*Wakili Madeleka auliza maswali magumu

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, amezungumza na Gazeti la JAMHURI na kusema suala la Uhamiaji kutoa visa feki gazeti limepotoshwa na mtoa habari.

Waziri Simbachawene ameliambia JAMHURI kwamba Uhamiaji hakuna mtandao wa uhalifu na wizi wa visa kama ilivyoelezwa na mtoa taarifa.

Amesema Uhamiaji ni moja ya idara ambazo zipo chini ya wizara yake na anafahamu kuwa uwepo wa mtandao wa visa feki ni suala lisilowezekana, kwani kwa sasa unatumika mfumo wa kielektroniki.

Anasema kwa sasa baada ya kuanza kutumika kwa pasipoti za kielektroniki (e-Passport), pia vibali vya kazi (work permits), vya kuingia nchini (visa) na vingine navyo vilianza kutolewa kwa njia ya kielektroniki.

“Sasa utagundua kuwa hakuna uwezekano wa kuwapo kwa visa feki nchini au mtandao wa uhalifu wa aina hiyo,” anasema Simbachawene na kusisitiza kuwa uadilifu walionao watendaji na wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji hana shaka nao.

Simbachawene anaonyesha shaka yake akisema huenda wanaoilalamikia idara hiyo nyeti kwenye vyombo vya habari, hususan Gazeti la JAMHURI, wakawa ni watu wenye hasira au chuki za aina fulani zinazotokana na masuala binafsi kati yao na idara.

“Wanafahamika. Lakini hawapaswi kuwa na chuki dhidi ya Idara ya Uhamiaji au maofisa wa Uhamiaji, kwa kuwa si wao waliowashitaki,” anasema.

Anasema hata waliofikishwa mahakamani mwaka 2019 walipelekwa kwa mujibu wa sharia, ambapo ni Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ndio wanaohusika na masuala ya kesi.

Hoja kwamba maofisa waandamizi wanapata migawo ya fedha nyakati nyingine wala hawajui zilikotoka, Simbachawene anasema huku akicheka:

“Kwa kawaida mtu hawezi kupokea fedha asizofahamu zilikotoka. Nani atakupa fedha kwa namna hiyo? Kweli hili linawezekana jamani? Mmeingizwa chaka. Katika hili kubali tu kuwa mmechemka.”

Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea Peter Madeleka, ambaye alikamatwa kwa tuhuma za kushiriki kughushi visa mwaka 2019, ameliambia JAMHURI, akisema:

 “Naomba niweke kumbukumbu sawa kuhusu malalamiko yangu:

 “1. Tarehe 2/8/2019 Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia udhibiti wa mipaka Ndugu Samwel Mahirane aliutangazia umma kuwa amemkamata JASMIN ALLY NGONGOLO katika Uwanja wa Ndege wa JNIA akiwa na VIZA FEKI zenye thamani ya Sh bilioni 1.4. Je, jambo hili ni kweli au si kweli? Mamlaka zinazohusika au yeyote mwenye mamlaka anijibu.

“2. Baadaye ilifunguliwa kesi ya uhujumu uchumi Namba 81 ya mwaka 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Mimi nikiwa mtuhumiwa namba 6 nikishitakiwa pamoja na mambo mengine kughushi VIZA. Je, jambo hili ni kweli? Mamlaka zinazohusika au yeyote mwenye mamlaka anijibu.

“3. Mnamo tarehe 12/5/2020 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliniachia huru baada ya DPP kutokuwa na nia ya kunishitaki. Je, jambo hili ni kweli? Naomba mamlaka zinazohusika zinijibu jambo hili.

“4. Kama kweli tangu mwanzo walikuwa na ushahidi kwamba ninahusika kughushi VIZA, kwanini mashitaka dhidi yangu yalifutwa? Naomba nijibiwe swali hili kwa usahihi.

“5. Kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haijanitia hatiani kwa kosa la kughushi VIZA, je, mashitaka dhidi yangu yalikuwa ni ya HILA ili kunikomoa?

“7. Je, kwa nini Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wanashikilia mali zangu wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilishaniachia huru tangu tarehe 12/5/2020?”

Madeleka ameliambia JAMHURI kuwa yeye yuko tayari kufungwa ikiwa alishiriki mtandao wa visa feki, ila anachofahamu mtandao huo upo na unafanya kazi kwa usiri mkubwa, kisha akaongeza: “Kuwa electronic, haiondoi ukweli kuwa hakuna physical document. Kama tunavyopewa passport bado hata stika za viza zinatolewa. Hapo ndipo kuna mambo. Mimi ninasema wanijibu hayo maswali kama hakuna viza feki, hizo walizokamata ni nini?”

 Hoja kwamba mke wake alikuwa anafanya kazi Uhamiaji na yeye anawatetea wateja wanaolalamikiwa na Uhamiaji, amesema: “Mke wangu kama wakili hajipangii kazi. Anao wakubwa zake wanaompangia kazi na mimi kama wakili wa kujitegemea siwezi kukataa mteja kimaadili eti kwa sababu ametoka Uhamiaji anakofanya kazi mke wangu.”

Kuhusu wafanyakazi wanaofukuzwa au kuhamishwa kiholela, Waziri Simbachawene amesema hadi mfanyakazi anafukuzwa, zinakuwa zimepitiwa hatua nyingi na baadhi ya watumishi wanaofukuzwa mtu akisikia wanayoyatenda atabaki ameshangaa.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, amesema yeye atakuwa tayari kuzungumza akikutana uso kwa uso na mwandishi ofisini kwake Dodoma.