Na Joe Beda Rupia
Ni msiba mkubwa mjini Sumbawanga. Huenda msiba huu ndio mkubwa zaidi kuwahi kuukumba Mkoa wa Rukwa tangu Februari 1994 alipofariki dunia Askofu Karolo Msakila.
Dk. Chrisant Majiyatanga (jina la utani la baba yake alilorudi nalo nyumbani kutoka Tanga) Mzindakaya. Mwanasiasa. Mzee wa kimila. Mwekezaji mzawa. Kondakta wa zamani wa mabasi ya Wastara. Mbunge. Naibu Waziri. Mkuu wa Mkoa… Hatunaye tena duniani.
“Ilikuwa ni fitina tu ‘we mwanche we’ (wewe mtoto)! Bado unakumbuka!” amewahi kuniambia hivyo mzee Mzindakaya miaka kadhaa iliyopita nilipokutana naye Dar es Salaam na kumuuliza kama ni kweli alimpiga kofi wakati wa kampeni Gilbert Ngua, mgombea mwenzake wa ubunge mwaka 1980.
Tukio hilo linadaiwa kutokea wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika Shule ya Sekondari Kantalamba. Hata hivyo, Mzindakaya anakanusha akiniambia huku akitabasamu (kama kawaida yake): “Yale yalikuwa maneno ya mtaani tu.”
Pamoja na wanafunzi wa Kantalamba kumpa kura nyingi Ngua katika uchaguzi huo, Mzindakaya, kama kawaida, alishinda kwa kishindo.
Ndio. Zilikuwa ni kampeni za ‘jembe’ dhidi ya ‘nyumba’. Alama zilizokuwa zikitumiwa na wagombea enzi za uchaguzi wa chama kimoja.
Aghalabu, anayepewa alama ya ‘jembe’ kule kwetu Ufipa, alikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda. Naambiwa Mzindakaya mara nyingi, kama si mara zote, alama yake ilikuwa ‘jembe’; na alikuwa hodari sana kutetea dhana au umuhimu wa jembe dhidi ya nyumba.
Ngua akakata rufaa. Kesi ikanguruma Mahakama Kuu, Mbeya. Mwaka 1981, huku akiwa ameshateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, ushindi wake ukatenguliwa.
Akanyang’anywa gari la uwaziri palepale mahakamani. Akarejea kijijini kwake Sumbawanga. Akawa balozi wa nyumba kumi.
“Ile kesi ilikuwa na lengo la kumdhalilisha tu. Matajiri wa Sumbawanga waliipanga na kuisimamia. Akashindwa,” anasema mzee Paulo Wazwila Kipeta, mkazi wa Mtowisa aliyefanya kazi kwa karibu na Mzindakaya tangu mwaka 1964.
Mzee huyu mzaliwa wa Izimba Misheni, amestaafu kazi mwaka 2007.
Mzindakaya hakudumu sana katika ubalozi wa nyumba kumi, kwani mwaka huo huo, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akamteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, eneo alikoporwa ubunge na gari la uwaziri.
Kusema ukweli Mzindakaya ni mtata. Alipoanza kazi mkoani Mbeya, akasema: “Nimekuja hapa kama nyati aliyejeruhiwa!”
Kauli ambayo haikuwafurahisha ‘wanyambara’, wakaiona kama ina kisasi ndani yake. Wakapiga kelele hadi akahamishiwa Morogoro baada ya muda mfupi sana.
“Labda kuna watu hawafahamu. Ukweli ni kwamba mapinduzi ya kilimo mkoani Morogoro yalifanywa na Mzindakaya.
“Aliamuru matrekta ya Chuo cha Kilimo (siku hizi SUA) kwenda kuwalimia wananchi mashamba yao. Akagawa maeneo ya kilimo. Akagawa mbegu bora,” anasema mzee Kipeta.
Kwa hakika msomi huyu wa Tengeru alikuwa kiongozi haswa! Ni bahati mbaya kwamba ‘wakubwa’ kule SUA, kwa mujibu wa mzee Kipeta, hawakufurahishwa na uchapakazi wake, hasa upande wa kusimamia kilimo. Wakamuundia ‘zengwe’.
Kukazuka mgogoro wa ‘kimasilahi’ kati yake na SUA, ikidaiwa kuwa alitaka kujiunga na chuo hicho ‘uzeeni’ wakati hana vigezo. Wakamkatalia. Akakasirika. Hatimaye akahamishwa. Akapelekwa Kigoma.
