ADDIS ABABA, ETHIOPIA
“Kuna njaa hivi sasa huko Tigray.” Ni kauli liyotolewa na ofisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock, na kuwashtua watu wengi.
Alikuwa akielezea hali ilivyo katika Jimbo la Tigray nchini Ethiopia ambalo kwa miezi kadhaa limekuwa katika mapigano baina ya majeshi ya jimbo hilo na yale ya serikali kuu.
Maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo na hivi sasa wanaishi kwenye makambi kama wakimbizi.
Aliitoa kauli hiyo katika kikao cha utangulizi kabla ya kikao cha viongozi wa nchi saba tajiri duniani (G7) kilichofanyika Uingereza mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kauli hiyo iliwashtua viongozi wengine wa G7, kwani kwa muda mrefu walidhani kuwa suala la Tigray lilishapatiwa ufumbuzi baada ya kutangazwa kukoma kwa mapigano miezi kadhaa iliyopita.
Ripoti iliyotolewa na UN inaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 1.8 wanaoishi katika makambi maeneo ya mijini katika jimbo hilo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Lakini kibaya zaidi ni kuwa nyuma ya namba hizi kuna madhila makubwa sana ambayo baadhi ya watu wanapitia, ikiwamo vifo.
Imeelezwa kuwa iwapo msaada wa haraka wa chakula hautapelekwa katika jimbo hilo katika kipindi kifupi kijacho, upo uwezekano na idadi ya vifo kuongezeka.
Ukiacha hali hiyo inayoonekana katika kambi zilizopo mijini, kuna maelfu ya watu wengine wanakabiliwa na hali mbaya ya chakula katika maeneo ya vijijini.
Ripoti kutoka katika vijiji vilivyo mbali inaonyesha kuwa watu wengi hawana chakula na kibaya zaidi hakuna namna au mpango wa kuwasaidia.
Pia lipo kundi la wanawake ambao walitekwa na wanajeshi wakati wa vita na kulazimishwa kufanya ngono, ambao hivi sasa wanatunzwa katika hospitali kadhaa bila uangalizi wa karibu.
Vita katika jimbo hilo ilianza Novemba mwaka jana baada ya jeshi la jimbo hilo kujitangazia madaraka zaidi, jambo ambalo lilipingwa na serikali kuu iliyoamua kupeleka majeshi yake kuzima kile ilichokiita uasi.
Wengi wa wanaokabiliwa na njaa hivi sasa ni watoto ambao ndio pia wanaofariki dunia kwa wingi kutokana na njaa. Takwimu zilizotolewa hivi karibuni jimboni humo zinaonyesha kuwa takriban watoto 300,000 wanahofiwa kufariki dunia kutokana na kukosa chakula.