Makala hii yenye anuani ‘Nafasi ya mwanamke katika Uislamu’ inakusudia kuweka wazi namna Uislamu ulivyompa heshima mwanamke, kinyume cha yale madai kuwa Uislamu umemdhulumu mwanamke na umemnyima haki zake mbalimbali.
Wakati mwingine madai kama haya yanatokana na kukosa kipimo sahihi cha kuupima Uislamu kwa kuutofautisha na baadhi ya matendo ya wanaoitwa Waislamu.
Uislamu unapaswa kupimwa kutokana na miongozo yake: Qur’aan Tukufu, Sunnah (Hadithi) za Mtume Muhammad na kauli za wanazuoni wa Kiislamu zisizopingana na miongozi hiyo miwili iliyotajwa na usipimwe kwa matendo ya baadhi ya Waislamu wasiofuata miongozo ya Uislamu.
Historia inashuhudia kuwa wakati Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) anapewa utume, aliukuta ulimwengu ambao mwanamke hakuwa na haki yoyote katika jamii yake bali alionekana kama bidhaa inayoweza kuuzwa wakati wowote.
Mwanamke alichukuliwa kama chombo cha kumstarehesha na kukidhi matamanio ya kimwili ya mwanamume.
Mwanamke alihesabika kuwa ni chombo cha uzalishaji na hakuwa na uchaguzi na uhuru wa kupanga na kuamua.
Mwenyezi Mungu kupitia Uislamu akamuondolea mwanamke unyonge, udhalili, dhuluma, uonevu na unyanyasaji ule.
Uislamu ukamjengea mwanamke mazingira bora, kanuni na sheria ambazo zitamhakikishia uhuru, usalama, amani, haki na usawa katika jamii yake.
Uislamu ukamtayarishia mwanamke anga zuri, chini ya anga hilo ataishi huku akijihisi kuwa ni binadamu kamili, mwenye haki sawa kama mwanamume na ukamdhaminia kupata haki zote kama binadamu bila ya kuhitaji upendeleo maalumu.
Uislamu ukamuondoshea mwanamke tuhuma ya kumpotosha Baba yetu Adam – amani iwashukie wote – peponi na kuwa yeye (mwanamke) ndiye asili na chanzo cha uovu wote huu utendekao ulimwenguni.
Uislamu ukabainisha kwamba ni shetani mlaaniwa ndiye aliyewapoteza Nabii Adam na mama yetu Hawa, kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 36 kuwa: “Lakini Shet’ani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyokuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda.”
Uislamu unakiri na kutangaza wazi kuwa watu wote bila ya kujali rangi au hali zao kimaisha wameumbwa kutokana na nafsi moja tu.
Haya tunayasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 4 (Surat An-Nisaai), Aya ya 1 kuwa: “Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliyekuumbeni kutokana na nafsi moja…”
Uislamu hapa unabainisha usawa wa wanadamu kutokana na msingi wa kupatikana kwao. Chini ya kivuli cha mfumo huu, mwanamke na mwanamume wanaogelea pamoja katika bahari moja ya usawa wa haki zote za msingi za binadamu bila ya kubaguliwa.
Isitoshe ule utukufu ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu aliompa mwanadamu katika kauli yake tunayoisoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 17 (Surat Al-Israai-Bani Israil), Aya ya 70 kuwa: “Na hakika tumewatukuza wanaadamu…”
Huu ni utukufu aliozawadiwa mwanadamu yeyote bila kuangalia ni mwanamume au mwanamke, wote wanashirikiana kwa usawa katika utukufu huu.
Qur’aan Tukufu inapomzungumzia mtu au wanadamu, basi huwa inamkusudia mwanamume pamoja na mwanamke. Na pale inapotaka kumtaja mwanamume au mwanamke peke yake bila ya kumhusisha mwenzake, basi hutumia istilahi ‘wanaume’ au ‘wanawake’.
Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anazidi kuudhihirishia ulimwengu nafasi aliyonayo mwanamke katika Uislamu pale alipotuonyesha uhusiano uliopo baina ya mwanamume na mwanamke katika kauli yake iliyo katika Kitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kiitwacho Sunan Abi Dawoud kuwa: “Wanawake ni ndugu – baba mmoja, mama mmoja na wanaume, wanayo haki kwa sheria (kufanyiwa na wanaume) kama ile haki iliyo juu yao kuwafanyia wanaume.”
Istilahi ya ndugu – baba mmoja, mama mmoja aliyoitumia Bwana Mtume inatoa sura kamili ya usawa baina ya mwanamke na mwanamume.
Kwa jicho la Uislamu, wanaume na wanawake kiasili ni sawa bila tofauti yoyote mbele ya Mola wao, na kwamba tofauti na ubora utajitokeza katika amali njema anazozifanya kila mmoja wao. Ni dhahiri kuwa mzuri na mwingi wa amali njema hawezi kulingana sawa na mchache wa amali njema bila ya kuangalia ni mwanamume au mwanamke, hii ndiyo mojawapo wa misingi na kanuni za Uislamu kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 16 (Surat An-Nahli), Aya ya 97 kuwa: “Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyokuwa wakiyatenda.”
