DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu 

Jioni ya Ijumaa Juni 18, 2021 nilitazama televisheni za nchini kwetu; Balozi Ramadhan Dau na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, wakimtambulisha Ikulu mwekezaji kutoka Malaysia kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Habari ilikuwa kwamba huyo mwekezaji aje atulimie mpunga na nafaka zinazotumika kusindika mafuta ya kula ili kampuni yake ituuzie/itulishe sisi Watanzania na ziada ya bidhaa hizo ziuzwe nchi za nje.

Nikiwa miongoni mwa wazee hapa nchini nimeshituka kwa kushangaa sana kwa kuona na kusikiliza maelezo ya ugeni tulioletewa. 

Mgeni alimwambia Rais wetu kuwa Tanzania ina ardhi nzuri na idadi kubwa ya watu, na kwamba kutokana na uwezo mkubwa alionao ati tutafanya naye biashara kubwa na nzuri!

Kupitia elimu niliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilijifunza, pamoja na mambo mengine, juu ya serikali dhaifu duniani ambazo ziliwahi kuzembea katika kuwekeza zenyewe kwa dhana ya kujitegemea katika kilimo ili kujenga uwezo wa kujitosheleza kwa chakula. 

Kupitia uzembe huo, Serikali ya Ufaransa iliangushwa na kuondolewa madarakani. Waheshimiwa Dk. Dau na Profesa Mkenda ni vizuri walijue hilo kama somo maalumu. Food security inapochezewa ndani ya taifa lolote lile madhara yake ni kuangushwa kwa serikali iliyoko madarakani.

Kilimo hapa kwetu Tanzania kinaendelea kuchezewa-chezewa na afya ya ardhi nayo tunazidi kuichezea tu bila kujali ongezeko kubwa la watu. Elimu ya ugani licha ya kuwa na vijana wahitimu wengi kutoka katika vyuo, nayo pale inapopatikana inakuwa kama ni hisani tu.

Pembejeo za kilimo licha ya kuzalishwa tena kwa viwango vikubwa ndani ya taasisi za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), bado halmashauri zetu hazina hamasa ya kuzinunua na kuzipeleka kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wetu.

Wazo la kutuletea ugeni wa aina hiyo nimwombe Profesa Mkenda ninayemheshimu, alichambue ipasavyo kwa kushirikiana na JWTZ ambao kama wakipewa mitaji na zana za kilimo kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na taasisi ya mbegu, Tanzania tuna uwezo mkubwa  wa kulima, tena kitaalamu bila kuleta wawekezaji aina ya waliokuja nayo hawa viongozi wetu wawili.

Nimwombe Balozi Dau kwa kuanzia asome kijitabu cha ‘Elimu ya Kujitegemea’ kilichoandikwa na Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1962 na ‘Siasa ni Kilimo’ cha mwaka 1972; pia ‘Afrika Inakwenda Kombo’ kilichotafsiriwa na Ruhumbika kutoka False Start in Africa cha Rene Dumont.

Pia wajifunze juu ya miradi ya Mbarali, Mbeya; Ruchili, Sengerema, Bugorola Murutunguru, Ukerewe; Bugwema, Musoma, Magugu, Babati na Ruvu, Pwani. Miradi yote hiyo na mingine ilikuwa na baadhi bado inashughulika na kilimo cha mpunga.

Kadhalika wajifunze juu ya mchango wa vyuo vya kilimo kama Uyole, Ukiriguru, Tengeru, Nyegezi, Mpwapwa na kadhalika. 

Dk. Dau ninadhani angekuja na ujasiri wa ushauri kwa kuitaka serikali yetu iwe na nidhamu stahiki ya kuheshimu wataalamu wa kilimo, mifugo, uvuvi na kuthamini taasisi hizo.

Kwa kuanzia inabidi tujifunze kutumia mataifa yetu ya hapa Afrika kama Misri, Sudan, na Ethiopia ambako wanatumia vizuri maji ya Mto Nile ambao chanzo chake ni Ziwa Victoria. 

Wao walitumia na bado wanatumia vizuri ujuzi mkubwa wa wanajeshi wao katika vipindi vya amani. Katika majeshi kuna rasilimali kubwa ya askari na maarifa/ujuzi mkubwa. Kuna sayansi na teknolojia, suala la usalama wa chakula wanalijulia fika.

Balozi Dau na Profesa Mkenda ninawashauri kwanza wamwombe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, awaruhusu wakae na wataalamu wa JWTZ ili waelezwe njia rafiki za kupambana na udhaifu wa kilimo chetu kuliko kuleta wawekezaji kuja kutulimia na kutulisha mafuta!

Mimi ninajitoa sadaka kwa kuwaambia Balozi Dau na Profesa Mkenda kuwa tuepuke kumsumbua Rais wetu kwa kumpelekea wageni wawekezaji sampuli ya aina hiyo. 

Matokeo yake ni kujiaibisha. Tanzania hatuna sababu ya kushindwa kujilisha kwa mafuta ya kula. Wawekezaji waje wawekeze kwenye mambo magumu.

Mzee Samwel Kasori ni Katibu mstaafu wa Mwalimu Julius K. Nyerere.

0754372141