TEL AVIV, ISRAEL

Mwamba wa kisiasa wa Israel umeanguka. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Benjamin Netanyahu kushindwa kutetea nafasi yake ya uwaziri mkuu nchini humo.

Netanyahu amedumu katika nafasi hiyo kwa kipindi kirefu kiasi cha kuonekana kuwa kioo cha Serikali ya Israel.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona hatua hiyo ya Netanyahu kuondoka madarakani ni muhimu sana kwani inaweza kuupatia ufumbuzi mgogoro uliodumu kwa miaka mingi baina ya Israel na Palestina.

Wachambuzi hao wanauona msimamo mkali wa Netanyahu wakati akiwa waziri mkuu kuwa kama kikwazo kikubwa cha kumaliza mgogoro huo.

Hata hivyo, viongozi wa Palestina wamesema hawaoni tofauti yoyote ya mabadiliko hayo kiuongozi, kwani uongozi unaoingia wa Waziri Mkuu Naftali Bennett ni mbaya kama unaoondoka.

“Hatuoni uzuri wowote wa uongozi mpya na tunalaani tangazo la Waziri Mkuu mpya Naftali Bennett la kuunga mkono makazi ya walowezi wa Kiyahudi,” anasema mmoja wa viongozi wa Palestina, Mohammad Shtayyeh na kuongeza:

“Uongozi mpya hautakuwa na mustakabali mzuri iwapo hautatilia maanani hatima ya Wapalestina na haki zao za msingi.”

Akihutubia baraza lake la mawaziri kwa mara ya kwanza, Bennett, mwanasiasa wa mrengo wa kulia ambaye aliwahi kuongoza jumuiya ya walowezi, amesema nchi hiyo inafungua ukurasa mpya.

Hata hivyo, amebainisha wazi kuwa serikali yake haina mpango wa kuunga mkono hatua ya kuunda taifa la Palestina na amesema Israel itaendelea kudhibiti ardhi yote iliyo chini ya mamlaka yake.

Kabla hajashika wadhifa huo aliwahi kunukuliwa akiitaka Serikali ya Israel kutumia nguvu zaidi inapokabiliana na wavamizi katika Ukanda wa Gaza.

Bennett aliwahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi katika serikali ya Netanyahu na mwanachama wa Chama cha Likud cha Netanyahu. Hata hivyo, hivi sasa wamekuwa mahasimu wakubwa kisiasa.

Walipofanya kikao cha kwanza cha kukabidhiana madaraka, viongozi hao walikataa kupiga picha ya pamoja.


Rais wa Israel, Reuven Rivlin (katikati mbele), akiwa amekaa karibu na Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo, Naftali Bennett (kushoto mbele) na Waziri wa Mambo ya Nje, Yair Lapid (kulia mbele), katika picha ya pamoja na baraza jipya la mawaziri la nchi hiyo.