DAR ES SALAAM

Na Alex Kazenga

Pamoja na serikali kutilia mkazo ujenzi wa sekondari na vituo vya afya kila kata, Kata ya Minazi Mirefu iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam hali ni tofauti.

Kata hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015 yenye wakazi zaidi ya 44,000, haina shule yoyote wala kituo cha afya, huku huduma hizo zikifuatwa katika kata jirani za Kiwalani (Ilala) na Sandali (Temeke) na kusababisha huduma kuzidiwa.

“Tumeandika barua Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji asaidie kuyaomba majengo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na maghala ya Mamlaka ya Sukari (Sudeco) yaliyopo Mtaa wa Migombani, tuyabadili kuwa shule na kituo cha afya,” anasema Godlisten Malisa, Diwani wa Minazi Mirefu.

JAMHURI limeyashuhudia majengo hayo ambayo hayatumiki kwa karibu miaka 40 sasa na Malisa anasema: “Tukipewa majengo haya tatizo la kata kutokuwa na shule ya msingi na kituo cha afya litakwisha.”

Eneo yalipo magofu ya TMA linatumika kuchungia mifugo, michezo na nyakati za uchaguzi hutumika kwa kuandikisha wapiga kura na upigaji kura; wakati eneo la Sudeco linatumika kwa kilimo cha bustani za mboga na maficho ya vibaka.

Malisa anasema serikali ikiridhia ombi na kubadili matumizi ya majengo hayo, watoto na wakazi wa kata hiyo wataondokana na adha wanayoipata kwa sasa.

“Kiwalani kuna vituo vitatu vya afya; Kituo cha Afya Kiwalani, cha walemavu Yombo na kingine cha Kanisa Katoliki. Wakazi wa kata hii kuna wakati hulazimika kufuata huduma hadi Temeke! Kuna wengine wamepoteza maisha kwa sababu ya umbali wa huduma za afya,” anasema.

Mkazi wa BomBom, Mwanaidi Suleiman, anathibitisha kauli ya Diwani Malisa, akisema mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba aliwahi kushikwa na kichomi saa saba usiku akashindwa kumpeleka Kiwalani kupata huduma.

“Nilitafuta Bajaj au pikipiki usiku ule, sikupata. Kwa kweli siwezi kuusahau usiku ule. Sikutarajia kama asubuhi ingefika salama. Mungu alisimama na mimi, asubuhi ikafika, nikampeleka Hospitali ya Amana,” anasema Mwanaidi.

Anasema wananchi wanaungana na diwani kuiomba serikali iwafikirie na wapo tayari kuchangia ujenzi wa shule na kituo cha afya.

Helman Nyange, mkazi wa Mtaa wa Migombani, anaamini serikali itakubali kubadili matumizi ya majengo hayo ingawa, anasema:

“Juhudi zimeshafanyika sana. Watangulizi wa Malisa walijaribu kuomba, hawakufanikiwa. Naamini sote tukishirikiana, Serikali ya Awamu ya Sita itatusikiliza.”

Anasema ni ufujaji wa fedha za umma kuweka walinzi katika majengo hayo kwa miaka yote hii.

“Kata ya Kiwalani ina shule za msingi saba, zote zimezidiwa na wanafunzi. Watoto wakipelekwa huko wanakataliwa. Itakuwa furaha kubwa Minazi Mirefu tukipata shule yetu,” anasema Nyange.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Migombani, Issa Jeshi, anasema shule ikipatikana wazazi wataokoa fedha wanazowapa watoto kwa ajili ya nauli kwenda na kurudi kata jirani.

Pia itakuwa ahueni kubwa kwa watoto wa kike wanaolazimika kwenda shule zilizoko Temeke.

“Wanaosoma Sandali, Temeke, lazima wavuke ng’ambo ya pili, vilipo viwanja vya ABC, na wanapolima mchicha pale kuna matukio ya ajabu. Kila siku mtoto wa kike apite hapo hadi amalize shule, ataona mangapi?” anahoji Jeshi.

Mbali na hayo, Jeshi anaongeza kuwa kata hiyo haina kituo cha Polisi hali inayosababisha kushindwa kudhibitiwa vitendo vya uhalifu.

Kata ya Minazi Mirefu inaundwa na mitaa ya Minazi Mirefu, Muwale na Migombani.

Wadau wa maendeleo katika kata hiyo akiwamo, Hadija Magube wanasema kipindi cha mvua kuna maeneo ya kata hiyo huwa hayapitiki, hivyo kuzuia watoto kwenda shule.

“Kuna baadhi ya madaraja hujaa maji, ili kwenda shule watoto hulazimika kuzunguka kufuata barabara ya lami. Vivyo hivyo kwa wajawazito,” anasema Hadija.