Badala ya utaratibu wa zamani sasa waonyesha sinema wamebuni utaratibu mpya wenye kuwawezesha watu wasioona kuangalia sinema sambamba na watu wanaoona.
Teknolojia hii ya aina yake, iko sawa na zile zinazotumika kwenye ndege ikiwa angani, ambapo mtu anaweza kufumba macho lakini bado akaendelea kusikiliza sinema hatua kwa hatua.
Wakati Aziz Bouallouchen akiingia katika jumba la sinema katika mji wa Marrakesh nchini Morocco, tofauti na ilivyo katika majumba mengi ya sinema siku hizi wateja wanapewa miwani maalum ya picha ya 3D, yeye anapewa vinasa sauti vinavyovaliwa kichwani (headphones).
Bouallouchen, ambaye umri wake ni miaka 20, si mwendaji sinema wa kawaida, na hili si jumba la sinema la kawaida. Kila kiti ndani ya jumba la sinema kina vifaa maalum vya kusaidia wapenda filamu wasioona.
Filamu kama Lalla Hoby, ambayo ni filamu maarufu ya vichekesho nchini Morocco kuhusu mtu ambaye anavuka bahari ya Gibraltar kumsaka mke wake aliyemkimbia na kwenda kuishi na mwanaume mwingine nchini Ubelgiji, inatazamwa mno.
Filamu hiyo ilitoka mwaka 1996, na ni filamu pekee kutoka Afrika Kaskazini kuwekewa maelezo ya maneno ndani yake.
Akiwa amevaa vinasa sauti ambavyo vimeunganishwa katika vishikio vya kiti, Bouallouchen anasikiliza sauti inayoelezea mfululizo wa matukio, ishara za watu na matukio ambayo usiposikia unapoteza mwelekeo wa filamu.
“Ni wazo zuri sana,” anasema Bouallouchen. “Sijaweza ‘kutazama’ filamu tangu nilipopatwa na maradhi yaliyosababisha kupoteza uwezo wa kuona.”
Sauti kutoka vinasa sauti maalum kuelezea matukio ya filamu baasa ya kuisikia anasema: “Lakini sasa nahisi kama sehemu ya ulimwengu wa filamu.” Bouallouchen alipoteza uwezo wa kuona mwaka 2005 baada ya kupatwa na maradhi yaitwayo Behcet’s syndrome yaliyoshambulia mishipa ya macho.
Miaka saba baadaye, amejikuta akiwa amekaa sambamba na watu wanaoona, “wakitazama” filamu pamoja. Na hiyo ni kutokana na maelezo ya maneno, kila mmoja anacheka wakati mwafaka katika vichekesho vya Lalla Hoby, akionekana kuanguka katika boti ndogo katika bahari ya Gibraltar.
Morocco inaongoza barani Afrika katika matumizi ya teknolojia hii mpya. Sauti inazungumza “sambamba” na matendo katika filamu na hutoa taswira njema zaidi kwa watu ambao hawawezi kuona.
“Sisi ni nchi pekee barani Afrika na katika mataifa ya Kiarabu ambao tunatoa huduma hii kwa wasioona,” anasema Nadia el-Hansali wa Wakfu wa Tamasha la Filamu la Marrakesh.
Wakfu huo, ambao unaandaa matamasha mengi makubwa ya filamu, ambapo filamu zenye maelezo ya sauti kwa wasioona zimekuwa zikioneshwa kwa miaka miwili, unatenga fedha kwa ajili ya filamu zote ziwe na viwango vya kuonekana na watu wasioona.
Filamu nane mpaka sasa zina maelezo ya sauti, ikiwemo L’Atlante ya mwaka 1934, The African Queen (1951) na East of Eden (1955).
Katika kipindi cha miezi 18 ijayo, filamu nyingine sita zitawekewa huduma hiyo ya maelezo ya sauti.
“Tumetazama kuona kiasi gani cha kusema na kipi ni muhimu kwa ajili ya filamu nzima kueleweka”
El-Hansali huandika mswada (script) kwa ajili ya wacheza sinema ili wasome sambamba na matukio katika filamu.
Iko kamilifu kabisa, na sauti huingia katikati ya mapengo kati ya mazungumzo ya wacheza sinema.
“Tumetazama kuona kiasi gani cha kusema na kipi ni muhimu kwa ajili ya filamu nzima kueleweka,” amesema el-Hansali.
“Naepuka kutoa taarifa nyingi kupita kiasi ambazo zitawachanganya wale wasio na uwezo wa kuona skrini.” Lengo ni kuondokana na mtindo wa zamani wa kutumia watu kutoa maelezo ndani ya sinema, huku wakiwa wamesimama, wakijaribu kuelezea kinachoendelea, lakini mara nyingi hutoa maelezo hayo wakati mazungumzo muhimu katika filamu yakiendelea.
Mohamed Doukkali, mhadhiri asiyeona wa falsafa katika chuo kikuu cha Rabat nchini Morocco, ni mshabiki mkubwa wa teknolojia na yeye hutumia kompyuta maalum katika kazi zake za kila siku. “Moja ya mambo muhimu ya teknolojia mpya ni kuwa huondoa vikwazo vinavyokukabili,” anasema Doukkali.
Anajielezea kama mtu “mpenda filamu”, lakini mara nyingi hutazama DVD akiwa nyumbani pamoja na mtu anayemuelezea kinachoendelea. Amefurahishwa sana sasa kuwa hatimaye anaweza kwenda sinema.
“Pongezi kwa sauti ambayo inatoa maelezo ya kinachoendelea na tunaweza kufuatilia filamu katika njia ambayo hatukuweza kufuatilia zamani,” amesema. “Unafurahia zaidi kutazama filamu ukiwa umejumuika na watu wengine wengi, kitu ambacho ndio hasa lengo la sinema.”