CAIRO, Misri

Jehan, mjane wa Rais wa zamani wa Misri, Anwar Sadat, amefariki dunia nchini Misri akiwa na umri wa miaka 87.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na shirika la habari la taifa, MENA, Jehan Sadat amefariki dunia Ijumaa ya Julai 9, mwaka huu.

Awali, vyombo kadhaa vya habari viliripoti kuwa mama huyo alikuwa amelazwa katika hospitali moja akisumbuliwa na saratani. 

“Mwaka jana, Jehan alipata matibabu kwa muda nchini Marekani, lakini muda mfupi baada ya kurejea nyumbani, afya yake ikadorora,” inasema taarifa iliyotolewa na familia. Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu ugonjwa wake.

Baada ya kifo chake, ofisi ya Rais Abdel Fattah el-Sissi, iliomboleza kifo chake na kumtaja Jehan kama mwanamke wa kupigiwa mfano nchini Misri; ikaahidi kumpa heshima ya kitaifa na moja ya barabara kubwa jijini Cairo kupewa jina lake.

Jehan Sadat alizaliwa mjini Cairo, Agosti 1933, katika familia ya kawaida, baba yake akiwa raia wa Misri na mama Mwingereza. 

Alifunga ndoa na Anwar Sadat mwaka 1949, ofisa wa jeshi ambaye baadaye akaja kuwa Rais wa Misri kuanzia mwaka 1970 hadi alipouawa mwaka 1981. Wawili hao wamejaliwa kupata watoto wanne, Noha, Gihan na Lobna ambao ni wasichana na Gamal, mtoto wa kiume.

Sadat alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kiarabu kutembelea Israel mwaka 1977 na kuhutubia ‘Bunge’ la nchi hiyo linalofahamika kama ‘Knesset’. 

Akaongoza juhudi za kurejesha amani kati ya Misri na Israel, kazi iliyompa umaarufu mkubwa duniani, lakini ikasababisha ukosoaji wa hali juu nyumbani Misri. 

Jehan alikuwa pamoja na mumewe katika ziara hiyo ya Uyahudi, kukutana na viongozi wa Israeli.

Akizungumzia ziara hiyo katika salamu zake za rambirambi, Rais wa Israel, Isaac Herzog, anasema: “Aliungana na mumewe Jerusalem wakati wa ziara ile ya kihistoria na kwa ujasiri mkubwa alisimama bega kwa bega upande wa Rais Sadat katika mapambano magumu kusaka amani na Israel.

“Kwa miaka mingine mingi, Jehan aliendelea kutangaza amani. Kwa niaba ya Taifa la Israel, ninatuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Misri na watu wote wa Misri,” anasema.

Isaac, mtoto wa Rais zamani wa Israel, Chaim Herzog, ameshika wadhifa huo kuanzia Julai 7, mwaka huu. 

Pia alituma rambirambi zake kwa Balozi wa Misri nchini Israel, Khaled Azmi.

Salamu nyingine za rambirambi zimetolewa na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Benny Gantz.

“Ningependa kutuma salamu za pole kwa watu wa Misri kutokana na kifo cha Jehan Sadat, mke wa mwamba wa amani, Rais Anwar Sadat.

“Alikuwa ni Sadat aliyetengeneza njia katika kuleta amani kati ya Israel na Misri na tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu,” anasema Gantz.

Jehan hakusita hata mara moja kumtetea mumewe kwa kitendo chake cha kusaini mkataba wa amani na Israel mwaka 1979 baada ya miongo mitatu ya vita, kitendo kilichozua mtafaruku ndani na nje ya Misri.

Baada ya kuuawa kwa Sadat, Jehan hakuonekana hadharani kwa muda mrefu kabla ya kuibuka hivi karibuni akiwa mmoja wa wanaomuunga mkono jenerali wa zamani, El-Sissi na serikali yake, baada ya taifa hilo kukumbwa na machafuko yaliyomwondoa madarakani mrithi wa mumewe, Hosni Mubarak, mwaka 2011.

“Nina matumaini makubwa kwamba alichokifanya mume wangu, kile alichojitoa hadi kupoteza maisha, kamwe hakitaishia hewani. 

“Ninaamini, ingawa mimi si kijana, kwamba nitaishi na kushuhudia amani ikitamalaki Mashariki ya Kati kati ya Waarabu na Waisraeli, na mimi ni mwanamke mwenye uhakika,” amewahi kusema Jehan alipozungumza na CNN mwaka 2009, katika maadhimisho ya miaka 30 ya mkataba wa amani kati ya Israel na Misri.

