DAR ES SALAAM
Na Paul Mahundi
Ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Masauni, Makao Makuu ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) wiki iliyopita, imeonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufuatilia hatua zinazochukuliwa na taasisi mbalimbali kuleta mageuzi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Masauni pamoja na kuridhishwa na kazi inayofanywa na TADB, ameitaka benki hiyo iendelee kwa nguvu kuhamasisha jamii kuwekeza katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, na kusema kwa kufanya hivyo benki itakuwa chachu ya kuleta mageuzi katika sekta hizo na ukuzaji wa uchumi wa nchi.
Pia amedokeza kwamba serikali itapitia mapendekezo ya kuiongezea TADB mtaji na kuipa nguvu ya kujishughulisha na mambo kama upatikanaji wa haraka wa pembejeo, utafiti na upatikanaji wa mbegu bora za mimea na mifugo ili kurudufisha tija.
Ameshauri uwepo ushirikiano baina ya TADB na taasisi kama vile Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuibua fursa za uwekezaji na ajira.
“Wananchi wengi wamekuwa wakiwekeza fedha zao kwenye bondi za serikali katika benki mbalimbali ambapo faida yake inachukua muda mrefu, ikilinganishwa na kuwekeza kwenye kilimo,” anasema Mhandisi Masauni, na kuiomba benki ibuni utaratibu wa kuwashawishi watu wenye fedha kuwekeza kwenye kilimo ili wapate faida katika muda mfupi ikilinganishwa muda wa kupevuka wa bondi za serikali.
Anasema sekta ya kilimo ni sekta nyeti ambayo inatoa mchango wa asilimia 26.9 kwenye pato la taifa na ndiyo maana serikali kwenye mpango wa tatu wa maendeleo imeiainisha kuwa moja ya sekta zitakazopewa kipaumbele.
“Serikali inaiangazia sekta hii kama sekta mama yenye mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa letu na hata kwenye kutengeneza fursa za ajira kwa takriban 65% kwa vijana wetu,” anasema.
Waziri anasema kitendo cha benki hiyo kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kutoka Sh bilioni 30 hadi kufikia Sh bilioni 300 ni jambo la kujivunia na lenye kuleta matumaini ya maendeleo mazuri siku zijazo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Anasema kuwa ili kuongeza ufanisi kwenye sekta ya kilimo, TADB inatakiwa iendelee kutoa elimu na mikopo nafuu pamoja na dhamana.
“Mambo haya matatu yakikazaniwa, wananchi wengi watakuwa na hamu ya kuwekeza katika sekta hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa huzalisha malighafi zinazotumika viwandani.
“Mbali ya kuwakopesha pesa wakulima, wavuvi na wafugaji wetu yatupasa kuwapatia elimu ya kutosha ya nidhamu ya fedha na matumizi, jambo ambalo likizingatiwa vema litaleta tija ya kutosha,” anasema Masauni.
Kwa kutambua mchango wa TADB kwenye maendeleo ya sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, serikali imedhamiria na itaendelea kuiwezesha benki hiyo ili kusudi izidi kuwahudumia watu wengi zaidi.
“Mbali ya kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya, ninataka niwahakikishieni kuwa serikali itaendelea kuwawezesheni ili muweze kuwatumikia watu wengi zaidi, jambo ambalo litaleta mapinduzi kwenye sekta hizi,” anasema Masauni.
TADB ikishirikiana vema na taasisi nyingine kama vile Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kuna uwezekano wa kuibua fursa nyingi za kiuwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
“Mkishirikiana vema na taasisi kama TIC mnaweza mkaibua na kubaini fursa nyingi zenye kuleta mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta hizi na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” anasema Masauni.
Anaongeza kuwa, japokuwa mtaji wa benki hiyo umekua kutoka Sh bilioni 50 wakati ikianzishwa mpaka Sh bilioni 80, bado mtaji huo ni mdogo na kuahidi kuwa serikali itapitia mapendekezo ya benki hiyo ili kusudi iwe na mtaji mkubwa zaidi utakaowezesha wakulima kuweza kunufaika zaidi kupitia benki hiyo.
