DAR ES SALAAM

Na Costantine Muganyizi

Licha ya kuwapo changamoto hasa za kibiashara zinazotokana na athari za janga la virusi vya corona duniani, mwenendo wa uchumi wa taifa unaridhisha na kuleta matumaini ya kuzidi kuimarika kuanzia mwaka huu.

Hiyo ni kwa mujibu wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo imeelekeza hatua stahiki za kisera kuendelea kuchukuliwa kuhakikisha unaimarika zaidi na kukaa sawa kabisa.

Hatua hizo mahususi ni muhimu kuchukuliwa inapobidi ili kuhakikisha uzalishaji hauteteleki kwa ajili ya kuendelea kuchangia kikamilifu ujenzi wa taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla. 

Kamati hiyo inasema kuwapo kwa changamoto zinazotokana na athari za corona kwenye baadhi ya shughuli za kiuchumi kulichangia uchumi kukua kwa kiasi pungufu ya matarajio mwaka jana. Badala ya kukua kwa asilimia 5.5 uchumi wa Tanzania unakadiriwa kuwa ulikua kwa asilimia 4.8 mwaka 2020, kiwango ambacho ni cha chini sana kwenye miaka ya hivi karibuni.

 Kwa takriban miongo miwili ukuaji wa uchumi nchini ulikuwa ni wa wastani wa asilimia saba, kiwango ambacho kiliifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yaliyofanya vizuri kiuchumi, si hapa Afrika tu, bali duniani kote kwa ujumla. 

“Shughuli za kiuchumi zinatarajiwa kuimarika zaidi mwaka 2021, ambapo ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufikia asilimia 5.6. Ukuaji huu utachangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, kilimo, uchukuzi na mawasiliano,” BoT inasema kupitia kamati hiyo katika taarifa kwa umma baada ya kufanyika kikao chake cha kawaida Ijumaa wiki iliyopita. 

Katika kikao hicho ambacho ni cha 214, kamati ilipitia utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia. 

Kamati ilisema inavutiwa na jinsi BoT inavyotekeleza sera ya fedha ambayo imewezesha kuwapo kwa ukwasi wa kutosha katika sekta ya benki. 

Hali nzuri ya ukwasi ilisaidia kuchochea na kuimarisha uzalishaji na kutoa mchango kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo. 

Aidha, kamati ilifafanua, kuendelea kuwapo kwa mfumuko wa bei katika viwango vya chini kumeendelea kusaidia utekelezaji wa sera wezeshi ya fedha.

 “Mfumuko wa bei umeendelea kubakia katika viwango vya chini, ukiwa katika wastani wa asilimia 3.3 mwezi Aprili 2021, na unatarajiwa kuendelea kuwa kati ya asilimia tatu na tano katika kipindi kilichobaki cha mwaka wa fedha 2020/21. Hata hivyo, ongezeko la bei za mafuta kwenye soko la dunia linaweza kusababisha bei za mafuta nchini kupanda,” inasema kamati.

Bei za mafuta kwenye soko la dunia ambazo zilishuka kwa kiwango kikubwa kutokana na janga la corona zimeanza kuimarika tena siku za hivi karibuni, kukiwa na uwezekano wa kufika dola 70 kwa pipa, kuanzia mwezi ujao baada ya wiki iliyopita kupanda hadi dola 69 kwa pipa moja.

 Pamoja na kuwa moja ya maeneo yanayokumbana na changamoto za COVID-19, biashara ya nje nayo inaonyesha dalili nzuri za kuzidi kuimarika. 

Urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje umeendelea kuimarika baada ya kupata athari za corona kwenye biashara na uwekezaji. 

 Mapato yatokanayo na mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka, hivyo kupunguza athari zilizotokea katika shughuli za utalii. 

Katika kipindi cha mwaka unaoishia mwezi Machi 2021 dhahabu ililiingizia taifa fedha za kigeni kiasi cha dola za Marekani milioni 3,025 ukilinganisha na milioni 2,324 kwenye kipindi kama hicho mwaka 2020.

Mapato ya mauzo ya dhahabu nje ya nchi kati ya Februari mwaka 2018 na Februari mwaka 2019 yalikuwa ni dola za Marekani milioni 1,685.8. Kabla ya janga la corona utalii ndiyo biashara iliyokuwa inaliingizia taifa fedha nyingi za kigeni, kiasi cha dola milioni 2,449.5 mwaka 2018 ukilinganisha na dola milioni 1,549.2 zilizotokana na mauzo ya dhahabu. 

Kwenye mwaka unaoishia mwezi Machi 2021, mapato ya fedha za kigeni yaliyotokana na utalii yaliporomoka kwa karibu asilimia 194 hadi dola milioni 885.2 kutoka dola milioni 2,598.1 kwenye mwaka ulioshia mwezi Machi 2020. 

“Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha kukidhi mahitaji ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, na imeendelea kuwa sawia na makubaliano yaliyofikiwa katika nchi za EAC na SADC,” taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita inasema, na kuongeza: 

“Hali hii imewezesha kuendelea kuimarika kwa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni na kuwezesha kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri urari wa malipo. Kamati ya Sera ya Fedha imehimiza umuhimu wa kuongeza thamani ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na kutafuta masoko zaidi ili kudumisha ustahimilivu wa sekta ya nje.” 

Kwenye ukopeshaji, kamati imesema mikopo ya benki kwa sekta binafsi imeanza kuongezeka na kufikia ukuaji wa asilimia 4.8 kwa mwaka unaoishia mwezi Aprili 2021 kutoka asilimia 2.3 mwezi Machi 2021. Hali hii inatarajiwa kuendelea kuimarika katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2020/21, kutokana na mwendelezo wa sera wezeshi ya fedha na kuendelea kuimarika kwa shughuli za biashara na uwekezaji nchini na duniani. 

Wachumi wanasema kupungua kwa mikopo ya benki ni moja ya sababu kubwa ambazo zimechangia sana “vyuma kubana” kwenye miaka ya hivi karibuni.

 Ukopeshaji wa benki kwa sekta binafsi kulikua kwa asilimia 24.6 kati ya Oktoba mwaka 2014 na Oktoba 2015. Ukuaji huo wa mikopo ya benki ulikuwa asilimia 4.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba 2021. 

Taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania pia inasema sekta ya benki imeendelea kuwa imara, ikiwa na mtaji na ukwasi wa kutosha katika kuchangia ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi. 

Vilevile kamati imeridhika na juhudi za serikali za kulipa malimbikizo ya wazabuni na marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani, hatua ambazo zitasaidia ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi na kuongeza mapato. 

Changamoto hizi mbili nazo kwa kiasi kikubwa zimesababisha kupungua kwa mzunguko wa fedha na kufanya vyuma kubana zaidi. 

“Kutokana na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia, Kamati ya Sera ya Fedha imeridhia Benki Kuu kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi katika kipindi kilichosalia cha mwaka 2020/21. 

“Hatua hii itasaidia ukuaji wa uchumi kupitia ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Mwisho, kamati imeielekeza Benki Kuu kuendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi hapa nchini na duniani na kuchukua hatua stahiki za kisera pale itakapobidi,” inasema taarifa ya kamati.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango na Gavana wa Benki Kuu, Florens Luoga