KIGOMA
Na Mwandishi Wetu
Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Mwandiga – Chankere – Mwamgongo yenye urefu wa kilomita 65 kwa kiwango cha changarawe ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na mikoa jirani.
Akizungumza katika ziara yake mkoani hapa, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema katika lengo la kuifungua barabara hiyo, serikali imekuwa ikiitengea fedha.
“Sasa ni utekelezaji tu. Niwahakikishie wananchi kuwa serikali ipo kazini na barabara hii itaendelea kutengewa fedha kila mwaka kuhakikisha inakamilika,” anasema Kasekenya.
Amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, kuhakikisha ujenzi unafika hadi Kagunga na kwamba barabara ipitike mwaka mzima kwa kuweka zege maeneo yenye miinuko mikali, huku makalvati yakiwekwa maeneo yenye maporomoko ya maji.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Asa Makanika, amesema barabara hiyo ni muhimu na mkombozi kwa watu wa eneo hilo, hasa kata za Ziwani, Mugongo na Kagunga.
“Itarahisisha usafiri kwani kwa sasa wananchi wengi hutumia usafiri wa majini kufuata huduma muhimu za afya na elimu. Kutoka hapa hadi mjini, watu hutumia hadi saa saba! Sasa kujengwa kwa barabara hii kutaleta kicheko kwa wananchi,” anasema Makanika.
Meneja TANROADS Mkoa, Mhandisi Choma, ameahidi kuweka uzio pembeni mwa barabara kuzuia magari kuanguka, hasa kwenye miinuko mikali.
Amesema tangu mwaka wa fedha 2018 /2019, serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo na mpaka sasa eneo la kilometa nane la mlima limekwisha kukatwa na linapitika.