BRUSSELS, UBELGIJI
Jumuiya ya NATO imetoa onyo kali kwa China dhidi ya harakati zake za kujiimarisha kijeshi lakini ikasema kauli yake hiyo haimaanishi kuwa ipo tayari kuingia kwenye vita baridi na nchi hiyo ya Mashariki ya Mbali.
Wakizungumza katika kikao chao jijini Brussels, viongozi wa NATO wametoa onyo hilo wakisema kuwa tabia za China kijeshi zinaleta changamoto za kimfumo.
Wamesema kuwa China imekuwa ikiongeza kwa kasi shehena yake ya silaha za nyuklia, pia haina uwazi kuhusiana na upanuzi wa programu za teknolojia za kijeshi.
Aidha, wamedai kuwa wana wasiwasi na ushirikiano unaoimarika baina ya China na Urusi.
Kiongozi Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, ameionya China na kueleza kuwa nchi hiyo imekaribia kukiuka vigezo vya kijeshi vilivyowekwa na jumuiya hiyo.
NATO ni muunganiko wa kisiasa na kijeshi unaohusisha nchi 30 za Ulaya na Marekani Kaskazini. Ilianzishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kama njia ya kukabiliana na kuimarika kwa nchi za kikomunisti.
Hata hivyo, ikijibu mapigo katika taarifa iliyotolewa na Balozi wake wa Jumuiya ya Ulaya (EU), China iliishutumu NATO kwa kukashifu jitihada za maendeleo za China na kusisitiza kuwa nchi hiyo bado ina malengo ya kuheshimu kanuni na mikataba ya ulinzi ambayo inairuhusu kujilinda.
“China haitaweka changamoto za kimfumo kwa yeyote. Lakini hatutakaa kimya na kutofanya lolote iwapo changamoto za kimfumo zitatukabili,” imesema taarifa hiyo.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mgogoro wa chini kwa chini ndani ya NATO baada ya baadhi ya viongozi kuhoji namna nchi wanachama zinavyochangia uendeshaji wa Jumuiya hiyo.
Mgogoro huo ulikua zaidi katika kipindi cha Rais Donald Trump, ambaye alilalamika hadharani kuwa nchi yake inachangia fedha nyingi sana katika NATO ukilinganisha na wanachama wengine na kuhoji nafasi ya Marekani katika ulinzi wa Bara la Ulaya.
Rais aliyemfuatia, Joe Biden, amefanya ziara ya kwanza barani Ulaya na kushiriki katika kikao cha NATO na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na wanachama wengine kuiimarisha Jumuiya hiyo yenye umri wa miaka 72 sasa.
Biden amesema Nato ni muhimu kwa masilahi ya Marekani na kuwa Jumuiya hiyo ina jukumu kubwa la kuhakikisha Kifungu cha tano cha mkataba wake kinachoitaka kila nchi mwanachama kumlinda mwenzake kinatekelezwa kikamilifu.