BAGAMOYO
Na Umar Mukhtar
Wapo baadhi ya watu wasiotaka kukiri kuwa miongoni mwa wanasiasa waliowahi kutokea Afrika ambao ni wajuzi wa mapiku ya kisiasa na masuala ya utawala kuwahi kutokea; watu wenye maarifa mapana na mizungu ya kisiasa wanaozijua vema mbinu zake, hususan Afrika Mashariki na Kati; Rais (mstaafu) wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, ni miongoni mwa wanasiasa hao.
Watu hawa ndio wale alioamua kuwazungumzia wakati wa mazishi ya mwendazake, John Magufuli, kule Chato, akisema walizusha maneno ya ajabu wakidai kuwa Kikwete hampendi Magufuli.
Wazushi hawa wameendelea kumzushia mitandaoni mambo kadhaa ya ajabu ajabu kiongozi huyu, mtu wa watu! Ajabu sana.
Hawafahamu kwamba mbele ya kizazi kilichotangulia cha wanasiasa katika safu ya kundi la kina Dk. Kikwete walikuwapo wanasiasa nguli kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mzee Nelson Mandela, Patrice Lumumba, mzee Jomo Kenyatta, Dk. Kwame Nkrumah, mzee Abeid Aman Karume, mzee Daniel arap Moi na Samora Machel.
Wengine ni Dk. Augustino Netto, Abdul Diof, Kenneth Kaunda, Seretse Khama, Robert Mugabe, Ahmed Sekou Toure, Sam Nujoma, Muamar Gaddafi na viongozi wengine kadhaa mashuhuri barani Afrika.
Makala hii inajaribu kumpambanua Kikwete tofauti na anavyochukuliwa na wazushi hawa ambao hawafahamu kuwa kwa mwanasiasa kusoma na kupata elimu ya juu ni katika nyongeza ya kutanua wigo wa ufahamu wa mhusika mwenyewe, lakini kiuhakika siasa itabaki kuwa ni johari itokanayo na ibra au kipaji cha ajabu.
Mwanasiasa lazima awe na mvuto na mvumo wa sauti inayoweza kuishi katika jamii kwa wakati wote akiwa yu hai.
Pia ajaaliwe muonekano wenye haiba ya ushawishi kwa mwanasiasa mhusika, mwenye maarifa thabiti, aliyejawa na mbinu ya jinsi atakavyomudu na kuzichanga vema karata zake hadi zikamfikisha mahali anakokusudia afike.
Vyovyote itakavyokuwa, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne amejipambanua kuwa mwanasiasa wa viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa, kutokana na wepesi wake katika kuhifadhi na kufuatilia mambo anuai, anayojituma na kutoa michango ya fikra, kujawa na mawazo endelevu na ukwamuzi katika mikwamo pale mambo yanapotaka kwenda mrama na kisha kuonyesha njia mbadala.
Wapo wanaoeleza kuwa kitendo cha Dk. Kikwete kubahatika kufanya kazi akiwa karibu na Mwalimu Nyerere kwa miaka kadhaa, kumemsaidia sana kuifahamu siasa vilivyo, kutambua njia zake pia akapata uwezo wa kutega na kutegua mitego na mambo magumu katika wakati ambao wengine hawawezi kutegemea.
Si hivyo tu, lakini pia Dk. Kikwete ambaye mara tu baada ya kuhitimu elimu yake ya juu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuamua kuingia kwenye siasa katika Chama cha TANU, baadaye CCM, amebahatika kuwakuta wanasiasa wajuzi walioshiriki mapambano ya kupigania uhuru wa Tanganyika, hali iliyomuongezea maarifa na ujuzi.
Hata kufanya kazi kwake katika maeneo tofauti nchini akishika nyadhifa kadhaa muhimu katika chama na serikali, kunatajwa ndiko kulikokuza fikra zake na kupata uwezo mkubwa wa kufafanua mambo, kujieleza na kumjengea uhusiano na watu wengi wa ndani na nje na kujikuta akiungwa mkono na kuwa mashuhuri.
