Mwanzoni mwa mwaka huu Tanzania imejikuta ikikumbwa na uhaba wa mafuta ya kula licha ya ukweli kwamba nchi hii imebarikiwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na maliasili za kila aina.

Ni ukweli wa kutia aibu kwamba kwa miaka mingi taifa letu limeshindwa kujitosheleza kwa chakula na aghalabu hulazimika kuagiza kutoka nje ya nchi mchele, sukari, maziwa na sasa hata mafuta ya kula.

Maelfu ya tani za mafuta ya kula yaliagizwa kuja nchini ili kuziba pengo  lililojitokeza na kuzua tafrani mijini, kitendo ambacho Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, anaamini kuwa hakipaswi kuendelea.

Sasa Mtaka anajipanga kuunganisha nguvu na Mkuu wa Mkoa wa Singida kuhamasisha kilimo chenye tija cha alizeti kitakachowahakikishia wawekezaji wa viwanda vya mafuta na wajasiriamali wenye viwanda vidogo vidogo upatikanaji wa malighafi hiyo.

Tunaomfahamu Mtaka tunaamini atafanikiwa katika malengo yake hayo, kwa kuwa historia inampambanua kama mmoja wa viongozi makini, wenye uthubutu na ubunifu wa hali ya juu, sambamba na usimamiaji wa yale anayokusudia.

Sasa Mtaka anataka kupanua kilimo cha alizeti katika ukanda wa kati wa Tanzania, eneo ambalo linastawisha zao hilo kwa wingi na kuwa nguzo ya uchumi kwa wakulima na hata wafanyabiashara.

Ni vema wazo lake alilolitoa katika hotuba yake ya kwanza akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma baada ya kuhamishiwa hapo kutoka Simiyu likaungwa mkono na wadau pamoja na wananchi kwa ujumla.

Serikali inapaswa kumsaidia Mtaka kufikia malengo hayo, si kwa kumtia moyo pekee, bali pia kumuongezea wataalamu wa ugani na biashara na kukibadili kilimo cha alizeti kuwa cha kisasa zaidi.

Hofu yetu ni kwamba msukumo na mawazo ya Mtaka yasipopewa sapoti na serikali huenda yakahujumiwa na wafanyabiashara wasio na uzalendo wanaofaidika kwa kuingiza nchini mafuta ya kula.

Sambamba na mikoa ya Dodoma na Singida, serikali inapaswa kuimarisha kilimo cha michikichi katika mikoa ya Kigoma na mingine ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, na kuunganisha mnyororo wa Mtaka wa uzalishaji mafuta.

Suala la kuagiza mafuta ya kula sasa linapaswa kuzuiwa haraka, kwa kuwa ni aibu kwa taifa, kwa kuwa ardhi ya Tanzania inastawisha karibu mazao yote yanayotumika kuzalisha mafuta ya kula.

Mbali na alizeti na michikichi, kilimo cha karanga kinafanyika katika maeneo mengi ya Tanzania; kwa nini kuagiza mafuta ya kula kutoka nje? Ndiyo maana tunampongeza Mtaka kwa wazo hilo na kushauri kuwa asiachwe peke yake.