Taifa lolote duniani linajengwa na nguvu kubwa ya vijana. Wao ndio kundi kubwa na pana katika shughuli za kila siku za binadamu.
Ingia katika fani yoyote utakutana na vijana. Rika hii muhimu inaanzia katika umri wa miaka saba hadi thelathini na tano, na pengine hadi arobaini.
Vijana hawa wanapatikana katika jinsia ya kike; yaani wasichana na wa kiume – wavulana. Ingawa watu mara kadhaa wanapozungumzia vijana ukweli wanawalenga wavulana na kuwasahau wasichana. Ama hakika tendo hili ni udhalilishaji wa kijinsia. Wakati umefika watu kutanabahi hili.
Kijana ni mtu mwenye fahamu zake; mtu mwenye nguvu. Anayetambua jema na baya, mwenye kupima jambo gani au lipi la kulifanya kwa masilahi yake na wenzake, bila kupuuza umoja ni nguvu katika kuleta maendeleo ya jamii.
Taifa letu la Tanzania lina vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa. Wazee ni wachache. Vijana hawa tuna imani nao kwamba wanao uwezo mkubwa wa kufanya kazi bila kusukumwa. Fahamu zao, vipaji vyao, uwezo wao na maarifa yao pamoja na hekima walizopewa na wazazi wao, watafanya kazi kwa weledi.
Walimu katika shule zetu za awali na msingi ni tegemeo kubwa la taifa kuona wanachapa kazi kwa weledi na umakini kutoa vijana wadogo wenye uelewa wa masomo.
Watoto hawa wanapopata misingi mizuri ya adabu, afya na ukakamavu wanakuwa na msimamo imara katika kupokea mafunzo ya elimu ya juu.
Wahadhiri nao katika vyuo mbalimbali viwe vya elimu ya juu, ufundi, utabibu na kadhalika wanapata mwendelezo mzuri wa kupokewa mafunzo.
Kazi zao zinatazamiwa kutia fora pale wahitimu wanapokwenda kufanya kazi maofisini, viwandani na mashambani.
Mlolongo huu unapouangalia kwa undani, utamaizi ni vijana ndio walioshika hatamu za kujenga elimu bora, uchumi imara, uongozi na utawala makini. Vijana hawa wanapokosa hekima na maarifa, ukweli taifa linakuwa la kuyumbayumba.
Malezi ya vijana yanaanzia nyumbani ndani ya familia. Walezi wakuu ni wanawake, ambao wanatokana na vijana wa kike.
Vijana hawa wasipolelewa vema ni dhahiri hawataweza kutoa mafunzo mema kwa vijana wadogo ambao taifa lina weka mategemeo makubwa ya kupata maendeleo yake.
Leo katika taifa letu, unapoangalia shughuli ndogo ndogo za uchumi, utaona idadi kubwa ya watu wanaoshughulika na ujasiriamali ni vijana wa kike wakishirikiana karibu mno na mama zao. Si katika uchumi tu, angalia katika masuala ya siasa, sheria, utawala na kadhalika.
Ukweli vijana hawa wanaweza na wanajituma kwa hali na mali. Wanadhihirisha wanawake wana uwezo, maarifa, elimu, hekima na busara katika kufanya kazi mbalimbali ndani ya jamii. Hili si jambo geni na halina ubishi. Ni sayansi iliyofuta udhanifu kuwa vijana wa kike hawajiwezi.
Jambo la msingi ni vijana wa kiume kukubali na kukiri kwamba vijana wa kike wanao uwezo mkubwa, pengine hata kuupita ule uwezo walionao.
Hapa inatupasa na sisi watu wazima na wazee kuona na kuzingatia kwamba mabinti wetu wanao uwezo wa kufanya kazi na kuongoza.
Aidha, vijana wa kike wasibweteke na kuamini wao katika shughuli za maendeleo ya taifa ni watu wa daraja la pili. Hapana.
Wote wamo katika daraja moja la kwanza. Jambo linalotakiwa ni umoja na mshikamano katika kufanya kazi za maendeleo ya taifa letu.
Watanzania wenzangu tunapowazungumzia vijana tuelewe ni wa kike na wa kiume. Wote ni vijana na wana haki sawa katika kupewa malezi, elimu, hekima na maarifa. Maendeleo ya taifa yanahitaji watu, na watu wenyewe ni hawa vijana.
Wiki ijayo tutaangalia chimbuko la wanawake kutengwa katika shughuli za maendeleo na wanawake kuwekwa katika shughuli za maendeleo.