Pia kubahatika kwake kuhamishiwa Zanzibar kikazi akiwa ofisa katika Ofisi ya CCM Kisiwandui, kuishi na wanasiasa wakongwe aliobahatika kufanya nao kazi kwa miaka kadhaa; kumemzidishia ufahamu, maarifa na jinsi ya kuicheza vema michezo ya kisiasa.
Dk. Kikwete aliyeteuliwa na Rais wa Awamu ya Pili, mzee Ali Hassn Mwinyi kuwa Naibu Waziri wa Maji na Nishati, baadaye akawa Waziri wa Fedha na kuteuliwa tena kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huko ndiko kulikomnoa na kuyapevusha maarifa yake na kupata ukomavu.
Kwa mara ya kwanza tena katika kipindi kigumu mno cha ushindani wa kisiasa, ni pale alipochukua fomu ya kuwania urais mwaka 1995 na kuingia hatua ya ‘tatu bora’, akapitwa na hayati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ndipo alipodhihirisha kwamba Dk. Kikwete si tu kwamba amepevuka kisiasa, bali pia amekomaa na anatosha kuitwa mwanasiasa bora.
Ushindani (na washindani wake) ulikuwa mgumu sana hadi kuingia hatua ya tatu bora. Lilipotangazwa jina la Benjamin Mkapa kuwa ndiye mshindi aliyeteuliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, wajumbe ndani ya mkutano huo walionekana kugawanyika na taharuki ikatanda, hivyo kuwatia hofu baadhi ya viongozi vigogo.
Hata hivyo, baada ya Mwenyekiti wa CCM (wakati huo) mzee Mwinyi kumtangaza Mkapa kama mshindi, Kikwete akaomba asimame na kusema machache mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu, huku kukiwa kumetanda wasiwasi na kutofahamika kile atakachokisema.
Makundi ya mashabiki wake walishaanza kuzungumza kwenye korido huku baadhi yao wakitoa maneno ya kukera kwa kumuona mgombea wanayemuunga mkono ameshindwa ilhali wao wakiamini ndiye aliyeshinda; joto la wasiwasi likazidi kutanda.
Aliporuhusiwa na mwenyekiti kuzungumza, ndipo Kikwete alipodhihirisha ukomavu wake, kupevuka kwake kisiasa na kuthibitisha kuwa yeye si tu kwamba ni mwanasiasa, bali pia ni mvumilivu na mchezaji stadi wa mchezo huo mgumu; siasa.
Hotuba yake iliyokuwa fupi si kwamba iliwashangaza wafuasi na mashabiki wake, bali pia iliwastaajabisha hata mahasimu wake na kumuona si mwanasiasa wa kawaida.
Hiyo ni kutokana na ujasiri wa maneno aliyoyatoa mbele ya Mwalimu Nyerere, ambaye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuinuka na kumfuata Kikwete, akamkumbatia kwa bashasha na furaha kubwa.
Kikwete akawaeleza kinagaubaga mashabiki wake, akianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumfikisha mahali alipofika, kisha akawaeleza kuwa uchaguzi na uteuzi kwa mwaka huo wa 1995, umekwisha.
Kwamba mgombea urais ameshapatikana na huyo ndiye mgombea urais wa CCM ambaye jina lake ni Benjamin Mkapa.
Tena akasisitiza mara kadhaa kuwa mgombea ameshapatikana na uamuzi halali umeshapita na kwamba huyo ndiye mgombea wa CCM atakayepambana na yule wa upinzani na wala hakutakuwa na kikao kingine cha uteuzi; hivyo akatamka kuvunjwa kwa kambi yao na kwamba tangu wakati huo mgombea atakayeungwa mkono ni Benjamin Mkapa.
Alipoteuliwa na Rais Mkapa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ndipo mwanasiasa huyo alipohama katika siasa za ndani na kuwa mwanadiplomasia wa kimataifa.
Alifanikiwa kuonyesha uwezo na kipaji chake, kwani katika utawala wake tangu mwaka 2005 hadi 2010, amejijengea mlahaka mwema na mataifa makubwa duniani.
