Na Joe Beda Rupia

Elimu elimu elimu. Ndiyo. Elimu. Inatajwa kuwa ufunguo wa maisha. Lakini kikubwa zaidi elimu ndiyo silaha dhidi ya ujinga.

Ujinga. Moja miongoni mwa mambo matatu yanayotajwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kama maadui wakuu wa taifa letu.

Maadui wengine ni umaskini na maradhi. Ujinga, umaskini na maradhi. Naam, maadui wakuu wa maendeleo.

Silaha kubwa dhidi ya maadui hao ni elimu. Kwamba elimu, tena elimu bora huwaondoa maadui wengine wawili; umaskini na maradhi, kwa mpigo.

Majuzi kumeibuka hoja, nzito, kiongozi mmoja wa kitaifa akihoji (au kupinga?) ‘maelekezo’ ya kiongozi mwenzake wa kitaifa.

Hoja ni maandalizi ya mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita.

Wakubwa wametofautiana. Waziri wa Elimu, Profesa Ndalichako hataki ‘kambi’. Si kambi za jeshi, hapana! Ni kambi za kusoma kwa pamoja wanafunzi wanaojiandaa kwa mitihani.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, hataki kutekeleza agizo hilo mkoani kwake. Ana hoja. Lakini ninaamini hata Profesa Ndalichako naye ana hoja. Hoja zinagongana.

Profesa anaamini kuwa kambi zinawaongezea gharama zisizo na maana wazazi na walezi; Mtaka anaamini kambi hizi zinaongeza ufaulu kwa watoto, hasa wa ‘shule za kata’, au tuseme shule za kawaida.

Hoja ya profesa ina ukweli ndani yake. Kuna familia zinaumizwa na wingi wa michango shuleni nyakati hizi serikali inaposisitiza kuwa elimu ni bure.

Hawaoni ‘ubure’ uliko. Wanajiuliza, kwa nini watoto wasiandaliwe mapema kwa ajili ya mitihani ya mwisho? Walimu walikuwa wapi? Na sasa wanatoka wapi kwenda makambini?

Je, kufanya hivyo (kuweka kambi za masomo) si sawa na kunenepesha ng’ombe siku ya mnada? Huko makambini watoto wanaelewa au wanakaririshwa kwa ajili ya kujibu mitihani iliyo mbele yao?

Upande mwingine Mtaka anaamini kuwa kambi zina faida kubwa. Anazifahamu. Tena sana tu. Amewahi kuzisimamia akiwa Simiyu na matokeo yake sote tumeyashuhudia. Watoto wamefaulu.

Sasa hilo analihamishia Dodoma. Anaomba kuungwa mkono na wazazi na walezi wote wa Dodoma. Watoto wapige kambi. Kazi kazi! Matokeo watayaona.

Mtaka anadai kuwa kati yake na profesa, yeye ndiye anapaswa kusikilizwa kwa kuwa yuko ‘field’. Kama ni vitani, yupo ‘mstari wa mbele’.

Profesa anakula kiyoyozi tu. Anasoma na kusaini mafaili. Hajui hali halisi mtaani/vijijini. Watoto wake hawapo shule za kata! Hawana habari kuwa, achilia mbali maabara na kemikali zake, kuna shule hazina matundu ya choo!

Hoja zinagongana. Wananchi hawajui wamsikilize nani. Waziri au Mkuu wa Mkoa. Bila shaka Mtaka anafahamu au ana hofu kuwa waziri ana nafasi kubwa ya kusikilizwa kuliko yeye.

Anajijengea ngome kwa kusisitiza yeye yupo ‘field’, bega kwa bega na wananchi wa hali ya chini. Anawajua vizuri zaidi.

Hoja yake ina mashiko. Wakati profesa anasimamia elimu nchi nzima; shule za umma na hata za binafsi, Mtaka anasimamia Mkoa wa Dodoma (awali Simiyu) pekee na amejikita kwenye shule za umma tu. Vitu viwili tofauti.

