IRINGA 

Na Mwandishi Wetu

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Clinton Development Initiative (CDI) imejipanga kutoa mikopo ya Sh bilioni 1.15 kufungua mnyororo wa thamani wa zao la soya mkoani hapa. 

Kwa mujibu wa randama ya maelewano iliyosainiwa hivi karibuni, ushirikiano huo utaongeza upatikanaji wa mitaji kwa vyama vya msingi (AMCOs) 29 na kuwanufaisha wakulima 2,900 walio katika programu.

“Hii ni mara ya kwanza kwa TADB kujihusisha na mradi katika mnyororo wa thamani wa soya. Kwa sasa duniani na hata nchini kuna ongezeko la mahitaji ya soya kama nyongeza ya virutubisho katika chakula cha binadamu. 

“Kuna wakulima na wajasiriamali wadogo na wa kati, hasa wanawake, ambao wanajishughulisha na biashara hii. Pamoja na hayo, kuna mahitaji makubwa ya soya kama kirutubisho katika chakula cha mifugo pia, hususan kuku,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine.

Anasema ushirikiano huo unawezesha kuwapo kwa mfuko maalumu wa mtaji ili kusaidia viongozi wa wakulima, benki za kijamii vijijini (VICOBA) na wanachama wa AMCOs waweze kupata mbegu kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora zaidi. 

Justine anasema AMCOs hizo zitapata mikopo maalumu kuwawezesha kununua mapema soya na kuwaunganisha katika soko la soya baada ya mavuno.

Mkurugenzi Mkazi wa CDI, Monsiapile Kajimbwa, anasema katika ushirikiano huo, CDI imechangia rasilimali kwa ajili ya mafunzo ya kifedha na maendeleo ya kibiashara ya kilimo.

“Uwekezaji huu utawaongezea kipato wazalishaji wadogo wa soya kwa sababu AMCOs zinazoshirikiana na CDI zina nafasi nzuri zaidi kuwahudumia wanachama wao. 

“Kwa miaka mingi, tumefanikiwa katika maeneo ya kutoa mikopo ya pembejeo za kilimo na mikopo ya shughuli baada ya mavuno kupitia vyama vya msingi tunazoshirikiana nazo. Hivyo, huu ni muda muafaka wa kupanua ukubwa wa mradi huu hapa mkoani Iringa,” anasema Kajimbwa.

Meneja wa Umoja wa Ushirika wa Wakulima Iringa (IFCU), Tumaini Lupola, anasema hatua hiyo ni fursa kwao katika kusaidia vyama vya msingi kurasimisha uuzaji wa mazao, hususan soya kwa manufaa ya wanachama na wakulima. 

Anasema mikopo hiyo itawanufaisha sana AMCOs kwa kununua mapema soya kutoka kwa wakulima, kukusanya na kuwauzia wanunuzi kwa idadi kubwa, viwango bora na namna bora zaidi.

IFCU ni wanufaika wa moja kwa moja wa mkopo huu, lakini pia watakuwa ni wasimamizi wa AMCOs hizo katika mradi huu.

Pamoja na hayo, Justine anasema: “Uzalishaji wa soya nchini Tanzania umeongezeka maradufu ndani ya miaka 10 iliyopita. Kutoka kuzalisha tani 3,100 mwaka 2009 hadi tani 22,953 mwaka 2019. 

“Hata hivyo, uzalishaji huu bado ni kiwango kidogo ukilinganisha na nchi nyingine duniani. Kupitia modeli yetu jumuishi wa kifedha wa mnyonyoro wa thamani, tuna kila sababu ya kutarajia ongezeko la uzalishaji Iringa.”

Akizungumzia ushirikiano huo, kiongozi wa wakulima kutoka Kijiji cha Mgama, Kilolo, Angelique Kitime, anasema umekuja kuokoa wakulima.

“Kuwa na uwezo wa kupata mbegu bora zilizothibitishwa na kwa gharama nafuu, itatuwezesha sisi wakulima kushusha gharama zetu za uzalishaji na kuongeza kipato chetu,” anasema Angelique.

CDI inafanya kazi na wakulima wadogo wapatao 80,000 nchini Tanzania, Malawi na Rwanda. Shughuli za CDI zimeweshwa kwa msaada wa Shirika la Nationale Postcode Loterij.