Umoja ni tabia ya kuungana ili kutekeleza shughuli fulani katika kundi kwa pamoja. Tabia hii ni ya binadamu, na baadhi ya wanyama na wadudu. Lengo la kuungana au kuwa na umoja ni kujipatia nguvu zaidi na uwezo zaidi katika kutenda jambo linalokusudiwa.

Umoja huu unaweza kuwa wa fikra au wa mwili au wa moyo. Mathalani, umoja wa nyuki wa kutengeneza chakula chake, yaani asali. Nyani hubeba watoto wao ili kuwapa usalama zaidi. Binadamu huishi pamoja ili wawe na nguvu na uwezo zaidi wa kupambana na mazingira.

Tunapoanzisha umoja wa michezo maana yake ni kuendeleza na kudumisha michezo. Tunapoanzisha chama cha siasa maana yake ni kutaka kushika dola (kuongoza na kutawala nchi). Tunapoanzisha chama cha wakulima maana yake ni kulima na kuendeleza mazao ya chakula na biashara.

Wanadamu wanapoanzisha umoja fulani, lazima wawe na msingi wa lugha ili waweze kuhamasishana, kuelimishana na kuelewana katika umoja wao.

Lugha huwa ndio msingi mkuu wa umoja. Rejea Watanganyika, Waunguja na Wapemba walipoanzisha umoja wao katika kupigania haki zao na uhuru wa nchi zao.

Msingi huo wa lugha hadi leo Watanzania tunautumia katika shughuli zetu mbalimbali. Lugha hiyo ni Kiswahili. Kila Umoja duniani una lugha yake yenye utamaduni wake. Narudia kusisitiza kila lugha ina utamaduni wake.

Lugha yetu ya Kiswahili ina utamaduni wake ambao ni ‘umoja na amani.’ Utamaduni huu umetuwezesha kuishi kwa usalama na kupambana na mazingira ya nchi yetu kwa upendo na utulivu. Lugha ya kejeli, vitisho na kuua watu na viongozi si utamaduni wa lugha yetu.

Ni kosa kwa mtu anayekwenda kinyume cha utamaduni wa lugha yetu ya Kiswahili. Kuzungumza lugha kali ya vitisho au kisasi ni kujaribu kuingiza utamaduni mpya katika umoja wa Watanzania. Watanzania tusikubali utamaduni huu kupewa nafasi ya kuranda kama pia mchezoni.

Naamini Watanzania wenzangu tumepata kusikia makundi au umoja fulani katika nchi za Afrika zikiingia katika utamaduni wa lugha isiyo ya kwao na kujikuta katika matatizo ya maisha na usalama wao kuwa shakani.

Lugha yetu ituongoze na tuitumie vema katika mazungumzo, mijadala na katika malumbano ya hoja ili kuendelea kudumisha umoja na utaifa wetu.

Kudumisha utamaduni wa lugha yetu si woga wala ubwege ila ni uelewa na ujasiri wa kulinda utu wetu na uhuru wa nchi yetu.

Ni sahihi haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu na kuwa mikononi mwetu tuitumie vema kwa kuanza na wajibu.

Hoja za msingi zitolewe na malumbano yakidhi hoja zilizopo. Kukosoa na kukosoana ndio utamaduni wetu katika lugha na siasa. Vipi tukubali kuacha utamaduni huu?

Wapo watu hapa nchini wanafikiri na kuwaza kuingiza lugha ya watu wengine katika nchi yetu ndiyo tiba ya matatizo yetu. Hapana. Lugha ya shari na fujo si mwanana kwetu. Tiba ni kutumia utamaduni wa lugha yetu Iliyojaa hekima, amani na utulivu.

Mtu kupenyeza vineno vya pekepeke katika mazungumzo ni kuhatarisha utulivu na amani yetu. Amani haiuzwi, inatengenezwa na watu wenye umoja wao ndani ya lugha yao. Mazingira hubadilishwa na kuneemeshwa kwa wanaumoja kuwa na lugha moja. Na hii ndiyo hoja iliyoko mbele yetu.

Huduma za kiuchumi, kisiasa na kijamii zitatekelezwa pale amani na utulivu upo. Kinyume cha amani na utulivu ni ghasia na vita, ambapo huduma hizo hazitapatikana. Watanzania tuwe macho, tusikubali kuwa watumwa wa bwana!!

Tumedai uhuru kutoka kwa wakoloni kwa madhumuni ya kujikomboa ili tuweze kupambana na mazingira. Kazi hiyo inafanyika kwa uungwana na utulivu. Tafakari.