LINDI

Na Christopher Lilai

Moja ya mambo yaliyosababisha kuwapo kwa vurugu za kuzuia mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam miaka kadhaa iliyopita ni kukosekana kwa uwazi.

Mwanzoni, wananchi wengi hawakuielewa kiundani dhima ya mradi huo, hivyo wakapinga ujenzi wa bomba hilo. Lakini baada ya kueleweshwa, wakibainishiwa faida ambazo watazipata wao binafsi na nchi pia, ubishi wao ukaisha na mradi ukaendelea kwa mafanikio.

Hii inadhihirisha kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya madini nchini ni kukosekana kwa uwazi, uwajibikaji na usimamizi kati ya wananchi wa kawaida, wamiliki wa migodi na watendaji wa serikali. Tatizo hili ni kubwa sana katika ngazi za chini.

Sehemu nyingi wananchi wanaamini kuwa kugundulika kwa  madini kutawaletea ukombozi kiuchumi bila kujua uhusika wao katika mradi husika.

Wananchi wengine wanakuwa na mawazo potofu kuhusu ulipaji wa fidia kwa wenye maeneo yaliyogundulika uwepo wa madini. Hata ulipaji wa tozo, mirabaha na kodi mbalimbali bado ni suala ambaalo linawapiga chenga watu wengi kiasi cha kuwa na dhana potofu.

Kwa maana hiyo, elimu zaidi inahitajika kwa wananchi na viongozi hao juu ya sheria ya madini na kanuni zake ili waweze kujua nafasi zao na haki zao katika utekelezaji wa miradi ya uchumbaji madini. Hali inakuwa mbaya zaidi pale baadhi ya viongozi wa vijiji na kata wanapotoa uamuzi bila kuzingatia matakwa ya sheria.

Aidha, mwingiliano wa majukumu kati ya wachimbaji vibarua na wachimbaji wadogo ni ishara tosha kuwa hakuna uwazi na uwajibikaji katika sekta hii.

Akizungumzia suala hilo, Meneja wa mgodi wa dhahabu wa Mpiruka wilayani Nachingwea, Selemani Ngoso, anasema elimu ya kutosha inahitajika kwa wachimbaji  na viongozi ili kuepusha migogoro mingi ambayo kimsingi haikupaswa kuwapo.

Anasema maeneo mengine kunakuwa na utoroshaji wa madini kwa sababu tu ya kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji kuhusu nini kinapaswa kufanywa na mchimbaji pale anapopata madini.

“Sijawahi kuona wataalamu wa madini wakija kutoa elimu hapa. Elimu ni muhimu sana huku migodini, kwani baadhi ya migodi kwenye mikoa mingine imeanza kutoa kozi kabla ya kuanza uchimbaji,” anasema Ngoso.

Anasema kukosekana kwa elimu hiyo kumesababisha migogoro isiyokwisha kwenye machimbo ya madini.

Ngoso anasema kutokana na kukosa elimu na uwazi juu ya masuala ya madini kumesababisha hata waliolipwa fidia ya  maeneo yao kupisha uchimbaji  wanarudi kwenye maeneo yao na kusababisha migogoro baina ya wachimbaji na wakulima.

Mmiliki wa machimbo ya Mibure wilayani Ruangwa, Maiko Malibiche, amekiri wazi kuwa licha ya kufanikiwa kupata leseni ya uchimbaji kwenye eneo lake, bado hana elimu wala uelewa wa masuala ya madini, hivyo kuomba  mamlaka zinazohusika kutoa elimu hasa sheria, kanuni na sera ya madini ili imsaidie kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria.

“Kwangu suala la ufahamu juu ya sheria ya madini na kanuni zake ni changamoto, hata hapa nilipo sijui kama ninafanya kilicho kwenye sheria au ninavuruga,” anasema.

Anabainisha kuwa uelewa wa sheria na kanuni utasaidia sana hata katika ulipaji wa maduhuli ya serikali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hashimu Komba, anasema kuwa kuna changamoto  kwa viongozi na wawekezaji kuingia mikataba bila kujua taarifa muhimu zinazohusu uwekezaji na kuwa kutojua taarifa na sheria zinasemaje kunachangia migogoro baina ya viongozi wa vijiji na wananchi na viongozi na wawekezaji.

