Asanteni sana nyote mnaoniunga mkono kwa kupokea barua yangu ya kila wiki kupitia ukurasa huu. Nia na madhumuni ya barua hii ni kukumbushana na kutoa au kuwasilisha maoni yangu kwa jamii kuhusu maisha yetu ya kila siku, sanjari na utamaduni wetu.

Kwa msomaji wa siku nyingi atajaribu kukumbuka baadhi ya barua za wosia wangu kwa watumishi wa umma au binafsi na suala la madaraka waliyonayo. 

Niliwahi kuandika barua dhidi ya unyenyekevu kwa tunaowatumikia na jinsi ya kutokujisahau katika maisha hasa pale unapopewa mamlaka.

Sisi wahenga tunajua jinsi ambavyo tumepita katika mapito mengi ya utawala bora na ule ambao si utawala bora, tangu enzi za kodi ya kichwa tupo na tunashuhudia jinsi dunia inavyopita na mapito yake. Ni dhahiri kwamba ukiishi sana kuna kitu utapata fursa ya kukijua, nacho ni madaraka, ni kama koti la kuazima tu.

Nimeianza wiki hii kwa bahati sana ya kukutana na mwakilishi wetu wa jimbo wakati tukipata uhuru, jambo la kwanza tumepeana kongole kwa kuchaguliwa na Mwenyezi Mungu kuendelea kuwapo mpaka leo ili tuwe mashahidi wa maisha ya mpito. 

Jambo la pili, tukapata fursa ya kuteta kidogo kwa yale ambayo yanaendelea katika dunia ya haraka kwelikweli, nasi pia tulikuwa tukijitahidi kujadili huku tukikimbia na mawazo kama kizazi cha leo.

Ni kweli kwamba maisha yanakwenda kasi sana lakini hatupaswi kupishana na maadili yetu na kutoa utu wetu, wakati wetu kuna mambo yalikuwa ni magumu sana kuyakabili kama ilivyo leo, si kweli kwamba yalikuwa hayafanyiki la hasha! Yalikuwa yanahitaji staha na stara katika jamii.

Ilikuwa ni vigumu sana kumuona kiongozi akiwa na kashfa ya kufanya usaliti katika ndoa yake, kuishi na mke ama mmoja au zaidi bila kuvunja ndoa ilikuwa ni moja ya sifa ya mtu kuwa kiongozi wetu, mara nyingi walioshindwa kuwa na ndoa imara walijikuta hawachaguliki kuongoza watu, hii ni dhana ya tofauti kabisa na uongozi wa sasa.

Sasa hivi tunawachagua viongozi bila kuangalia maisha yao ya kifamilia, tunaangalia umaarufu na kutapanya fedha wakati wa uchaguzi, sasa hivi tunaviongozi wengi waliochaguliwa na wananchi lakini siyo familia zao, jambo hili linafikirisha sana unapofikiria uwakilishi wa jumla kama jamii.

Uongozi enzi zetu lilikuwa suala la kujitolea zaidi katika ngazi zote, iwe chama au serikalini, hili halina ubishi kwamba wengi wao walijitolea na hata wengine walijitolea mishahara yao kukatwa kwa ajili ya mahitaji ya jamii maskini zaidi wakati huo.

Wakati wetu viongozi walisikiliza matatizo ya wananchi na kuyatatua papo kwa hapo, iwe kwa kushirikiana au kutumia akili na uwezo wao kumaliza tatizo lenyewe. Leo hii idadi kubwa ya viongozi wanakuja kutusikiliza ili nao waende wakalalamike mbele kana kwamba tumeamua kutafuta muongeaji, si kiongozi.

Wananchi tunalalamika na viongozi wetu wanalalamika na sisi tunawachagua walalamishi ili wakalalamike tusaidiwe matatizo tunayoyalalamikia, kiongozi anayejitahidi kutafuta fursa ya kuonekana analalamika ili wananchi tuone analalamika ili tumchague tena akalalamike wakati ujao.

Kiongozi anayeangalia masilahi kwa janja ya kusema anataka kututumikia wananchi kwa moyo wake wote, kumbe ni kwa mahitaji yake yote, kiongozi anayebishana juu ya masurufu na mapato yake bila kuangalia anaowaongoza.

Kiongozi anayeonekana simba baada ya kumpa madaraka kisheria, kwamba tunamsujudu badala ya kutusujudia, kwamba anataka tumtambue kwa cheo, si jina lake lililompa kazi, kwamba ndiye mtoa amri mkuu bila kuangalia tuliomchagua na kibaya zaidi sisi tulimchagua aliyesoma kutuzidi kiasi kwamba hahitaji tena ushauri kutoka kwetu sisi mazoba.

Najua barua yangu itahitaji muda mrefu kuandika juu ya mapito ya kiutawala tangu enzi za mkoloni mpaka miaka ya sasa ya maisha bora ni siasa na uteuzi na si kilimo na ufugaji tena, kwamba maisha yanabadilika na wao ndio wanaobadilika na siyo sisi tunaowachagua.

Kichwa kinapata moto lakini waraka ujao nitaangalia kwa jicho jipya la kizamani ni nani ambaye anapaswa kuwa kiongozi wetu katika uchaguzi ujao, nitauliza ni hawa wabakaji, wahujumu, wezi, wenye dharau, wapika majungu, wanafiki, wanaojiita wazalendo au ni wapi? 

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.