Kwa ambao hawamjui, hawamuelewi na wale wanaohadaika na muonekano wa haiba yake ya upole, ukimya, kupenda kwake cheko na kila mtu, sasa wanataka kumjaribu na kumdhihaki kiongozi huyo ambaye uwezo na sifa zake ni za viwango vya kimataifa.
Ni mwanasiasa mwenye nguvu na mipango mingi, anayetosha kuitwa ni mwamba na nguzo isiyotikisika, na mbio zake haziwezi kukamatika kutokana na kujaaliwa akili na maarifa.
Majuzi katika kongamano la maadhimisho ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Kikwete amedhihirisha tena umahiri, uhodari, upeo na ujuzi wake, akishiriki kwenye vikao mbalimbali vya kikanda akiwa nyuma ya wanasiasa wote wakongwe kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alijipambanua kama hazina ya historia kwa namna alivyokuwa akilielezea chimbuko la kuundwa kwa SADC, alivyokuwa akisimulia harakati za mapambano kusini mwa Afrika, siasa za ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, mikakati ya ukombozi na jinsi ya uendeshaji wa vikao vya ukombozi hadi kutoka gerezani kwa mzee Mandela na mataifa mengine kuwa huru! Kwa hakika alithibitisha ujabali wake wa kisiasa.
Lakini sasa katika hali ya kushangaza, wamejitokeza watu ambao ninathubutu kusema kwamba hawakupata malezi mema wala maadili.
Hawa wamekuwa ni wakosefu wa nidhamu wakijaribu kumpaka matope na kutunga propaganda za kijinga wakitaka kumshusha kwenye kiti chake cha ‘nguli wa siasa’, lakini bila mafanikio.
Kutaka kumchafua Dk. Kikwete ni sawa na mtu au vikundi vya watu wapuuzi kuamua kuulinganisha Mlima Kilimanjaro na kichuguu; au kuufananisha Mto Ruvu na Ziwa Victoria.
Ni sawa na kutaka kujaribu kuogelea kutoka Bagamoyo kwa matamanio au matarajio ya kufika Zanzibar ukiwa mzima wa afya.
Iwapo kuna kikundi, vikundi, watu fulani, aidha wanaotumiwa na watu waovu, wanaojituma kwa azima ya kuchumia tumbo ili wapate shibe kwa jasho la dhambi, wajiandae siku moja mizimu ya Afrika itawaumbua na kupata fedheha isiyosahaulika daima.
Hata wale waliokuwa wakisemea vibaya ndani ya vibuyu, waliokuwa wakimzushia na kumnanga bila hatia kiongozi huyo huku wengine midomo yao ikiwekwa mikanda ya kaseti na kujikuta wakiropokwa au kufundishwa kejeli dhidi ya mtu aliyewahi kuliongoza taifa kwa nia njema, siku moja mizimu ya Afrika itawatokea na kuwasuta chini ya misitu ya mibuyu.
Ifahamike kuwa Kikwete ni hazina kubwa kwa Tanzania na hata Afrika, kwa kuwa nyuma yake ndiko kuna kundi na rika la wanasiasa aina ya kina Mwalimu Nyerere.
Katika kundi la Dk. Kikwete, Afrika Mashariki, utakutana na wanasiasa mahiri kama Raila Odinga, Moses Wetangula, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi. Hawa ni kutoka Kenya.
Uganda wapo watu kama kina Dk. Kiiza Bisigye na Jenerali Mugisha Muntu.
Huko Zimbabwe mwanasiasa anayeonekana kurithi uongozi ni Jonathan Moyo na Morgan Tsvangirai wakati Afrika Kusini wakachomoza kina Chris Hanni na Steve Biko.
Hapa kwetu wapo kina Kanali Abdulrahman Kinana, Edward Lowassa, George Mkuchika, Kapteni Jaka Mwambi, Kapteni John Chiligati, Kasapira, Kapteni Ditopile Mzuzuri na Azan Al Jabry.