DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Michezo ya mzunguko wa pili michuano ya mataifa Ulaya maarufu kama EURO 2020, imeanza wiki iliyopita. Kila taifa limeshacheza mchezo mmoja, huku baadhi ya mataifa yakicheza michezo miwili.

Michuano hiyo ya mwezi mmoja iliyopaswa kuchezwa Juni na Julai mwaka jana, nachezwa mwaka huu baada ya kuahirishwa kutokana na dunia kukumbwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona, COVID-19.  

Katika michezo hiyo; miwili kwa mataifa kadhaa na mataifa mengine yakiwa na mchezo mmoja, tumeshapata kitu cha kukijadili vijiweni kwetu.

Ni mapema kuanza masuala ya utabiri, lakini tutazame hatua hii ya michezo miwili na mmoja tumepata kitu gani cha kukijadili. Na vipo vitu hivyo.

Roberto Baggio alistaafia soka lake Brescia, Paolo Maldini alipigwa muhuri wa moto na AC Milan, Fransesco Totti ‘alifia’ zake As Roma, Andrea Pirlo alicheza Seria A misimu 21 huku Alessandro del Piero akicheza kwa misimu 23.

Hao ndiyo Waitaliano na hizo ndiyo mila na desturi zao. Mwaka 2016 wakati kocha Antonio Conte anajiunga Chelsea, alimuhitaji Leonard Bonucci wa Juventus. Man city pia walimuwania Bonucci aliyekuwa katika kiwango bora sana.

Hata hivyo, Bonucci akaishangaza dunia kwa kukataa ofa nono ya Chelsea na Man City na kujiunga na AC Milan kwa Euro milioni 42 tu. Kwake kucheza Serie A ilikuwa ufahari zaidi kuliko Premier League ya England na mabilioni yake ya fedha.

Asilimia 96 ya kikosi cha Italia kwenye michuano ya Euro 2020 inayochezwa mwaka huu, wanacheza ligi ya nyumbani kwao, Serie A. Ni wachezaji wanne tu kati ya 26 wanaounda kikosi hicho wanaocheza nje ya Italia.

Marco Verrati na Allesandro Florenzi wako Ufaransa na PSG, Jorginho Ferro na Emerson Parmieri wanachezea Chelsea ya England.

Asilimia 85 ya kikosi chao kinachoanza ni wale wanaocheza soka Italia. Ni Jorginho na Florenzi pekee wanaopata nafasi ya kuanza. Kama Marco Verrati angekuwa ‘fit’ angecheza, hivyo takwimu ingekuwa ni wachezaji watatu tu nje na Serie A, wanaoanza kwenye kikosi cha Italia.

Waitaliano wanaamini Serie A ndio ligi bora zaidi. Kwao ni bora timu ya taifa wamjumuishe mshambuliaji Andrea Belotti wa Torino iliyonusurika kushuka daraja na kumuacha bwana mdogo Moise Kean wa PSG.

Kwa Waitaliano beki Francesco Acerbi wa Lazio iliyomaliza nafasi ya sita Serie A ni bora kuliko Angelo Ogbonna wa West Ham iliyomaliza nafasi ya sita katika Ligi ya England.

Kocha aliyeipa mafanikio ya kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2006, Marcello Lippi, aliwahi kusema: “I will not pick players on reputation alone.” Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba hachagui wachezaji kwa kuzingatia ‘ubora pekee’. Kiburi cha Kiitaliano.

Ukija na Bruno Fernandez wako wao wana Lolenzo Insigne, ukimuhusudu Mbappe; wao wanamuhusudu Ciro Immobile. Ndio Waitaliano walivyo.

Ukiipamba EPL, wao mioyo yao imepigwa muhuri wa Serie A. Ndioo. Wataziamini vipi ligi zenu wakati Euro ya mwaka 2000 walicheza fainali na Uholanzi bila kuwa na mchezaji anayecheza nje ya Italia, huku Totti akiibuka mchezaji bora wa mechi?

Umemtazama Ronaldo na Ureno yake dhidi ya Hungary? Mchezaji mkubwa huonekana katika mechi kubwa. Hungary walihitaji miujiza ili kuwafanya wasiadhibhiwe katika mchezo ule wa kwanza.

Mpaka dakika 85, matokeo yalikuwa 0-0, lakini dakika tano za kukamilisha dakika 90 na dakika 4 za nyongeza zikafanya mchezo umalizike kwa Hungary kuadhibiwa mabao 3-0.