Nilisoma mahali Azam FC walivyoachana na fundi wao wa mpira raia wa Ivory Coast, Richard Djodi. Richard ni fundi kweli kweli, mpira ukiwa mguuni mwake hautamani autoe haraka. Lakini namba zimemhukumu. Azam FC wamemuonyesha mlango ulioandikwa Exit.
Soka la kileo linahitaji wachezaji wanaokimbia kilomita nyingi kiwanjani. Haliwahitaji tena mafundi, linawahitaji wachezaji wavuja jasho jingi kiwanjani katika kuipigania timu. Ukiwa haukimbii sana kiwanjani na hauvuji jasho ni vigumu kufanikiwa. Djodi amehukumiwa hapa.
Nina marafiki zangu wengi wanaocheza kama Djodi. Nikikaa nao maskani tunalishana ‘ujinga’ kuwa Deus Kaseke na Ditram Nchimbi hawajui mpira. Tunaaminishana ‘ujinga’ huu.
Lakini soka la kileo linawahitaji wachezaji kama kina Kaseke na Nchimbi. Hawa ni wachezaji wanaokimbia sana kiwanjani.
Ukiwa nao jua ni kama una chui mpambanaji katika mbuga. Ukiwa na Djodi kiwanjani tegemea atatembea, kama akikimbia, atakimbia kivivu.
Soka la kileo haliwahitaji tena kina Djodi. Ukiwa na kipaji kama cha Djodi kisha ukawa mfia timu kiwanjani unakuwa na faida mara mbili kwa timu, lakini ukiwa na kipaji kama chake kisha ukawa mvivu, unaikaba timu.
Azam FC hawajamuonea Djodi. Namba zimemhukumu Djodi. Hakuna anayeweza kusema Djodi hajui mpira. Mtu huyo hayupo.
Lakini siku hizi mpira ni zaidi ya kuwapiga maadui danadana, matobo, kuupanda mpira na kuwapiga kanzu wachezaji wa timu pinzani. Ni zaidi. Mpira unahitaji vitu vingi vya ziada.
Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solkjaer, aliwahi kusema timu yake inahitaji mshambuliaji ambaye yuko tayari kung’oka pua ili afunge bao. Sijui kama tumemuelewa Ole hapa. Hakusema anataka mshambuliaji mwenye chenga nyingi na madoido, anataka mshambuliaji mpambanaji. Soka la kileo liko hivi. Mahitaji yake ni makubwa zaidi.
Djodi hakuwa mtu wa kufanya kazi ngumu kiwanjani. Alikuwa mtu aliyependa kujifurahisha zaidi kuliko kuifurahisha timu. Ukiwa unacheza kwa kujifurahisha ni vigumu kufanikiwa.
Tumeamua kuchagua upande wa kuushangilia. Kirahisi tu, tumewatoa kafara kina Kaseke na tumejiaminisha kuwa hawajui mpira. Katika hili tumejiaminisha na tumekubaliana kwa pamoja.