*Alalamikiwa Tume ya Haki za Binadamu
*Adaiwa kujiundia tume kinyume cha sheria
*Mwenyewe ajitetea kwa kumwaga matusi
DAR ES SALAAM
NA MWANDISHI WETU
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, analalamikiwa na mfanyabiashara, Dk. Hamis Kibola, katika Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Anamlalamikia kwa kumbambikia kesi na kumharibia biashara zake, akihusisha matukio hayo na utawala uliopita.
Matukio yanayofanana na hili yamekuwa yakiibuka baada ya uongozi wa Rais John Magufuli kufikia tamati Machi, mwaka huu.
Miongoni mwa waliokwisha kulalamikiwa na kufunguliwa kesi mahakamani ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya.
Mnyeti ambaye sasa ni Mbunge wa Misungwi mkoani Mwanza, analalamikiwa na Dk. Kibola, anayemiliki kitalu cha uwindaji katika Pori Tengefu la Simanjiro mkoani Manyara kupitia Kampuni ya HSK Safaris.
Anamtuhumu mbunge huyo na mfanyabiashara Saleh Al Amry. “Mnyeti alipanga njama kwa ustadi mkubwa akishirikiana na Al Amry anayefanya biashara ya uwindaji ili kunufaika na kitalu hicho. Al Amry akapeleka tuhuma kuwa HSK Safaris inajihusisha na ujangili.
“Mateso yakaanzia hapo. Taarifa zikapelekwa Polisi. Mnyeti akaingilia kati na kuunda Tume ya Uchunguzi,” analalamika Dk. Kibola.
Dk. Kibola anasema yeye na Al Amry walianza kushirikiana kibiashara kwenye kitalu hicho mwaka 2016. Al Amry alijihusisha na utafutaji wageni pamoja na uendeshaji wa shughuli zote za kitalu, kabla ya kutofautiana Juni 2019.
Dk. Kibola analalamikia hatua ya Mnyeti ya kumuundia tume ya kumchunguza ilhali akijua hana mamlaka hayo kisheria. Tume hiyo iliongozwa na polisi anayeitwa Mchaki. Ilifanya kazi kwa wiki moja tu ya Desemba 2019 na ikawasilisha ripoti kwa Mnyeti.
Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchunguzi (Commissions of Inquiry Act) kifungu cha 3(1) na Sheria ya Tawala za Mikoa (Regional Administration Act) kifungu cha 6(2); ni rais pekee mwenye mamlaka ya kuunda tume ya uchunguzi, na kwa kuwa mamlaka hayo amepewa kwa sheria iliyoandikwa, naye anaweza kuyakasimisha kwa mkuu wa mkoa kwa maandishi.
Mtoa taarifa wetu anasema: “Ilikuwapo kinyume cha sheria. Mnyeti hakupewa mamlaka na rais kuunda tume ya uchunguzi. Hakupewa kibali kwa maandishi. Aliamua kufanya hivyo kutokana na ukaribu aliokuwa nao na Rais Magufuli.”
Chanzo cha ugomvi kinatajwa ni masilahi kati ya washirika wa kibiashara kwenye kitalu hicho, yaani Al Amry na Dk. Kibola. “Mnyeti alitumia mwanya huo kuvuruga uwindaji kwa masilahi yake,” kinasema chanzo chetu.
Dk. Kibola anamtuhumu Al Amry kwa kuzua ugomvi baada ya yeye Dk. Kibola kumpata mwekezaji mwingine, kisha kwenda kulalamika kwa Mkuu wa Mkoa, Mnyeti.
“Mnyeti akamwelekeza Mtendaji wa Kata ya Emboret, Belinda Sumari, kuwazuia maofisa wa HSK Safaris kuingia kambini kuendelea na kazi.
“Maelekezo hayo pamoja na utekelezaji wake vilifanyika bila barua wala maandishi rasmi kama taratibu za serikali zinavyoelekeza, hivyo kutia shaka uhalali wa amri na maelekezo yote,” anasema mtoa habari wetu.
Dk. Kibola analalamika kuwa nyuma ya Mnyeti kulikuwa na mfanyabiashara bilionea kutoka moja ya nchi za Kiarabu aliyekuwa anaandaliwa kukabidhiwa kitalu hicho.
“Ni pesa nyingi sana zinahusika kwa kuwa nyuma yake yupo mfanyabiashara tajiri wa uwindaji anayeishi Uarabuni (jina tunalo) anayetaka kumiliki kitalu hicho kupitia kwa Al Amry,” anasema Dk. Kibola.
Kwenye tume iliyoundwa, miongoni mwa vielelezo vilivyowasilishwa ni picha za ndege wanaodaiwa kuwindwa kiharamu mwaka 2019 ili kuonyesha kuwa Dk. Kibola amepoteza sifa za kumiliki kitalu hicho.
Picha hizo zinamwonyesha mwindaji mwenye asili ya Kiarabu akiwa ameshikilia ndege aina ya ‘kori bustard’ ambao wamo hatarini kutoweka, hivyo hawaruhusiwi kuwindwa.
Hata hivyo, picha halisi zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii ni za Desemba 22, 2018; mwaka mmoja nyuma wakati Al Amry akiwa mbia wa HSK Safaris akisimamia operesheni zote.