Kwa hiyo ni kweli kuwa anafahamu vizuri sana hali halisi. Ni kweli kuwa yupo ‘field’. Sasa Mtaka anataka hata kama nchi nzima ikitekeleza agizo la profesa, Dodoma wasifanye hivyo kwa kuwa yeye ndiye ‘Rais’ wa mkoa huo.

Sawasawa. Swali ni je, kambi zina faida au hasara? Wananchi wanazitaka au hapana? Michango yake kila mtu anaimudu? Haibagui wenye nacho na wasio nacho? Ina tofauti yoyote na ‘twisheni’?

Kambi. Si za jeshi. Za kusoma. Kiasili kusoma kwa nguvu au kwa ziada mitihani inapokaribia, ni suala lisiloepukika.

Miaka ya mwanzoni ya 1980 kaka zangu walipokuja likizo nyumbani Mpanda, walikuwa wakihadithia namna walivyokuwa wakikesha; miguu kwenye beseni la maji, kujiandaa na mitihani. Hawakuwa na kambi! Lakini walisoma kwa nguvu sana.

Ooh, samahani. Kambi walikuwa nazo lakini si kama hizi za Mtaka. Walikuwa na vikundi vya ‘discussions’ na kujisomea. Walikesha wakisoma. Tena kwa vibatali.

Mmoja alikuwa Itaga, mwingine Kantalamba na mkubwa alikuwa Minaki. Dada yangu mkubwa alisoma Rugambwa Girls miaka ya mwanzo ya 1970. Mwingine akasoma Loleza. Kote hadithi ile ile!

Ikafika zamu yangu. Kaengesa Seminari. Mitihani ikakaribia. Vikundi vya kujisomea vikajiunda vyenyewe! Tukakesha ingawa hatukuweka miguu kwenye mabeseni ya maji kwa kuwa Kaengesa kuna baridi sana!

Sikumbuki kama mapadri walituruhusu! Lakini tulisoma kweli kweli.

Kwa hiyo kuanzia miaka ya 1970 hadi miaka ya 1990, watu walisoma ama katika vikundi au mmoja mmoja kujiandaa kwa mitihani. Tunarithishana.

Nadhani hata kama kuna walimu wazuri na mazingira bora ya elimu, bado kuna hofu ya mitihani inayosababisha au kushinikiza kusoma hata muda wa ziada. Au labda ni utamaduni wetu.

Profesa amesoma. Watoto wake wamesoma. Naamini naye pia anafahamu ‘presha’ ya mitihani. Si mchezo!  

Zikaja zama za ‘twisheni’. Watoto wakasoma kwelikweli. Lakini ‘twisheni’ zikaleta balaa. Zikaonekana kama ‘maficho’ ya maovu hasa kwa watoto wa kike.

Zikapigwa vita hadi makanisani. Sijui kama zipo kama zilivyokuwa miaka ya nyuma! Wapo walionufaika na ‘twisheni’ na wengine walipata hasara.

Naam. Kila jambo lina faida na hasara zake. Ndiyo maisha.

Profesa hataki kambi. Anataka watoto wasome kwa bidii na wafundishwe na kuandaliwa kwa ajili ya mitihani ndani ya muda wa masomo wa kawaida! Hii ni ngumu kidogo. Mwaka wa mitihani una ‘presha’ jamani!

Mtaka hataki. Anataka muda wa ziada utafutwe. Nguvu ya ziada itumike hata kama ni kuwakaririsha watoto, lakini wafaulu mitihani na kusonga mbele kupambana na adui ujinga.

Akakemea kwa jeuri kauli ya waziri. Nadhani alikosea kwa namna fulani. Ni muungwana huyu bwana. Akaomba radhi haraka sana. Lakini ujumbe wa kijeuri tayari umetawanyika nchi nzima.

Je, iwapo Baraza la Mawaziri ndilo lililoamua kupiga marufuku makambi, kauli yake haipingani na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri? Hatari sana.

Profesa hajajibu. Busara. Utu uzima. Lakini mjadala unafungwaje? Lazima tutafute namna sahihi ya kuwaandaa watoto kwa mitihani yao bila kulumbana.

Bila wakubwa kukosana.