“Ninawapongeza kwa kuweza kuukuza mtaji wenu kutoka Sh bilioni 50 hadi kufikia Sh bilioni 80, ni jambo zuri na linatupa fursa na sisi kama serikali kwenda kuangalia namna ya kuweza kuwaongezea nguvu ili muweze kuharakisha juhudi za kuleta maendeleo katika sekta hizi,” anasema.
Masauni anasema upatikanaji wa mbegu bora pamoja na pembejeo ni jambo la msingi katika kuongeza tija, si tu kwenye kilimo bali hata kwenye mifugo na kuihimiza benki kuendelea kutoa mikopo ya pembejeo kwa wakulima na mbegu bora ya mifugo.
“Ili kuwa na kilimo na ufugaji wa kisasa, unahitaji uwe na pembejeo za kisasa na mbegu bora na hapa benki mko kwenye nafasi nzuri ya kupaangalia kwa umakini ili watu wetu waweze kupata tija maradufu.
“Juhudi kubwa inahitajika kufanywa na TADB katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuchagiza maendeleo ya sekta nyingine kama vile sekta ya viwanda ambayo inapewa kipaumbele na serikali kama moja ya sekta itakayozalisha ajira kwa wingi nchini.
“Kupitia kilimo tumeweza kuajiri takriban 65% ya watu, sasa uzalishaji wenye tija unahitajika ili kusudi mazao hayo yaende kutumiwa na kuleta maendeleo katika sekta zingine kama vile sekta ya viwanda ambayo ni sekta iliyoainishwa na Serikali ya Awamu ya Sita kama moja ya sekta itakayofungua fursa nyingi za ajira kwa vijana wetu nchini,” anaongeza Masauni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TADB, Ishmael Kasekwa, mbali ya kumpongeza Waziri Masauni kwa kuitembelea benki hiyo, amemhakikishia kuwa benki hiyo itaendelea kutimiza lengo lake kwa kufuata taratibu na miongozo ya uanzishwaji wake.
“Pamoja na kumpongeza, ninataka nimhakikishie Waziri Masauni kuwa tutatekeleza vema lengo la serikali la kuanzisha benki, ambalo ni kuona benki inashiriki kikamilifu kwenye kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini, ” anasema Kasekwa.
Anasema benki itaendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wakulima ili waweze kunufaika na mikopo nafuu itakayochagiza ufanisi na kuleta tija katika sekta ya kilimo.
Lengo la benki ni kuona wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi kupitia vikundi vyao wakinufaika na mikopo hii nafuu.
Anasema TADB imepata urahisi zaidi kuwasaidia na kuwawezesha wananchi kupitia Amcos, vikundi mbalimbali, hivyo akatoa rai ya watu wengi kujiunga kwenye vikundi hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, anasema ili kuleta mapinduzi ya sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, benki hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ya kuhakikisha inaendeleza juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya kilimo nchini.
“Kwa niaba ya Benki ya TADB ninapenda niwahakikishie wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kuwa sisi kama benki tuko tayari na tutaendelea kuwa mstari wa mbele kwenye kutekeleza majukumu yetu ili kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi,” anasema Justine.
“Suala la kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao tumeupa kipaumbele kwa sababu kwa kufanya hivyo tunajua tutakuwa tumemgusa mkulima moja kwa moja, jambo ambalo litaongeza kipato kwa wakulima,” anaongeza Justine.
Aidha, Justine anasema TADB itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya upatikanaji wa mikopo nafuu na kuwawezeshe wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
TADB itaendelea kuweka mazingira rafiki ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na fursa ya kukopeshwa na kuwezeshwa ili kusudi maendeleo ya sekta hizi yazidi kukua na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Matarajio ya wengi ni kuona ushirikiano mzuri uliopo baina ya Wizara ya Fedha na Mipango unachagiza jitihada za serikali katika kuleta maendeleo ya ukuaji wa sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili sekta hizo zifungue fursa kwenye soko la ajira kwa vijana.