Kuhusu makubaliano hayo yaliyosainiwa Camp David, Marekani, Jehan anasema: “Ni kitu kisichosahaulika kuona ujumbe wa Israeli, wa Misri na ule wa Marekani ukikaa pamoja kama marafiki badala ya uadui, wakizungumza na kutaniana. 

“Ni kitu ambacho siwezi kukisahau hata siku moja. Machozi yalinitiririka, sikuweza kuyazuia kwa kuwa nilikuwa na furaha isiyo kifani kuona kuwa sisi sote sasa ni kama familia moja.”

Tangu makubaliano hayo ya amani na Misri, Israel imeshafanya mkataba mwingine na majirani zake Jordan mwaka 1994. Mwaka jana, Serikali ya Jerusalem imefanya majadiliano ya amani na Uarabuni, Bahrain, Morocco na Sudan.

Wakati wa utawala wa mumewe, Jehan alijijenga kama mwanaharakati wa haki za wanawake akisukuma kuanzishwa kwa sheria ya mwanamume aliyemtelekezea watoto mwanamke (hata kwa talaka) kumpa msaada wa kifedha huku watoto wakiwa chini ya uangalizi wa mama. 

Pia alivuma kwa shughuli za kujitolea na za hisani. 

Katika miaka ya 1970 wakati mama huyu alipokuwa akionekana hadharani mara kwa mara, wakosoaji walimlaumu kwa kutumia nafasi ya mumewe kujipatia umaarufu kisiasa.

Ni wakati huo ndipo pia alipoongoza taasisi kadhaa kadhaa muhimu kama Chama cha Mwezi Mwekundu cha Misri, benki ya damu ya taifa na Chama cha Wagonjwa wa Saratani. 

Wakati wa vita ya mwaka 1973 dhidi ya Israel, picha zake akiwatembelea majeruhi zilitokea kurasa za kwanza za magazeti karibu yote ya Misri.

Mwaka 1972, Jehan alianzisha Chama cha Imani na Matumaini, kwa Kiarabu ‘Wafa’ Wal Amal’, ambacho kwa sasa kinaendesha kijiji (eneo) cha maveterani wa vita ambao hawajiwezi na raia wa kawaida. 

Mwaka 1997 alitoa mchango wa kuanzishwa ‘Kigoda’ cha Amani na Maendeleo cha Anwar Sadat katika Chuo Kikuu cha Maryland kama kumbukumbu ya mumewe.

Tovuti ya kigoda hicho inamnukuu akisema: “Sitaki kuona tena sura za watoto wenye njaa au kusikia kilio cha mama aliyepoteza mwanaye vitani. 

“Amani, hiki ndicho kitu ambacho mume wangu alijitolea maishani mwake, na ninataka dunia ifahamu kwamba hakufa kwa uchungu. Amani. Hii ndiyo itanifanya kuwa mwenye furaha.”

Anwar Sadat aliuawa kwa risasi Oktoba 6, 1981 kwenye gwaride la kijeshi jijini Cairo. 

Mubarak, aliyekuwa karibu yake, alinusurika akiwa na majeraha madogo mkononi baada ya askari kuvurumisha risasi jukwaani. Siku chache baadaye, Mubarak akaapishwa kuwa Rais wa Misri.

Wakati Sadat akiwa madarakani, serikali yake ilitafuta uungwaji mkono kutoka vikundi vya Kiislamu kupambana na ushawishi wa watu wenye mrengo wa kushoto. 

Mamia ya wanachama wa Muslim Brotherhood waliachiwa kutoka jela na kukiunga mkono kikundi cha Kiislamu, Al Gamaa al-Islamiyya. 

Lakini mwishowe ni hao hao Muslim Brotherhood waliomgeuka na kushirikiana na Al-Gamaa kumuua.

Jehan alihitimu Shahada ya Fasihi ya Kiarabu mwaka 1977 katika Chuo Kikuu cha Cairo. Mwaka 1986, katika chuo hicho hicho, akapata shahada ya uzamivu ya fasihi

Ameandika vitabu viwili; ‘A Woman OF Egypt’ ambayo ni taasisi yake na ‘My Hope for Peace’, kinachohusu mgogoro kati ya Waarabu na Israel na kuibuka kwa uhafidhina wa Kiislamu.