Kampuni ya Mabangu Mining ya Mbogwe, mkoani Geita imekanusha kununua mashamba ya wananchi wa Kijiji cha Nyakafuru, JAMHURI limeelezwa.

Awali, wananchi wa kijiji hicho walikuwa wakiilalamikia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya wakidai imezuia gawio la asilimia saba ya mapato yanayotokana na shughuli za uchimbaji dhahabu kwenye eneo walilokuwa wakimiliki.

Madai ya wananchi hao yamo kwenye barua waliyomuandikia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Elias Kayandabila, Oktoba 10, mwaka jana yenye kumbukumbu namba B/N0.ML/01/2020.

“Kwa muda sasa Ofisi ya Mkurugenzi imekuwa ikikusanya mapato katika mashamba yetu bila makubaliano yoyote,” inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa na Lutonja Mashilingi kwa niaba ya wengine, wakidai kuwa wao ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo.

Mashilingi anasema walikuwa wamekubaliana na kikundi cha Isanjabadugu and Partners Miners Group kilichokuwa kikikusanya mifuko ya mawe na kuwapatia asilimia saba ya mawe hayo.

“Hata hivyo, kiasi hicho ni tofauti na taratibu zinazotumika katika migodi mingine ambako wamiliki wa mashamba hugawiwa asilimia 30 ya kinachopatikana,” anasema.

Mara ya mwisho walipata mgawo wao wa asilimia saba Septemba 22, mwaka jana kabla halmashauri haijaanza kukusanya mapato bila kuwashirikisha.

Majibu ya malalamiko hayo yamo katika barua ya Kayandabila ya Oktoba 22, mwaka jana yenye kumbukumbu namba MDC/C.40/4/60, akisema:

“Ofisi ya Mkurugenzi haina mamlaka ya kufuta umiliki wa ardhi ya mwananchi yeyote wala Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe haijawahi kufanya hivyo. 

“Ofisi ya Mkurugenzi inatekeleza maagizo ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambayo ipo chini ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi si mjumbe wa kamati hiyo.”

Kwa upande mwingine, mshauri wa Mabangu Mining Limited, Meja (mstaafu) Bahati Matala, anasema kwa muda mrefu walikuwa wakijishughulisha na utafiti katika maeneo ya Nyakafuru, Kanegele na Mkweni.

“Tuliingia makubaliano na baadhi ya wamiliki wa mashamba wa Nyakafuru kurahisisha shughuli ile bila bughudha.

“Makubaliano yalikuwa ni pamoja na kuwalipa wamiliki 22 wa mashamba walio hiyari wenyewe,” anasema Meja Matala.

Anawalaumu wananchi kuvamia maeneo yaliyokuwa kwenye makubaliano kati ya kampuni na wamiliki wanaoishi Kijiji cha Nyakafuru, akisema hicho ndicho chanzo cha mgogoro uliodumu tangu Septemba 13, 2017.

“Hawajaondolewa hadi sasa ingawa ni kweli kwamba utafiti tulioufanya ulitugharimu fedha nyingi sana. Uvamizi huu ulivuruga mipango ya kampuni na kuleta hasara kubwa,” anasema.   

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyakafuru C, Sandu Mboje, anasema malalamiko ya wananchi ni halali na kwamba mahakama ilikwisha kutoa uamuzi juu ya nani ni wamiliki halali wa mashamba hayo.

“Malalamiko yao kwa sasa yapo kwa Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jaffo. Tunachosubiri ni maelekezo yatakayotolewa, ikiwamo kukazia hukumu,” anasema Mboje.  

Suala hilo pia linafuatiliwa na Ofisi ya Mbunge wa Mbogwe, ambapo Katibu wa Mbunge, Juma Mohamed, anasema ni vema serikali ikawa makini na wawekezaji na kuwabana watekeleze ahadi walizowapa wananchi kama zilivyo kwenye mikataba ya makubaliano.