Kama ilivyokuwa Morogoro, Mzindakaya akapeleka hamasa kubwa ya kilimo mkoani humo. Akaanzisha kilimo cha kisasa cha michikichi (mawese). Kwa asili mzee huyu ni mkulima. Kazi ya mababu zake wa Ufipa, hivyo haikuwa ajabu kwake kupenda kusimamia kilimo. Kigoma ikabadilika.
“Hiyo ndiyo kazi yake. Mzindakaya. ‘Uwikolo wa nchito’ (mzee wa kazi),” anasema William Mseo a.k.a Intambo wa Maka, Ofisa Ardhi Wilaya ya Moshi, mwenyeji wa Sumbawanga ya Wenyeji.
Maisha ya Mzindakaya mkoani Kigoma yalijaa visa na mikasa. Mingine mikubwa kweli kweli!
Kukazuka madai ya ‘wizi’ wa mapipa ya lami zaidi ya 100! Lami kwa ajili ya barabara za mji wa Kigoma/Ujiji ‘imepotea’! Itapoteaje? Utawabebea mbeleko gani Waha!
Kwamba watu wameamka asubuhi, wakakuta eneo yalipokuwapo mapipa hayo linawaka moto. Lami imeungua. Yote!
Lami inaungua yote kwa usiku mmoja! Haieleweki.
“Mkuu wa Mkoa (Mzindakaya) anahusika. Yeye na wenzake wameuza lami yetu Zaire,” minong’ono ikazagaa vijiwe vya Bangwe, Mwanga, Mnarani hadi Ujiji.
Wabunge wa mkoa huo wakaungana na kulifikisha suala hilo bungeni. Katikati ya mjadala, Oktoba 1993, Mbunge wa Kigoma Mjini, Rajab Mbano, anafariki dunia ghafla.
Wazee wa Kigoma wanadai kuna ‘mkono wa mtu’. Kidole cha lawama kinaelekezwa kwa Mzindakaya. Wanasema watalipa kisasi. Wanampiga marufuku kuhudhuria msiba. Anagoma. Anahudhuria na kumzika mbunge ‘wake’. Hotuba kali zinatolewa makaburini.
Yakafuata yakufuata (hayaandikiki). Mzee Ali Hassan Mwinyi akaamua kumhamishia Mzindakaya nyumbani, Rukwa.
“Wala ile lami haikuuzwa Zaire kama walivyokuwa wanadai watu wa Kigoma! Serikali iliihamisha,” anasema mzee Kipeta bila kufafanua ilihamishiwa mkoa au mji gani.
Mwaka 1995 akagombea ubunge na kushinda kama alivyoshinda tena mwaka 2000 na 2005. Akastaafu mwaka 2010 sambamba na mkongwe mwenzake, Paul Kimiti, akiwa amedumu bungeni kwa miaka 45 huku Kimiti akilitumikia Bunge kwa miaka 35. Vingunge wa Sumbawanga hawa! Si mchezo.
Ni katika kipindi hiki cha pili cha ubunge wa kuchaguliwa ndipo Mzindakaya alipolitikisa taifa kwa kuibua kashfa nzito nzito bungeni kiasi cha kupachikwa jina la ‘mzee wa mabomu’.
Alikuwa akisimama bungeni, viti upande wa mawaziri vinawaka moto! Kashfa za mafuta ya kula na sukari ziliwaondoa madarakani mawaziri wawili akiwamo ‘mwamba’, Idi Simba.
Huo ni umaarufu wake kitaifa. Lakini Mzindakaya hakuwa na mchezo hata nyumbani, hasa Sumbawanga.
Kwanza, alishiriki kikamilifu katika mchakato ulioanzishwa na Mwalimu Nyerere wa kuundwa Mkoa mpya wa Rukwa mwanzoni mwa miaka ya 1970.
“Hoja ikawa makao makuu ya mkoa yawe wapi? Malumbano yakaanza. Watu wa Mpanda wakiongozwa na mjumbe wa NEC (ya TANU), Mzee Kalubu, wanataka yawe Mpanda,” anasimulia Mzindakaya nilipozungumza naye miaka mingi iliyopita.
Hoja ya Kalubu ni kwamba wakati huo mji wa Mpanda ulikuwa na miundombinu bora kuliko Sumbawanga. Lami. Umeme. Dhahabu. Kubwa zaidi reli!
Mzindakaya akashtuka. Akaanzisha kampeni kuipiku Mpanda. Wakati huo Nyerere akampeleka Michael Baruti masomoni Urusi kusomea masuala ya utawala, akimwandaa kuwa mkuu wa mkoa huo mpya. Nyerere ni baba wa ubatizo wa Baruti.
