ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Baraka Mohamed Shamte, ameyatilia shaka matamshi ya mara kwa mara ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, akisema yanaweza kuvuruga upepo na ustawi wa umoja wa kitaifa.

Akizungumza na JAMHURI, Shamte anasema pia si sahihi kuzungumzia shauri ambalo bado lipo mahakamani.

Othman amekaririwa akisema wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ, alimshauri aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, kuhusu kukamatwa kwa masheikh wa uamsho.

“Matamshi kama haya hayana msingi wala nia njema. Mwanasheria Mkuu wa SMZ na Makamu wa Pili wa Rais wote ni wateule wa Rais.

“Hivyo kama kweli alikusudia kuishauri SMZ, alitakiwa kwamza akutane na Rais (mstaafu) Dk. Ali Mohamed Shein, kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria na si kutoa madai haya wakati Dk. Shein hayupo madarakani,” anasema Shamte na kuongeza:

“Masheikh wa uamsho na wengine wote walikamatwa chini ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, si SMZ. Kwamba alimshauri Makamu wa Pili ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, ni sawa na kuichokoza CCM iingie kwenye malumbano na ACT-Wazalendo.”

Anasema hadi sasa watuhumiwa hao wapo katika mahabusu za Tanzania Bara kwa mujibu wa sheria, hivyo si Othman (akiwa Mwanasheria Mkuu), Balozi Idd wala Dk. Shein ambao wangezuia kukamatwa kwao.

Shamte anasema hata katika kesi ya kukutwa na nyaraka za siri za SMZ iliyowahi kumkabili Maalim Seif Sharif Hamad miaka ya nyuma, alilazimika kukata rufaa Mahakama ya Rufaa  Tanzania ndipo akaachiwa huru.

“Kwa hiyo kuhoji sababu za masheikh hao  kushitakiwa Tanzania Bara ni upotoshaji, wala kwa muundo uliopo sasa chini ya dola moja, hauwezi kuhoji sababu hizo.

“Kudai kwamba alimwambia Makamu wa Pili badala ya Rais, inaonyesha kwamba Othman anataka kumsakama bure Balozi Idd. 

“Wapo wengi tu waliowahi kukamatwa hapa Zanzibar na wakapelekwa Bara. Iweje hoja na mjadala uwe kwa masheikh wa uamsho?” anahoji Shamte.

Kada huyo anashauri na kusema ni vema Othman akasubiri uamuzi wa mahakama badala ya kutaka kuwapaka matope wenzake ambao kwa sasa hawana jukwaa la kumjibu.

“Kwa nini hasemi iwapo pia alikwenda kumshauri Maalim Seif (wakati huo akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais)? Watu wakijitokeza na kudai kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulitokana na ushauri wa Maalim, ayaafiki? Matamshi kama haya lazima yawe na indhari ili yasizushe malumbano,” anasisitiza.

Matamshi mengine ya Othman yanayomtia shaka Shamte ni yale kwamba watu wote wapatiwe vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi (ZAN ID) ili waje kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, akisema hatua hiyo inalenga kuamsha utata siku zijazo.

Shamte anasema suala la kila mtu kuwa na ZAN ID ni jambo jingine na ukaazi hadi kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni suala la kisheria.

“Sheria inamtaka mtu atimize masharti ya ukaazi wa miaka mitatu kwenye shehia husika huku akitambuliwa na Sheha wake.

“Mara kadhaa nimekuwa nikimsikia (Makamu wa Kwanza wa Rais) akizumgumzia uchaguzi uliopita na kusema haukuwa huru na wa haki. Hivyo ni vijembe vya uchokozi dhidi ya wenzake. Amekuwa akidai wapo baadhi ya viongozi wameshika madaraka kwa kura za ‘nguvu za kiza’. Hivi navyo ni vijembe. Vikijibiwa kwa aina ya vijembe, hapatakalika,” anasema.