TABORA
Na Benny Kingson
Ujumbe wa kupinga vitendo vya kubakwa na kutumikishwa katika kilimo cha tumbaku na kazi nyingine ngumu uliotolewa na watoto wa shule za msingi Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, umewasisimua viongozi, wazazi na walezi na kusababisha watokwe machozi.
Ujumbe huo wa kusikitisha uliwasilishwa kwa njia ya ngonjera wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika katika Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Igagala.
Mtoto wa darasa la tatu Shule ya Msingi Igagala Namba 5, Sandra Yusuph (10), amesema dunia imejaa magonjwa mengi, watoto wanatumikishwa na wengine kubakwa bila hata aibu, na kuhoji maadili ya jamii kwa watoto yako wapi?
Amebainisha kuwa mtoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, mtu anayemtesa huharibu zawadi yake mwenyewe akitaka mtoto kupewa malezi bora ili amfae mzazi wake siku zijazo, hasa uzeeni.
Matilda Gaspar (11), mwanafunzi wa darasa la nne shuleni hapo, anasema wanaowafanyia vitendo viovu watoto Mungu anawaona na watapata hukumu kali.
“Mlezi wa watoto ni Maulana, hivyo ukimtesa mtoto hautabaki salama,” anasema.
Ujumbe mwingine wenye mguso umetolewa na Shakira Salimu (11) wa darasa la nne Shule ya Msingi Igagala No. 6, amesema utumikishwaji wa mtoto ni dhambi isiyo kifani, iwe kwa mzazi au mlezi.
“Mtoto ndiye taifa la kesho na mlezi wa wazazi wake, kama ataendelea kudhalilishwa, kutumikishwa au kubakwa, ni nani atakayekulea wewe mzazi na taifa litaongozwa na nani?” anahoji kwenye ubeti wa ngonjera.
Akizungumzia ujumbe huo, Helena Andrea, mkulima na mkazi wa Igagala No. 5, anatoa wito kwa wazazi kubadilika na kuacha kuwatumikisha watoto, bali wawapeleke shuleni kusoma.
Mwalimu wa shule hiyo, Yusuph Ramadhani, anakiri kuwa watoto wanapata taabu sana wakati wa kilimo, kwani hulazimika kupalia mashamba ya tumbaku badala ya kusoma.
Kutokana na kuguswa na ujumbe huo, wageni waalikwa wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Abel Busalama, wamewazawadia watoto hao zaidi ya Sh 50,000 na kuwapongeza kwa ujumbe mzuri.
Busalama amewahakikishia watoto kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mzazi, mlezi na yeyote atakayebainika kumzuia mtoto kwenda shule.