DAR ES SALAAM 

Na Regina Goyayi

Hatimaye Kampuni ya The Look na Kamati ya Miss Tanzania imeweka hadharani makosa sita yaliyosababisha kuenguliwa kwa Miss Tanzania 2020/2021, Rose Manfere, kuwakilisha nchi katika mashindano ya urembo ya dunia, yaani Miss World.

Akizungumza na JAMHURI jijini Dar es Salaam, Katibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Azama Mashango, amesema sababu ya Rose kuenguliwa ni kukiuka sheria, taratibu na miongozo aliyokuwa akipewa na wasimamizi wake.

The Look ndio wasimamizi wa mashindano ya urembo na warembo nchini.

“Kwa hadhi aliyonayo Miss Tanzania, yapo mambo anayotakiwa kuyafanya na yapo ambayo hatakiwi kuyafanya.

“Lakini Rose akipewa mwongozo sahihi wa kufuata, anabisha! Kwa mfano, amekuwa akishiriki matamasha yanayoandaliwa na watu wengine bila ruhusa ya The Look, na wakati mwingine yeye mwenyewe anaomba mialiko.

“Hili la kuomba mialiko ni jambo linalofedhehesha na kudhalilisha hadhi ya Miss Tanzania. Miss Tanzania si kitu kidogo. Yeye hualikwa badala ya kuomba mwaliko! Ni aibu sana hii,” anasema Mashango.

Kwa taratibu zilizopo, Kampuni ya The Look ndiyo yenye haki ya kusimamia shughuli zote za kisanii za mrembo wa Tanzania.

Pamoja na maelezo hayo, Mashango anasema kisheria Rose sasa hana sifa ya kuliwakilisha taifa kwenye mashindano ya dunia, kwani makosa yake yanamwengua moja kwa moja.

“Miongoni mwa makosa mengine kadhaa aliyofanya ni kuunda menejimenti yake binafsi nje ya mkataba, kutokufuata maelekezo ya Kampuni ya The Look ambao ni wasimamizi wa shindano, na kutokukubaliana na mwongozo anaopewa wa jinsi ya kushirikiana na wadhamini wa mashindano,” anasema.

Anasema kwa kuwa leseni ya kusimamia mashindano ya Miss Tanzania ni mali ya The Look, basi ni kampuni hiyo ndio wanaotoa jina la mshiriki wa urembo wa dunia.

“Ni The Look ndio wanaowasilisha jina la mshiriki huko ‘duniani’ na tayari jina lililopelekwa huko si la Rose, bali la mrembo anayeitwa Juliana Rugumisa. Huyu ndiye mwakilishi wa Tanzania kwa kuwa alishika nafasi ya pili nyuma ya Rose,” anasema.

Hata hivyo, anasema taji la Miss Tanzania 2020/21 litaendelea kushikiliwa na Rose Manfere; kwamba hatavuliwa taji hilo.

“Adhabu kwa makosa yake ni kutoshiriki Miss World, lakini kiti cha Miss Tanzania kitaendelea kukaliwa na Rose,” anamaliza Masango.