya mita 22.5 hatufai kulipwa wakati kuna waliokuwa ndani ya mita hizo walilipwa fidia.
“Lakini ukiisoma barua hiyo inasema kuna watu wamo ndani ya mita 22.5 mpaka 30 na wamekwisha kufanyiwa tathmini na hesabu zao zimetunzwa hadi hapo serikali itakapohitaji ardhi hiyo ili itumike kwa shughuli za baadaye ndipo watakapolipwa fidia,” anasema Kitona.
Pia, anahoji ikiwa waliolipwa walikutwa ndani ya mita 22.5 walipaji walizingatia vigezo gani kuwapa fidia ilhali sheria ya barabara inasema ukiwa ndani ya mita 22.5 haustahili kulipwa fidia.
Kitona anasema anashangaa ilikuwaje jirani aliyekuwa anapakana naye amelipwa lakini yeye hajalipwa?
“Nyumba yangu mimi sikulipwa lakini nyumba ya jirani yangu amelipwa, nyumba ya tatu kutoka kwangu imelipwa, na nyumba ya tano imelipwa na nyingine zinarukwa.
“Inawezekanaje mimi na wenzangu tuambiwe hatutalipwa, hawa waliolipwa vilitumika vigezo gani?” anahoji Kitona.
Anahoji, ilikuwaje mwaka 2016 TANROADS walirudi katika vijiji vyao na kuwaelekeza kwamba ambao hawajalipwa fidia watulie haki zao zipo?
Pia, anahoji fedha hizo zimepelekwa wapi ikiwa wizara ilihakiki majina na kuahidi kuyafikisha Ofisi ya Rais kwa ajili ya kuidhinisha malipo?
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Razeki Alinanus, ameulizwa na JAMHURI kuhusu madai ya wananchi hao ambapo amejibu kuwa wote waliostahili kulipwa fidia walishalipwa.
“Barabara imekamilika tangu mwaka 2016, hata kama unataka kujua malalamiko ya hao unaowasemea muulize mbunge uliyemtumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu yake, mimi sina zaidi,” anasema Mhandisi Alinanus.
Wananchi wenye madai hayo wanasema alipoletwa Mkuu wa Wilaya mwingine ambaye ni Julius Mtatiro alijiapiza kufukua makaburi ili wananchi hao wapate fidia zao.
Lakini wanashangaa kwa sasa Mtatiro ameweka nondo na zege ngumu juu ya makaburi hayo na kwa sasa hayafukuriki.
JAMHURI limemtafuta Mtatiro, akaahidi kutoa ushirikiano, lakini baadaye akaacha kupokea simu.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amelitahadharisha JAMHURI kuwa kufuatilia suala hilo kunaweza kuwa chanzo cha kuhatarisha amani kwa wananchi.
“Usirahisishe mambo kwa kutafuta taarifa kwenye vyanzo visivyo sahihi, suala hilo ni la muda mrefu. Kuwa makini,” anasema Brigedia Jenerali Ibuge.
JAMHURI linafahamu kuwa Brigedia Jenerali Ibuge amepokea ofisi hiyo hivi karibuni baada ya RC aliyekuwapo, Christina Mndeme, kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara.
Kwa upande mwingine, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Segorena Francis, amelieleza JAMHURI kuwa suala hilo analifahamu, hivyo analifuatilia kujua undani wake.