Kwanza niwatakie habari njema waungwana wa uga huu wa ‘Waraka wa Mzee Zuzu’ mnaonijulia hali kila iitwapo leo, lakini pia wale wote mnaoguswa na kile ninachokiandika.
Si lazima kila mtu anielewe kwa sababu ninaamini msomaji wa waraka huu lazima awe mrika mwenzangu au kijana aliyepishana na matendo ya usasa wa Tanzania.
Leo tena ninaandika jambo dogo ambalo labda linaweza kuwa na hekima kwa wachache ambao wameamua kujitoa katika kundi la wale wanaoitwa wanakwenda na wakati, wakati upi? Mimi na wewe ambaye labda ni zuzu mwenzangu hatuujui, ni wakati wa kuacha maadili yetu na kuuza utu wetu kwa vipande vya fedha.
Leo baadhi yetu tupo hapa kwa sababu ya malezi ambayo tuliyaishi kutoka kwa wazazi wetu, malezi yale ili yanyooke yalinyooshwa kama pasi kwa bakora na adhabu nyingi na maneno ya hekima kila siku jioni kutoka katika vinywa vya babu na bibi zetu waliokuwa wakitupa simulizi za kimafunzo, ilikuwa ni baada ya chakula cha jioni kilicholiwa kwa kuzunguka sinia au ungo huku tukielekezwa namna ya kula na watu wakiwamo watu wazima.
Nakumbuka sana hekima zile, ni kama filamu ambayo inajirudia ikikosa mbadala wa filamu mpya ambazo naziona leo, filamu za familia kuwa na marafiki zaidi nje ya familia kwa kutumia simu zao, filamu za wasichana kuacha kufanya kazi na kuamua kufuga kucha na kuziposti TikTok, haya ndiyo maisha ya sasa.
Sina hakika uzee wa kizazi hiki kutakuja kuwa na akina nani ambao watategemewa kutoa maneno yenye hekima pale ambapo kuna msigano, kizazi ambacho leo kinaoa au kuolewa na kesho kinatoa au kuomba talaka bila hata ya aibu usoni.
Kizazi ambacho kinadhani wakwe zao wanapenda kuona jinsi wanavyojua kukatika kiuno au kukata mauno ukumbini, sijui hawa wazee watakuwa wa namna gani.
Wengi hawajui kwamba wakati ukuta na siku zinatembea kwa kasi sana, ujana wa leo ndio uzee wa kesho. Sisi tuliokula chumvi ya kutosha tunauona utoto wetu jana na si juzi.
Ujana maji ya moto, hupoa yakapooza na maungo nguvuye muda hufika yakakaa na kukakamaa, siku ni chache sana kutoka kwenye uhuni na kuwa mzee.
Nasaba ya uzee na busara ni kitu muhimu sana kwa majaliwa ya maisha ya mtu, tabia ya mtu mwema huishi na tabia ya muovu ni kukosa historia katika jamii.
Leo mambo yamebadilika kwa sababu matendo yetu hatuyafanyi kwa kuzungumza bali kuandika katika mitandao ya kijamii, leo hifadhi zetu za akili tumeziweka katika mambo ambayo jamii ya kale iliyapinga.
Naandika waraka huu nikiwa ninawaona watoto wengi mitaani wakiwa hawana wazazi wakati wazazi wao wapo.
Zamani ilikuwa nadra kuona hilo, lakini leo mtoto aliyezaliwa na watu ambao wangali hai wanamtelekeza, kisa tamaa zao za mwili. Maadili yako wapi? Ndugu wako wapi? Wazee wa busara wako wapi?
Najua inakera sana kwa watu ambao wanaangalia Magharibi, tunawaangalia watoto, wajukuu, vitukuu, vilembwe, vilembwekezi na vining’ina na kuwaona wazee wa wakati huo watakavyokuwa hawana maana katika jamii.
Wazee ambao huenda wakaamua kutovaa kabisa hata nguo, naiogopa hiyo dunia ambayo naamini inakuja kama hatutasali na kuomba msamaha sana kwa Muumba wetu. Si kwamba sijui mabadiliko ya dunia, hapana, nayajua sana lakini tunatakiwa kuyaangalia mabadiliko katika upana mwingine wa utashi na utu wa mtu.
Naliona kundi la watoto na vijana wasioweza kufikiri bali wanaweza kutazama na kuona majibu, kundi la kesho na wazee wa kesho kutwa, hawa ndio wanaoigiza ngono na kujitangaza na taarifa zao kuendelea kuishi katika kanzidata, naliona taifa la watazama ngono lakini si la wasoma vitabu vyenye maarifa na hawa ndio watakuwa wazee wa hekima wakati huo.
Naliona kundi kubwa la vijana linalojua zaidi maisha ya umalaya na habari za umalaya na umaarufu utokanao na upumbavu na ujinga lakini lisilojua maadili mema na kufanya kazi, lisilojua maisha halisi bali ya kuigiza, kundi linalodhani linapaswa kupewa na si kutafuta, kundi la vijana ambao ni wazee wa kesho wahuni.
Najua labda sijui kwamba haya ndiyo maisha ya kisasa, samahani sana kama nimewakwaza mnaojua maisha.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.