Komba anasema kuwa viongozi wa serikali za vijiji wanatakiwa kuwashirikisha wananchi katika hatua zote kabla ya kuingia mikataba, kwani uzoefu unaonyesha ni viongozi peke yao wanafanya uamuzi unahusu masilahi ya wananchi.

“Wananchi wasifanywe kama mihuri ya kupitisha uamuzi uliofanywa na viongozi. Kutowashirikisha wananchi kunasababisha wawekezaji kwenye sekta ya madini kukiuka makubaliano, kwani huenda walipatikana kwa njia zisizo halali,” anasema Komba.  

Akizunguzia juu ya changamoto hizo hasa za uwajibikaji, Kaimu Meneja wa Madini Mkoa wa Lindi, Mhandisi Jeremiah Hango, amesema ofisi yake imekuwa ikijitaidi kutembelea  maeneo ya machimbo lakini changamaoto kubwa ni pamoja na ubovu wa miundombinu, kwani barabara nyingi kwenye maeneo ya machimbo hazipitiki kiurahisi hasa wakati wa masika.

Aidha, Kaimu meneja huyo anasema kutokana na Ofisi ya Madini Mkoa wa Lindi kuwa pembezoni kumesababisha  baadhi ya wateja kutofika ofisini kufanyiwa mahesabu kwa ajili ya malipo, hasa kwa wale wanaotoka Wilaya ya Kilwa, ambao kwa wale wanaofika ofisini hapo wamekuwa wanalalamika kuwa wanatumia muda mwingi kusafari.

Pia idadi ya safari za maofisa wa madini kwenda machimboni kwa kazi za ukaguzi na ufuatiliaji maduhuli inakuwa ngumu kutokana na ofisi hizo zilipo.

Kuhusu soko la madini lililopo wilayani Ruangwa, Mhandisi Hango anaeleza kuwa lipo kwa kila mchimbaji kuuzia madini yake bila ubaguzi wa aina yoyote.

“Zipo changamoto chache kwenye soko letu la Rungwa ambalo ndilo linalotegemewa na wachimbaji, hata hivyo hazifanyi wachimbaji kushindwa kuuza madini,” anafafanua.

Anazitaja changamoto hizo ndogo ndogo kuwa ni pamoja na uchache wa vifaa vya kupimia madini (XRF mashine). 

Anasema taarifa ya kukosekana kwa mashine hiyo tayari imefikishwa kwa uongozi wa Tume ya Madini na kuwa fedha zilikwisha kupatikana na taratibu za manunuzi zinaendelea.

Changamoto nyingine ni uchache wa wanunuzi kwenye soko hilo, jambo ambalo linafanya wakati mwingine wachimbaji kukosa mnunuzi wa madini yao, hali ambayo husababisha madini yamayouzwa kwenye soko hilo kukosa bei nzuri.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, kaimu meneja huyo amesema juhudi zimeanza kuwashawishi wanunuzi zaidi waweze kuja katika soko  hilo.

Hata hivyo kaimu meneja huyo amebainisha kuwa licha ya changamoto hizo bado mkoa umeweza kuvuka lengo la kukusanya maduhuli ya serikali, ambapo hadi mwezi Aprili mwaka huu walikuwa wamekusanya Sh bilioni 2.4, ambazo ni zaidi ya lengo walilojiwekea la kukusanya Sh bilioni 2 hadi mwisho wa mwaka wa fedha. 

“Kweli, licha ya changamoto hizo bado tumeweza kuvuka lengo la kukusanya maduhuli ya serikali ambapo kupitia soko letu la Ruangwa tumekusanya Sh bilioni 2.4 na hii ni kabla ya mwisho wa mwaka, ambapo lengo ni kukusanya Sh bilioni 2 hadi mwisho wa mwaka wa fedha,” anafafanua.


p.p1 {margin: 0.0px 0.0px 10.0px 0.0px; font: 26.0px Garamond}
Wachimbaji wadogo wa madini wilayani Ruangwa mkoani Lindi wakiwa kazini.