Kuna wakati niliwahi kuandika waraka nikauliza baadhi ya maswali ambayo nilidhani waliosoma wangesema hili tulijadili kidogo badala ya kupita kimyakimya. 

Haikuwa hivyo, na kwa kweli ninaendelea kuumia sana kwa sababu sioni mahali ambapo tunasisitiza kuacha majungu. Badala yake tunatafuta namna ya kuimarisha taaluma ya majungu.

Sina hakika sana kama hili pia ni moja ya mambo ambayo ni ya kisasa na yatanifanya nionekane wa zamani sana, niliyepitwa na wakati. 

Ninajua kwamba kuzungumza mambo ambayo hayana ukweli wowote na kuleta taharuki katika jamii, hasa iliyostaarabika ni ushamba. Kama nitagombezwa kwa kusema ukweli huu niko tayari kuubeba msalaba.

Katika waraka wangu wa wakati huo niligusia juu ya vyombo vya habari ambavyo kimsingi vina nguvu sana katika jamii yetu. 

Vyombo hivi vinatuelimisha, vinatupa habari na matukio na vinatuburudisha pia baada ya kazi nzito ya kutafuta riziki ya kutwa.

Vyombo hivi kwa mujibu wa sheria vipo kisheria, pia vyombo hivi kuna wakati vilidai nafasi ya kuwa mhimili unaoweza kujitegemea, na kwamba usiingiliwe. 

Kwangu nilitaka kukubaliana na mawazo hayo kwa sababu ninajua umuhimu wa taarifa na elimu ndani ya vyombo hivi.

Isivyo bahati, waliokuwa mstari wa mbele kushadidia suala hili ambalo lilianzishwa na nguli wachache ambao waliona manufaa ya mhimili ni wale waliokuja kujulikana kama watu wasio na taaluma katika kutoa habari na kuelimisha. 

Wachache tuliopata bahati mpaka leo ya kupitia baadhi ya vyombo hivyo, iwe televisheni, redio au majarida mbalimbali tumeona balaa juu ya balaa katika mhimili huu mpweke.

Suala hili halina mjadala kabisa wa kitaifa, ni suala la kuingia katika teknolojia yetu na kupakua baadhi ya maudhui ambayo yamo na kujiuliza je, hiki ndicho kilichodhamiriwa na hao wachache wenye weledi katika kutaka tasnia ya habari kuwa mhimili unaojitegemea?

Kuna kichefuchefu fulani ambacho kinapatikana katika mitandao yetu ya habari. Kwanza unaweza ukadhani kuwa taifa hili linaishi na watu ambao hawana weledi wowote katika masuala ya habari, lakini pili, utaona jinsi ambavyo tunalishwa mambo tofauti na yale ambayo tumeahidiwa katika taarifa hizo. 

Ninajua kuna vyombo mbalimbali vya kuweza kudhibiti haya, lakini vinabanwa na sera ya sheria zetu na kitu kinachoitwa uhuru wa watu kupata habari.

Katika waraka wangu ule wa wakati huo nilihoji uhalali wa kuletewa taarifa ambayo si niliyokusudia. Nilihoji uhalali wa kudanganywa kama mdau na mpokea taarifa, tena kwa gharama kubwa ya kisimbusi au intaneti. Nilihoji faragha za watu ambazo kimsingi zinapaswa kulindwa kisheria, pia nilihoji namna ya kuhakiki habari, kwa maana ya kuwa na pande zote mbili. Mwisho, nilihoji uwezo wa mtoa habari kwetu kitaaluma.

Haya ni maswali ambayo nilidhani ningejibiwa kwa wakati, lakini nikaona kimya. Leo tunashangilia kwa sababu jambo lenyewe halituhusu sisi ambao majina yetu na taarifa zetu hazijatajwa katika mhimili huo. 

Leo tunashangilia kwa sababu tunapata taarifa za kufurahisha nafsi zetu bila kujua nafsi zingine zilizoguswa zinaumia kiasi gani.

Mwanahabari mmoja aliwahi kusema: “Ogopa sana teknolojia ya Mungu.” Ninakubaliana naye kwa sababu teknolojia haipotezi taarifa mapema. 

Teknolojia hii tunayoiacha ikusanye maudhui na kuyatupa hewani ni dhahiri kuwa inaweka maktaba nzuri ya taarifa mbaya kwa vizazi vijavyo. 

Ni wazi kwamba kuna watu watakuja kujutia utoto wao na kuwakosesha haki ya faragha ukubwani. Ni dhahiri kwamba kuna wazazi watawapa laana watoto wao pindi watakapokuwa na uwezo wa kutaka kujua nafasi ya wazazi katika ujana wao.

Ninajua wapo wenye mamlaka ya kudhibiti na linawauma sana. Ninajua wapo wenye taaluma yao juu ya tasnia ya habari nchini na inawakera sana. 

Lakini pia ninajua lipo kundi kubwa ambalo linapenda taarifa hizo ambazo hazina tija kwa taifa letu, ndilo linaloogopwa katika kuchukua hatua. Rai yangu ninaomba tuvae viatu vya wenye kuumizwa na si wenye kufurahi.

Naamini wenye kujua umuhimu wa habari watalikumbusha hili ili siku moja tasnia ya habari uwe mhimili unaojitegemea katika taifa letu. 

Hapo tutapata maendeleo, tutapata elimu, tutapata burudani, tutaona umuhimu wa habari, kinyume cha hapo tutaendelea kulishwa umbeya unaowaumiza wengine.

Lakini waraka wangu wa wiki ninataka kuwauliza wanazuoni na wanataaluma wenye kisu kama kweli hapa ndipo tumefika kwa sasa bila hatua zozote kuchukuliwa, lau kama sivyo, basi tunawaomba mkatae lisiwe taifa la umbeya tu.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.