Ilipokuja Awamu ya Pili ya Mzee Ruksa (Ali Hassan Mwinyi) mimi sioni kwa nini aliendeleza ule utamaduni wa kuongea Kiingereza katika dhifa zile za kitaifa au hata aendapo nje ya nchi yetu.

Kulikuwa na ugumu gani kwa Mzee Ruksa kumwaga uswahili wa lafudhi ya mwambao hata watu wakajua sasa Tanzania ina utaifa? Sielewi mpaka leo, bado naona ni kasumba ya ukoloni mtu kujifikiria eti akiongea kwa lugha ya taifa lake Wazungu mabwana zetu hawatamthamini au watampuuza kama vile si wa ulimwengu wa kisasa. Na kwa mazoea hayo na dhana namna ile, kiongozi anaendeleza ukoloni kwa kuongea Kiingereza hali yuko ndani ya nchi na taifa lake lililo huru.

Wajapani kwa kuendeleza lugha na mila na utamaduni wao, mataifa yote ya ulimwengu huu yanakiri kuwa ni Taifa. Enzi zile za ubaguzi, Afrika Kusini, makaburu walidharau sana watu weusi na watu wenye rangi mchanganyiko, wakawaita “coloureds”– iwe Wahindi, Wachina, Wavietnam na kadhalika kwao ilikuwa mamoja tu ni “coloureds”, lakini Wajapani waliwajumlisha katika uzungu wao na wakawaita Wajapani kama “whites”. Hadi leo mataifa yote ya Ulaya na Marekani, wanaweka Wajapani kama moja ya mataifa makuu ya ulimwengu huu – ni weupe wenzao. Kisa? Wana mila na utamaduni usiotetereka wala kuyumbishwa.

Nchi zote ulimwenguni alama kuu ya utaifa wao ni LUGHA yao na mila na utamaduni wao. Sisi vipi lugha ya Kiswahili hatuionei fahari? Mfaransa, Mwingereza, Mjerumani, hata Mreno, lugha kwake ni alama nambari moja kwa utambulisho wa mataifa yao. Huku sisi eti Bendera ya Taifa ndiyo alama nambari moja. Lugha ya taifa haimo kabisa katika kitabu cha Alama za Taifa.

Juzi juzi niliona kwenye runinga katika dhifa ya Taifa, Rais wetu Jakaya Kikwete akitumia lugha ya kigeni – Kiingereza kumkaribisha mgeni wake, Rais wa Ujerumani. Huyu bwana aliposimama tu akakipiga Kijerumani kile kile cha Bavaria, tena kwa madaha kweli. Nikasema lakini Watanzania kulikoni? Kiswahili hakifikishi ujumbe sahihi kwa wakubwa mpaka tutumie Kiingereza?

Hapa natoa uzoefu wangu kidogo juu ya fahari wanazoonea wenzetu kwa lugha na mila zao. Septemba, 1965 nilikwenda Bulgaria kutafuta nafasi za masomo ya uhandisi kwa vijana wetu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Umoja wa Vijana wa Bulgaria. Kule niliambiwa ili watu wetu wasome, itawapasa mwaka mmoja wasomee lugha ya Kibulgaria, na wakishakuhitimu ndipo wasomee uhandisi kama watoto wa kule Bulgaria.

Wao hawana mfumo wa vyuo vya wageni, bali wana vyuo vya uhandisi kwa Wabulgaria wenye kuteuliwa (who merit) kuingia vyuoni humo. Huu ndio mtindo wa mataifa yote duniani. Ukifanikiwa kupata nafasi katika chuo chochote huko majuu unalazimika kusomea lugha yao kwa mwaka mmoja na ukifaulu ndipo unastahili kama watoto wa kule kuingia vyuo vya juu.

Ndivyo ilivyo kwa Ufaransa, Ujerumani, Russia, China, Italia, Japani, Ureno, Sweden, Norway, Ubelgiji na kadhalika. Sisi huku kwetu eti ni holela tu mradi mwombaji anajua Kiingereza, basi unaweza kupata nafasi chuo chochote. Vipi? Tumejidhalilisha wenyewe kwa kusema Kiswahili hakijitoshelezi kimisamiati kwa elimu ya juu. Ndivyo wasomi wetu wanavyotutolea sababu namna hiyo. Hapo ndipo wanakiponda Kiswahili -lugha ya Taifa letu kwa vigezo vya kutokujitosheleza kimsamiati kwa elimu ya juu.

