DAKAR, SENEGAL

Senegal imetangaza kuwa imeanza maandalizi ya kuzalisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa corona.

Inaungana na nchi nyingine kadhaa za Afrika ambazo nazo zimetangaza mipango yao ya kuzalisha chanjo dhidi ya ugonjwa huo ambao umeisumbua dunia kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Taarifa zinaonyesha kuwa Senegal itaanza uzalishaji wa chanjo hiyo mwakani.

Wiki iliyopita nchi hiyo ya Afrika Magharibi iliingia mkataba na Kampuni ya dawa ya Ubelgiji, Univercells, ili kuanza kuzalisha chanjo hizo kuanzia mwaka ujao.

Wakati nchi kadhaa duniani zilikimbizana kuwapatia chanjo raia wake, Afrika inapata shida kupata chanjo za kutosha kuwachanja wananchi wake kutokana na bara hilo kutozalisha chanjo hizo kwa wingi hivi sasa.

Hadi hivi sasa ni takriban watu milioni saba tu ndio wamepatiwa chanjo dhidi ya corona barani Afrika na dozi nyingi za chanjo zimehodhiwa na nchi tajiri duniani.

Inaaminika kuwa nchi hizo hazitaruhusu chanjo hizo kuja barani Afrika hadi zitakapojiridhisha kuwa zimetosheleza wananchi wake.

Katika harakati za uzalishaji wa chanjo, Senegal inaungana na Misri, Morocco na Afrika Kusini miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimeshatangaza kupata haki ya kuzalisha chanjo.

Ripoti kadhaa zinaonyesha kuwa Kampuni ya UNivercells iliingia makubaliano ya ushirikiano wa kuzalisha chanjo na taasisi ya Senegal iitwayo Institut Pasteur mwezi Aprili mwaka huu.

Univercell ilieleza pia kuwa itahamishia sehemu ya mitambo ya kuzalisha chanjo nchini Senegal katikati ya mwaka 2022 ili kuimarisha kazi hiyo.

Uzalishaji huo utafanyika kwa kuwaajiri wananchi wa Senegal na mara uzalishaji utakaposhika kasi chanjo zitakazozalishwa zitaanza kusambazwa katika nchi za Afrika Magharibi.

Siku chache zilizopita Marekani ilitangaza kusambaza mamilioni ya dozi za chanjo nje ya nchi hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo.

Chini ya mpango huo, Marekani itanunua chanjo kutoka kwa watengenezaji na kuzisambaza katika nchi zenye mahitaji lakini hazina uwezo wa kupata chanjo hizo kwa wingi.


Askari wa jeshi la Senegal akipewa chanjo aina ya Sinopharm iliyotengenezwa nchini China.