Matendo na miamala yote itendwayo duniani inagawanyika katika makundi mawili ya mema na maovu. 

Kila nafsi imepewa uwezo wa kuyajua mema na maovu kabla ya kusomeshwa au kuambiwa na mwingine, kwani tayari ilishajengewa uwezo wa kuyajua mema na maovu kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura 91 (Surat Ash-Shams), Aya ya 7 na 8 kuwa: “Na (naapa) kwa nafsi na kwa aliyeitengeneza! Kisha akaifahahamisha uovu wake na wema wake.”

Anuani ya makala ya leo ‘Jamii iamrishe mema na ikataze maovu’ inajaribu kuikumbusha jamii wajibu wake wa kuhakikisha inajenga jamii bora yenye mwenendo mwema kwa kuamrisha mema na kukataza mabaya kama Mwenyeezi Mungu Anavyotutanabahisha kuwa ubora wa jamii au umma unazingatiwa katika kutekeleza wajibu huu mkubwa wa kijamii wa kumuamini Mwenyeezi Mungu, kuamrisha mema na kukataza mabaya kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 3 (Surat Aali Imraan), Aya ya 110 kuwa: “Nyinyi mmekuwa bora ya umma waliotolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyeezi Mungu…”

Naam, ubora wa jamii utathibiti kwa jamii hiyo kumuamini Mwenyeezi Mungu na kisha kutekeleza wajibu wa kuamrishana mema na kukatazana maovu. 

Jamii ambayo haiamrishi mema na haikatazi mabaya hiyo ni jamii mfu, iliyo katika hatari ya kuangamia hata kama itaweka mabango na kutangaza kuwa inamuamini Mwenyeezi Mungu.

Ni vema tukakumbushana kwamba jamii yetu inahitaji sana kukumbushwa juu ya kutenda mema na kuacha maovu. 

Yapo maovu kadhaa ambayo pamoja na kupigiwa kelele nyingi na viongozi wengi wa dini bado yapo na jamii haijakatazika. 

Wajibu wa kuamrishana mema na kukatazana maovu hauna budi kuwa wajibu endelevu kwa jamii yetu, wala si wajibu wa wakati maalumu.

Miongoni mwa maovu ambayo jamii inatakiwa kuendelea kukatazana ni: 

Dhambi ya kusema uongo: Jamii imeizoea sana dhambi ya kusema uongo kwa kiasi cha dhambi hii kutokuwa ya watu wa rika maalumu, bali kusema uongo ni dhambi iliyoenea kwa watu wote watoto, vijana na wazee. 

Kusema uongo kumeleta madhara makubwa ya watu kutoaminiana kiasi cha kuwatia katika mtihani na majaribu hata wale wenye shida za kweli kwa kuonekana waongo. 

Kwa kuwa kuna watu wenye kutembea na vyeti vya hospitali wakiomba msaada wa kununuliwa dawa kama njia yake ya kutekeleza shughuli yake ya kuombaomba, hili limewachongea hata wenye shida za kweli nao kuingizwa katika kundi la wadaganyifu hawa. Dhambi hii inahitaji kukemewa sana.

Dhambi ya kukosa uaminifu: Katika jamii yetu suala la kukosa uaminifu limeota mizizi kiasi cha kutokuaminiana hata ndugu wa familia moja. 

Uaminifu unakosekana kwenye miamala ya kibiashara kwa udanganyifu kutawala. Ni mara ngapi zimesikika taarifa ya kuwekwa mawe katika magunia ya bidhaa ili kuongeza uzito? Ni mara ngapi yameripotiwa na vyombo vya habari matukio ya utapeli na wizi wa kimachomacho hayo yakifanywa na watu wa rika mbalimbali usiowatarajia?

Dhambi ya kununua vitu vya wizi: Ni jambo la kawaida katika jamii yeu watu kuzoea kununua vitu vya wizi, vikiwamo vyakula, nguo, vifaa vya ujenzi, vifaa vya umeme, vipuri vya magari na kadhalika.

Hakuna mwizi hata mmoja ambaye ana tatizo la kupata ‘soko’ la bidhaa yake ya wizi, tatizo kuu la mwizi ni namna ya kupata bidhaa. Na hakuna mteja wa vitu vya wizi ambaye hajui kuwa vitu anavyovinunua ni vya wizi.

Vitu vya wizi vinajulikana kwa njia tatu: Kwanza, uuzaji na mapatano yake ya bei hayawekwi wazi, kuna usiri unaoingizwa. Pili, bei yake inaachana sana na ile bei halisi ya soko la halali. Tatu, muuzaji hafanani na umiliki wa anachokiuza.

Wanaonunua vitu vya wizi wanachangia kwa asilimia kubwa katika kuidumisha dhambi ya wizi. Na kama Watanzania tukiazimia kwa dhati kukomesha wizi, basi yatupasa kwanza tuazimie kuacha kununua vitu vya wizi. 

Tufahamu kwamba kile unachokinunua wewe kwa bei rahisi ameibiwa mwenzako, hivyo ni vema nawe ukubali siku ukiibiwa amefaidika mwenzako naye kama ulivyofaidika wewe.

Dhambi ya kamari za mitandaoni na kubeti: Jamii hivi sasa inakaribia kuhalalisha dhambi hii ya michezo ya kamari. 

Mtu anapotuma namba fulani kwenda katika namba fulani kisha akakatwa shilingi mia tano kwa mfano na kuahidiwa kwamba anaweza kujishindia mamilioni ya shilingi, hiyo ni kamari kupitia mitandao ya simu, na dhambi hii inazidi kushamiri katika jamii.