Je, tuliwahi kujiuliza kile Chuo Kikuu cha kwanza ulimwenguni cha Plato kule Ugiriki walipata misamiati ya kutosheleza elimu ile ya juu kutoka wapi? Wajerumani, Wafaransa na Warusi au hata Wachina na Wajapani wasiotumia Kiingereza walipata misamiati ya lugha zao kutoka wapi kwa elimu yao ya juu? Tuondokane na kasumba ya Kiingereza katika vyuo vikuu vyetu.

Ningependa kutoa mifano miwili hapa chini kuelezea namna lugha inavyothaminiwa kimataifa. Kulikuwa na padre mmoja alikwenda Ujerumani kusomea shahada ya juu ya uzamivu (doctoriate) katika dini. Akasoma vizuri kwa Kijerumani. Akaandika tasnifu yake kwa Kiingereza na akaenda kuitetea mbele ya watahini wake (maprofesa wa Kijerumani) eti kwa Kiingereza! Bwana we! Hawakumwelewa, na akaanguka vibaya! Sababu watahini wake waliona lugha iliyotumika si waliyomfundishia, basi hawakuthamini vilivyo. Balaa! Alirudi huku Tanzania mikono mitupu. Kisa? Lugha! Alidhani atawageuza maprofesa wale kwa Kiingereza chake, kumbe wakamdharau kwa kasumba yake na wakamponda. “In Rome do as the Romans” methali ya kale inatuasa.

Mimi niliongoza kikundi cha utamaduni cha JKT kwenda Zambia kwenye sherehe ya miaka 10 ya Uhuru wa Taifa lile Oktoba 1973. Tulikuwa watu 45, maafisa watatu na wapiganaji 42. Tulipangiwa siku ya kumchezea Rais Keneth Kaunda, Ikulu. Siku ile nilibahatika sana kukaa jukwaa kuu tena kushoto kwa Rais Kaunda. Balozi wangu akiitwa Obedi Katikaza akakaa baada ya mimi.

Wakati natoa utambulisho wa kikundi, niliamua kuongea Kiswahili na Senior Master Adam Mwakanjuki (marehemu sasa) akawa mkalimani wa kutafsiri kwa Kiingereza. Lakini mwisho wa mazungumzo yangu, Mzee Rais Kaunda alinieleza kushangazwa kwake kuwa nimetumia Kiswahili rahisi hata yeye na Mzee Reuben Kamanga (Makamu wake) wameweza kufuatilia kwa ukaribu. Nimetumia utamaduni wa Tanzania kuwaelimisha wazambia. Nikajisikia nimewakilisha Taifa langu ipasavyo.

Nilikitukuza Kiswahili, lugha ya Taifa. Kwa nini viongozi wakienda nje ya nchi wanajiandaa kuongea k]

Kiingereza, lugha ile ya waliotutawala?

Kwanini niyaseme yote hayo? Kwanza mimi ni mkereketwa wa UZALENDO. Nikiwa Mwalimu wa Siasa katika JKT nilijisikia nawajibika kuwaonesha vijana uzalendo siyo kinadharia, bali kivitendo. La kwanza kabisa ni hiyo lugha ya Taifa. Taifa haliwezi kutambulika bila kuwa na lugha yake na utamaduni wake. Serikali zote duniani zinajivunia lugha ya Taifa lao, utamaduni wao mila na desturi ambavyo ndio viunganishi vikuu vya asilia katika mataifa. Wimbo wa Taifa au bendera ya Taifa vinaweza kubadilishwa tu, lakini LUGHA na MILA na UTAMADUNI kamwe havibadilishiki. Kuna mataifa ulimwenguni yamebadili bendera za mataifa, yamebadili wimbo wa Taifa, lakini kamwe hayakubadili lugha wala mila na utamaduni wao.

Sasa iweje sisi wabongo, tunajenga utamaduni wa kutumia lugha ngeni ya mkoloni Mwingereza mbele ya mataifa wanaotutembelea? Ni wakati sasa, miaka 53 ya Uhuru tufikirie kuamua suala zima la matumizi ya lugha yetu ya kitaifa KISWAHILI. Lugha yetu hii ndiyo imetuwezesha kushikamana; na kwa nguvu za lugha ya Kiswahili tumepata Uhuru kwa haraka haraka tena bila ya kumwaga damu.

Wasomi wawe wabunifu wa kukuza lugha hii ya Kiswahili kutosheleza masomo ya elimu ya juu. Dhana ya kuwa Kiingereza ni lugha ya kimataifa na ya biashara haijitoshelezi maana sasa Umoja wa Afrika wanakubali Kiswahili kuwa ni lugha ya mikutano huko Adis Ababa. Isitoshe hata huko Umoja wa Mataifa Kiswahili kina nafasi kubwa ya kutumika kama moja ya lugha kuu hasa katika vikao vya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

 

ITAENDELEA