“Hapo ndipo Mzindakaya akapata mwanya wa kufanikisha kampeni yake. Akaenda kumwomba Askofu James Sangu (wa Jimbo la Mbeya) asaidie kupata majengo ya ofisi za mkoa. Askofu Sangu akamshawishi Askofu Msakila.
“Msakila akakubali kutoa bure majengo ya kanisa yaliyopo Kantalamba. Akawaambia (akina Mzindakaya) wachukue na majengo ya Community Centre yaliyopo Mazwi; wamuachie kanisa tu,” anakumbuka mzee Kipeta.
Majengo hayo mazuri na ya kisasa yalitosha kuupa mji wa Sumbawanga uwezo wa kuwa makao makuu ya mkoa. Kalubu na timu yake hawakuwa na habari kuwa tayari Sumbawanga wamepata majengo ya ofisi! Kampeni zikaendelea. Kimyakimya!
Mzindakaya akamshawishi Felix Mwanambilimbili, m-NEC kutoka Chunya (wakati huo Chunya ikitarajiwa kuwa ndani ya Mkoa mpya wa Rukwa kwani ilikuwa Jimbo la Magharibi – Western Province, Tabora), aunge mkono hoja ya Sumbawanga kuwa makao makuu ya mkoa. Akakubali.
Baruti anakaribia kurudi kutoka masomoni kuchukua mkoa wake. Malumbano yanaendelea; wapi pawe makao makuu?
Ikalazimika wilaya tatu za mkoa mpya; Sumbawanga, Chunya na Mpanda, zipige kura. Sumbawanga ikashinda kwa kura mbili dhidi ya moja ya Mpanda. Ikawa makao makuu.
Mwaka 1974, Rukwa ikazaliwa na kaulimbiu ya ‘Rukwa Ruka’ ikiwa na wilaya mbili tu; Mpanda na Sumbawanga. Chunya ikaenda Mbeya. Baruti akawa mkuu wa mkoa wa kwanza.
“Kazi ya mzee Mzindakaya hiyo. ‘Umonsi wa masumo’ (mwanaume wa shoka)! Alikuwa mzalendo wa kweli wa Rukwa. Aliipenda sana! Na alikipenda Kifipa wala hakujificha,” anasema Mseo.
Miaka yote Mzindakaya ni mfanyabiashara na mwekezaji. Ana kiwanda cha kisasa zaidi cha kuchakata nyama mjini Sumbawanga.
Miaka ya 1970 na 1980, alihamasisha na kuhakikisha kila kijiji cha Mkoa wa Rukwa kinakuwa na mashine ya unga. Akasimamia mpango wa kila kijiji kuwa na gari kubwa la mizigo.
Akaanzisha viwanda vidogo vya mafuta ya kula vijijini. Hadi leo viwanda hivyo vipo au vimebaki katika vijiji vya Laela na Mtowisa ambako kuna kiwanda cha seketa.
Vijiji vikakopa na kununua magari aina ya Isuzu. Ni kwa kukosekana usimamizi mzuri tu ndiyo maana malori na mashine havikuendelea, sivyo vijiji vya Rukwa vingesonga mbele kweli kweli.
“Mzindakaya akishirikiana na akina Mfupe na Kameka, wakaanzisha kampuni kubwa ya usafirishaji. Lyangalile Transport Company,” anasema mzee Kipeta.
“Ndiyo maana nilisema Mzindakaya ni mzalendo wa Rukwa. Hata uamuzi wa kutumia jina ‘Lyangalile’ ni ishara ya kuenzi historia ya mkoa wetu,” anasema Mseo.
Historia inaonyesha kuwa Lyangalile ni eneo la kiutawala la Ufipa ya juu lililokuwa likiongozwa na Mwene Maria, makao yake Mpui na maeneo ya Isakalilo; huku eneo la kiutawala la Ufipa ya chini likifahamika kama Nkansi chini ya Mwene Kapele (au Kapufi?).
Maeneo haya ya kiutawala yalikuja baada ya utawala wa asili wa Milanzi (Milansi) chini ya Ntatakwa kudorora.
Kampuni ya Lyangalile haikudumu sana hasa baada ya serikali kuanzisha Rukwa RETCO.
Poleni Watanzania, poleni wana Rukwa na Katavi; poleni wana Sumbawanga.
‘Uupite lwa mpemba, monsi wa masumo!’