Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Hii ni methali kongwe katika lugha yetu ya Kiswahili, ikiwa ibebeba ujumbe muhimu katika kuongoza watu kupata ufanisi mkubwa pindi wanapoamua kufanya jambo katika hali ya kushirikiana. 

Watu walio makini mara nyingi wanapenda kufanya kazi zao kwa njia ya ushirika, kwani wanatambua mtu mmoja peke yake hawezi kupata maendeleo. Ili afanikiwe katika kusudio lake ni vema kujiunga na wenzake, na hapo hupata mafanikio makubwa. Na hayo ndiyo tunayoyaita maendeleo.

Maendeleo yoyote yanapatikana kwa watu kufanya kazi pamoja. Iwe katika kazi kiwandani, kilimo shambani, michezo michezoni na kadhalika, alimradi kutimiza azima au lengo la ushindi na mafanikio. Shughuli zote hizo na nyinginezo katika siasa, ulinzi, utamaduni na uchumi, umoja unahitajika.

Chama cha uganga, michezo, siasa na kadhalika, na kadhalika, msingi au shina lake ni UMOJA. Tunapata umoja kuanzia katika familia, jumuiya hadi taifa. Kumbuka na angalia Umoja wa Nchi za Afrika – AU,  Umoja wa Nchi za Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika – SADC, Umoja wa Mataifa – UN na umoja wa kila jambo katika dunia hii.

Binafsi nakili kutamka Umoja ni Maendeleo. Kama hivyo ndivyo, watu au taifa halina budi kuthamini na kuenzi umoja. Watu waTanganyika na Zanzibar walipokuwa wanadai Uhuru na haki zao kutoka kwa wakoloni walianzisha umoja. Umoja huo uliwaongoza katika harakati zao za kuondoa ukoloni. 

Naam, walifanikiwa. Leo Tanganyika na Zanzibar hazipo, iko Tanzania. Nchi inayosonga mbele kuleta maendeleo yake ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Katika muktadha huu wapo baadhi ya Watanzania waona umoja ni jambo dogo sana na la kipuuzi!  Watu kama hawa si bure, wana lao jambo.

Watu hawa usiku na mchana wanafanya hujuma za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa lengo la kuvunja umoja wa Watanzania. Kila siku tunasikia na kusoma katika vyombo vyetu vya habari, chama fulani cha siasa kina mgogoro, maofisa wa serikali wamekwapua fedha, wananchi wameharibu miundombinu ya usafiri na usafirishaji n.k.

Wote hao shabaha yao ni kuvunja umoja wa nchi kwa maana ya kuweka utengano kati ya wenye nia na wasio na nia. Huo ndiyo udhaifu. Watu hawa mara nyingi wanaonekana mbele ya jamii wana sura moja; kumbe wanazo sura mbili. Sura ya utu  na uungwana wakati  wa mchana, na sura ya unyama na ukatili wakati wa usiku.

Wapo viongozi wanaojifanya wema katika umoja kumbe ni waovu. Ndio hao tunaowaita wasaliti. Wapo wanaojikweza ni waalimu wa mambo kumbe ni matapeli na wezi. Lakini tukumbuke wapo wanaojionyesha ni watetezi wa haki na wapenda watu, kumbe ni wanafiki. 

Kauli zao ni tamu mbele ya majukwaa na sura zao zimejaa tabasamu na ukarimu. Lakini nyoyo zao zina inda na choyo. Ukweli watu wa aina hii ndio wanaovunja umoja. Umoja unapokuwa katika hali kama hii utambue umo shakani. 

Nguvu inahitajika. Nguvu inayohitajika ni kuwaelewa, kuwabainisha hadharani na kuwatoa katika umoja. Kazi ya uchunguzi iwe imara na wana umoja wawe madhubuti katika kuwakabili waovu hawa. Ama sivyo maendeleo yao waliyoyapata yatayeyuka kama theluji juani.

Nimenena haya kutokana na watu mbalimbali wanavyohujumiwa katika umoja wao. Jambo la msingi ni kutoa hadhari na watu wenyewe wakubali na kuamini kweli umoja wao umo shakani. Wanapobaini umoja wao umo shakani, wasikubali kuyumbishwa na hao wanaojifanya wataalamu wa umoja.

Wana umoja popote walipo wanao wajibu kwanza wa kujichunguza wao wenyewe wapo kamilifu? Pili, wanao moyo wa ujasiri na wapo tayari kukabili mapambano kulinda maendeleo yao yasitetereshwe na wajanja wa siasa na taaluma? Tatu, daima watambue ndani ya umoja wamo wasaliti, wezi na wahujumu uchumi wa umoja.

Nakamilisha makala hii kwa kurudia kusema, umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Yaani ushirikiano katika kufanya jambo una manufaa makubwa kuliko kufanya kazi kwa ubinafsi. Nawaaga kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi iendelee.