Na Bashir Yakub
Wenye nyumba mnatakiwa kujihadhari sana. Hakikisha unapompangisha mtu unajua historia yake. Wakati mwingine ni vigumu lakini ndiyo iko hivyo.
Unalazimika kufanya hivyo kutokana na madhara ambayo unaweza kupata kutokana na makosa ya mpangaji.
Kifungu cha 20, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kinawahusisha hadi wenye nyumba ikiwa nyumba anayomiliki patakutwa dawa za kulevya.
Ikumbukwe dawa za kulevya ni pamoja na bangi. Kifungu hakizungumzii kukuta tu dawa za kulevya ndani ya nyumba bali pia kuvutia humo, kunusia humo, kuuzia, kutengenezea, kuhifadhi, kujidunga nk.
Shughuli yoyote kati ya hizi ikifanyika ndani ya nyumba, mwenye nyumba naye anaingia katika makosa.
Na si lazima iwe nyumba, hadi eneo kama uwanja au eneo lolote shughuli ya namna hii ikifanyika, mwenye eneo naye anaingia katika makosa.
Kifungu hakijasema kwamba mwenye nyumba ama eneo hataingia hatiani kama alikuwa hajui kama shughuli hiyo inafanyika, au hajaruhusu.
Maana yake ni kwamba uwe ulikuwa unajua ama haujui, uwe uliruhusu ama hukuruhusu, haijalishi, madhali tu hiyo shughuli imekutwa kwako, basi unayo makosa.
Adhabu yake panapo hatia ni faini ya Sh milioni tano, kifungo miaka mitatu au vyote.
Kwa hiyo utaona wazi kuwa ni wajibu mwenye nyumba kujua historia ya anayempangisha.
Sheria imefumba macho kwa kukataa utetezi wa mwenye nyumba kama alikuwa anajua achofanya mpangaji au hajui, kwa sababu kama kutokujua kingekuwa kigezo, kila mwenye nyumba ambaye angekuwa anakamatwa kwa kosa hili angesema alikuwa hajui. Kila mmoja angejitetea hivyo.
Haya ni baadhi ya mambo ambayo watu hujikuta wamo ndani ama magerezani na kubaki na mshangao. Mtu anahisi ameonewa kumbe ipo sheria inasema hivyo. Kwa hayo, ni muhimu sasa tujihadhari.