Kwa upande wa pili ni haya makundi ya vijana pamoja na watu wazima yanayojaa katika maduka ya ‘kubeti’ ili kujishindia pesa baada ya kutabiri ushindi wa timu fulani dhidi ya timu pinzani, hiyo pia ni kamari.

Hizi kamari kupitia mitandao ya simu na maduka ya ‘kubeti’ ni hatari sana kimaadili na kiuchumi kwani kijana akiahidiwa kupata uchumi na utajiri mkubwa kupitia kamari hizi kamwe hataweza kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii, bali atapenda njia ya mkato ili kujinufaisha kimaisha.

Dhambi ya udanganyifu katika elimu na taaluma: Miongoni mwa dhambi zenye athari mbaya kwa jamii ni dhambi ya udanganyifu katika elimu na taaluma. 

Kwamba rushwa ya aina mbalimbali inatumika katika kuthibitisha sifa ya elimu na taaluma kwa yule asiyestahili hatimaye anakwenda kufanya kazi asiyo na ujuzi nayo na kazi kufanyika chini ya ubora na kusababisha hasara kwa rasilimali fedha iliyotumika na kusababisha madhara kwa mali na roho.

Dhambi ya kuiba muda wa mwajiri: Katika jumla ya madhambi ambayo watu hawaoni ubaya wake ni dhambi ya mfanyakazi kutofanya kazi kwa muda na ufanisi unaolingana na mkataba ulioingiwa baina ya mwajiri na mwajiriwa.

Ni jambo la kawaida kumuona mfanyakazi akitumia muda wa kazi ambao ni haki ya mwajiri wake kwa mambo yasiyohusiana na kazi yake kama vile kuperuzi katika mitandao ya kijamii, kupiga gumzo lisilonufaisha kazi yake na hata kusoma magazeti kama sehemu ya kujiliwaza na kujiburudisha badala ya kufanya kazi ambayo analipwa mshahara. 

Mbali ya dhambi ya kuiba muda wa kazi, wapo wafanyakazi ambao wanadiriki kutumia rasilimali na vifaa vya mwajiri wake kufanya yale yanayomletea masilahi binafsi, wala haoni kuwa hiyo ni dhuluma na wizi wa mchana kweupe.

Dhambi ya kuwadhulumu wafanyakazi wa majumbani: Dhambi hii inahusika na uonevu wa kukosekana urari wa haki kati ya kazi anayoifanya mtumishi na masilahi anayoyapata. 

Kwa mfano, wafanyakazi wengi wa majumbani wanalipwa kati ya Sh 50,000 na Sh 150,000. Unapohesabu muda wa kufanya kazi wa mtumishi huyu utaona kwa kuwa yupo pale nyumbani basi anafanya kazi mtawalia kutoka kuamka kwake alfajiri hadi nusu ya usiku huku akiwa hana siku ya kupumzika. 

Mazingira haya ya kazi kwa mtumishi huyu hayana tafsiri nyingine zaidi ya kudhulumiwa haki zake za msingi za kufanya kazi kwa muda maalumu unaokubalika na kupewa mapumziko stahiki.

Dhambi ya kula riba: Riba ni nyongeza ya jinsi ya kitu kimoja, cha aina moja, viwango vya aina moja, kwa malipo ya baadaye. 

Riba ni haramu. Kwa mfano: Kukopeshwa taslimu sarafu moja hivi sasa kwa malipo ya ziada ya sarafu hiyo hiyo baadaye; au kukopeshwa debe moja la ngano hivi sasa kwa malipo ya debe moja na nusu la ngano hiyo hiyo baadaye. Hiyo ni riba na ni haramu; pesa haijizai yenyewe pesa ziada wala ngano haijizai yenyewe ngano.

Riba ninayotaka kuielezea hapa ni tabia inayoendelea kuzoeleka katika jamii kwa watumiaji wa mitandao ya simu, pale mtu anapolipwa haki yake kwa njia ya malipo ya simu kumtaka mlipaji amuongezee ada ya kutolea fedha husika. 

Yaani, mdai anamdai mdaiwa Sh 10,000, na pale mdaiwa anapotaka kumlipa mdai kwa njia ya simu, mdai anamshurutisha mdaiwa kuongeza juu ya anachodaiwa ‘fedha ya kutolea’. Hiki kilichoongezwa ni riba na ni haramu.

Dhambi hizi chache nilizozigusia ambazo kwa mzunguko wa maisha yetu tunazo kila siku bila ya kuona au kujali kwamba tunaharibikiwa katika maisha yetu ya kidunia na ya kiroho.

Hapo ndipo tunapoona umuhimu mkubwa wa kazi ya kuamrishana mema na kukatazana maovu bila ya kazi hiyo kuihusisha na msimu na wakati maalumu. 

Kuamrishana mema na kukatazana maovu ni jambo lenye umuhimu mkubwa hasa tukizingatia jamii zetu zilivyoharibika.

Nihitimishe makala hii kwa kuinasihi jamii kuchukua hatua za makusudi kuimarisha wajibu wa kuamrishana mema na kukatazana mabaya ili kujenga jamii bora inayoridhiwa na Mwenyeezi Mungu Mtukufu.

Tuuzingatie ukweli kuwa kama hatapatikana katika jamii mwanajamii aliye tayari kununua mali ya wizi ni dhahiri wizi utapungua kama si kwisha na mali za wanajamii zitasalimika. 

Na ni hivyo hivyo wale ndugu zetu wanaoendesha biashara ya kuuza miili yao wangekuwa wanakosa wateja miongoni mwa wanajamii ni dhahiri biashara yao haramu ingekufa.

Hivyo wajibu mkuu wa kupiga vita uovu na madhambi katika jamii utabaki kwa jamii yenyewe kwa kutekeleza wajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu.

Shime jamii iamrishe mema na ikataze maovu!

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/0754603050