Baada ya ripoti ya tume, Mnyeti aliwasiliana na Kikosi Kazi (Task Force) Dhidi ya Ujangili na kukielekeza kufanya uchunguzi wa tuhuma za ujangili dhidi ya HSK Safaris.
Desemba 19, 2019 kikosi kazi hicho kilimkamata Dk. Kibola na watu wengine kadhaa wakiwamo wawindaji mahiri (professional hunters).
Dk. Kibola alitolewa Dar es Salaam hadi Arusha na kuwekwa rumande siku saba katika Kituo cha Polisi cha Utalii bila kupelekwa mahakamani.
Anasema baada ya kuachiwa kwa dhamana yeye na wenzake waliendelea kuripoti polisi tarehe 10 ya kila mwezi, hadi Oktaba mwaka jana walipopelekwa mahakamani.
Tofauti na ilivyotarajiwa, Dk. Kibola anasema alifunguliwa kesi ya ukwepaji kodi akidaiwa kutolipa tozo kadhaa za serikali katika mishahara ya wafanyakazi wake, ikiwamo ‘Skilled Development Levy’. Kesi hiyo inaendelea mahakamani.
Anasema kwenye sakata lote la kuandamwa na Mnyeti, amewekwa rumande kwa nyakati tofauti kwa siku 30.
Ripoti haionekani Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
JAMHURI limewasiliana na kiongozi wa tume iliyoundwa na Mnyeti, Mchaki, na katika maelezo yake amesema: “Siwezi kuzungumzia suala la tume ile kwa sasa. Mtafute RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) wa Manyara atakufafanulia.”
RPC wa Manyara, Merson Mwakyoma, anasema kwa kuwa kazi ilifanywa kwa maelekezo ya mkuu wa mkoa aliyeondoka, ni vema kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa mpya, Makongoro Nyerere.
“RC ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa. Ukimpata atakueleza ni nini kilichomo kwenye ripoti ya tume na umuhimu wake kwa usalama wa mkoa,” amesema Mwakyoma.
Makongoro amezungumza na JAMHURI na kusema suala hilo ni jipya kwake na kutaka lipelekwe kwa msaidizi wake, Musa William, kwa kuwa alikuwapo na amefanya kazi chini ya Mnyeti.
Kwa upande wake, William anasema hana taarifa za kuwapo kwa uchunguzi huo.
“Nadhani wakati huo nilikuwa bado wilayani. Nimehamia hapa Mei, mwaka jana, kwa hiyo sijui chochote, wala wajumbe waliounda tume hiyo siwajui…Sijawahi kuliona faili hilo. Ni ngumu sana kuwa na majibu. Lingekuwapo ningeliona kwenye ‘confidential’ (mafaili ya siri). Kwa kifupi halipo. Hakuna taarifa hizo,” anasema.
Wahusika wakuu wazungumza
Dk. Kibola anakiri kuhojiwa na Tume ya Mchaki, na baadaye kukamatwa na kikosi kazi. “Ni kweli. Lakini kwa sasa nisiseme zaidi kwa kuwa malalamiko yangu nimeyafikisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Ninaamini huko nitatendewa haki,” anasema.
Kuhusu kubambikiwa kesi ya ujangili, Dk. Kibola anasema kesi aliyonayo mahakamani kwa sasa si ya ujangili, bali ni ya ukwepaji kodi, ingawa awali alituhumiwa kufanya ujangili.
Mmoja wa watu waliokamatwa na kikosi kazi pamoja na Dk. Kibola, Gerald Kashiro, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
JAMHURI limezungumza na Mnyeti kwa simu, na alipoulizwa ushiriki wake kwenye yale anayolalamikiwa na Dk. Kibola, amesema: “Huo ni upumbavu na utapeli mtupu, hao HSK Safaris na wakurugenzi wake wote ni matapeli na majangili. Mimi huwa sihangaiki na siasa za kitapeli, JAMHURI hamjui kuwa HSK Safaris ni jangili? Yaani mnashirikiana na matapeli na majangili!”
Baadaye alikata simu, na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi (sms) wenye maswali kuhusu sakata hili, hakujibu.
Kwa upande wake, Al Amry, anakiri kuifahamu HSK Safaris akisema imekuwa ikimchafua bila sababu.
“Huyo mkurugenzi (Dk. Kibola) kwa sasa sekta ya uwindaji haimtaki tena. Madeni yamemzidi. Anadaiwa karibu Sh bilioni 1, ushuru wa TAWA (Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania) hajalipa kwa miaka minne.
“Ni jangili aliyekuwa akikodisha bunduki moja kwa dola za Marekani 500,” anasema.
Dk. Kibola amekanusha vikali tuhuma za yeye kushirikiana na majangili, na hata deni la TAWA. Barua aliyoandikiwa na TAWA ya Aprili 30, mwaka huu inaonyesha kuwa deni la HSK Safaris Limited ni dola za Marekani 63,630. Dola moja ni wastani wa Sh 2,320.
Kuhusu picha za ndege wanaodaiwa kuuawa kijangili, Al Amry anasema anazitambua ni za mwaka 2019 wakati yeye akiwa ameshatengana na HSK Safaris.
Pia anadai kutoifahamu picha aliyopigwa akiwa na Kashiro aliyefungwa miaka 30 jela kwa makosa ya ujangili.