Uislamu unazidi kumthibitishia na kumhakikishia mwanamke nafasi ya usawa kwa kumpa fursa sawa ya kukubaliwa na kujibiwa dua sawa sawa na mwanamume bila ya kupoteza amali zake njema.
Hili linathibitishwa na Qur’aan Tukufu tunaposoma Sura ya 3 (Surat Ali-Imraani), Aya ya 195 kuwa: “Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanyakazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi waliohama, na waliotolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika mabustani yanayopita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake yapo malipo mema kabisa.”
Ukizingatia kwa makini utaona muundo wa maelezo ya Qur’aan Tukufu “NI NYINYI KWA NYINYI” unatufahamisha kuwa kuna hali ya kutegemeana baina ya mwanamume na mwanamke na kwamba maisha ya kila mmoja wao hayakamiliki bila ya kushirikiana na mwenziwe.
Uislamu umempa heshima mwanamke na kumkomboa kutoka katika utumwa wa kutumikishwa na mwanamume. Pia umemkomboa kutoka katika madhila ya kuwa bidhaa rahisi isiyokuwa na hadhi wala heshima. Miongoni mwa mifano inayohusiana na heshima kwa mwanamke ni hii ifuatayo:
- • Uislamu umempa mwanamke haki yake ya kurithi, katika mgawanyo mzuri na wa uadilifu. Katika baadhi ya mgawo, anakuwa sawa na mwanamume, na katika mgawo mwingine anatofautiana na mwanamume kwa kuzingatia uhusiano wake na kwa kuzingatia gharama za huduma anazotakiwa kuzipata.
- • Uislamu umefanya usawa kati ya mwanamume na mwanamke katika mambo mengi tofauti. Miongoni mwa mambo hayo ni miamala yote ya kifedha, mpaka Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akasema kama tunavyosoma katika Kitabu cha Hadithi za Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kiitwacho Sunan Abi Dawoud kuwa: “Wanawake ni ndugu wa damu wa wanaume.”
- • Uislamu umempa mwanamke uhuru wa kuchagua mume. Pia umempa sehemu kubwa ya wajibu wa kulea watoto. Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema kama tunavyosoma katika vitabu vya Hadithi za Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) viitwavyo Sahih Bukhary na Sahih Muslim kuwa: “Na mwanamke ni mchungaji katika nyumba ya mume wake, naye ataulizwa juu ya kile alichokichunga.”
- • Uislamu umemwachia mwanamke jina lake na heshima ya nasaba ya baba yake. Nasaba yake haibadiliki baada ya kuolewa, na ataendelea kujinasibisha na baba yake na familia yake. Hili linasaidia kuhifadhi utambulisho wa mwanamke huyu. Kinyume chake ni mwanamke kubadilika jina lake la ukoo kwa kubadilika wanaume aliofunga nao ndoa katika kipindi cha maisha yake.
- • Uislamu umempa mwanaume wajibu wa kumtunza na kumhudumia mwanamke, bila ya masimango au masimulizi, kama mwanamke huyo ni miongoni mwa wale ambao ni wajibu kwa mwanamume kuwapa huduma, kama vile mke, mama na mtoto wa kike.
- • Uislamu umelitilia mkazo jambo zuri la kumhudumia mwanamke dhaifu ambaye hana mtu wa kumhudumia, hata kama si ndugu yako. Uislamu umehamasisha kuhangaika ili kumhudumia, na umelifanya jambo hilo kuwa miongoni mwa ibada bora sana mbele ya Allah. Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema kama tunavyosoma katika vitabu vya Hadithi za Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) viitwavyo Sahih Bukhary na Sahih Muslim kuwa: “Mwenye kumhangaikia mjane na maskini ni kama mwenye kupigana Jihadi katika dini ya Allah, na ni kama mtu anayesali usiku hampumziki, na ni kama mtu anayefunga saumu hafungui.”
Nihitimishe makala hii kwa kubainisha kuwa mama akiwa ni sehemu ya wanawake amepewa daraja kubwa kuliko baba, mwakilishi wa wanaume.
Tunasoma katika vitabu vya Hadithi za Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) viitwavyo Sahih Bukhary na Sahih Muslim vikimnukuu Swahaba Abu-Huraira (Allah amuwie radhi), akisema kuwa: “Alikuja mtu mmoja kwa Mtume na kumuuliza kwamba: Ewe Mjumbe wa Allah, ni mtu gani ana haki zaidi kwangu kuishi naye vizuri? Mtume alijibu: Ni mama yako. Yule mtu akauliza tena: Kisha ni nani? Mtume akajibu: Kisha ni mama yako. Yule mtu akauliza tena: Kisha ni nani? Mtume akajibu: Kisha ni mama yako. Yule mtu akauliza tena: Kisha ni nani? Mtume akajibu: Kisha ni baba yako.”
Tukutane Jumanne ijayo, In-Shaa-Allaah!
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
Muhimu:
Makala hii imewahi kuchapwa katika gazeti hili na imerudiwa kutokana na maombi ya wasomaji wetu – MHARIRI