LONDON, UINGEREZA
Bei ya mafuta katika soko la dunia imeanza kupanda baada ya kuwa chini kwa kipindi kirefu kutokana na madhara ya janga la COVID-19.
Bei ya pipa moja la mafuta ilifikia dola 70 jijini New York katikati ya wiki iliyopita, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi kirefu.
Kupanda huko kwa bei kunahusishwa na kuanza kuchangamka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kutokana na watu wengi kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya COVID-19.
Inaaminika kuwa jinsi watu wengi zaidi wanavyopatiwa chanjo na hivyo kuondolewa vikwazo vya kusafiri, bei ya mafuta nayo itakuwa ikiongezeka.
Wakati New York ikirekodi kiasi hicho cha bei, huko magharibi mwa Texas inaelezwa kuwa bei ilipindukia dola 70 kwa pipa na kukaribia kufikia kiwango cha juu tangu Oktoba 2018.
Uzalishaji wa mafuta nchini Marekani uliporomoka kwa mapipa milioni 2.11 wiki iliyopita, ilieleza taasisi ya American Petroleum Institute katika ripoti yake.
Hii itakuwa ni wiki ya tatu mfululizo kwa uzalishaji mafuta kushuka nchini humo iwapo takwimu hizo zitathibitishwa na takwimu za serikali zilizotarajiwa kutolewa mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo inatarajiwa kuwa hali hiyo itabadilika baada ya muda mfupi, kwani taarifa zinaonyesha kuwa mahitaji ya mafuta yanaanza kuongezeka duniani.
Kwa mujibu wa REUTERS, kiwango hicho cha bei ya mafuta kilichorekodiwa Alhamisi iliyopita ni cha juu zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Hali hiyo imetokea sambamba na kupanda kwa takwimu za idadi ya watu wenye ajira nchini Marekani kutokana na watu wengi zaidi kupatiwa chanjo dhidi ya COVID-19, hivyo kuruhusiwa kurejea katika shughuli zao bila vikwazo.
Hata hivyo soko la mafuta lilipata msukosuko kidogo baada ya baadhi ya vombo vya habari kutangaza kuwa Marekani ilikuwa imeondoa vikwazo dhidi ya maofisa kadhaa wa Iran ambao wanahusika na kampuni kubwa za mafuta lakini Wizara ya Fedha ya Marekani ikaeleza baadaye kuwa jambo hilo lilikuwa ni la kawaida na halihusiani na mazungumzo ya muda mrefu kuhusu vikwazo ilivyowekewa Iran kutokana na kuendelea na mipango ya kutengeneza silaha za nyuklia.