Mgodi maarufu wa dhahabu wa Buzwagi uliomo ndani ya Manispaa ya Mji wa Kahama unatarajia kuacha uzalishaji Juni mwaka huu, na kufungwa kabisa ifikapo mwaka 2026.
Bila shaka habari hii si njema sana kwa wakazi wanaouzunguka mgodi huo, kwa kuwa kwa miaka mingi umekuwa chanzo cha ajira na kipato kwa kaya nyingi.
Waswahili wana msemo kwamba ‘wakati ukuta, ukifika hugota’. Mgodi huu unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick Gold yenye ubia na serikali, sasa unafungwa.
“Ndiyo, tumo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa kufungwa kwa mgodi huu kwa mujibu wa sheria zilizopo nchini,” anasema Rebecca Stephen, Meneja Mazingara na Ufungaji Mgodi (Environmental and Closure Manager); migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu.
Rebecca amewaambia wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea mgodini hapo mwishoni mwa mwezi uliopita kuwa maandalizi ya kufungwa kwa mgodi yanaendelea vema.
Ili mgodi uweze kufungwa na wafanyakazi kuondoka, kwa mujibu wa Rebecca, kuna hatua kadhaa zinazopaswa kuchukuliwa.
“Sheria zinahitaji mgodi kukarabati mazingira na kurejesha hali ya ubora wa eneo la mgodi kuwa kama ilivyokuwa zamani. Yaani kurejesha uoto wa asili tulioukuta kabla uchimbaji wa dhahabu haujaanza. Hilo ndilo linalofanyika kwa sasa kwa kiasi kikubwa,” anasema.
Mawe-taka makubwa yaliyochimbwa kutoka ardhini na kurundikwa kama mlima (waste rock dump) wa mawe unaoonekana kutokea mbali na kuwa kama alama ya Buzwagi; sasa yanasawazishwa (battering) ili yasianguke, kisha yanafukiwa kwa udongo wenye rutuba na miti ya asili pamoja na ya biashara inapandwa.
Tayari kuna maeneo ambayo miti hiyo imekua, uoto wa asili umerejea, na kuwa msitu wa kuvutia; huku ukarabati ukiendelea katika maeneo mengine.
Kwa hakika eneo la leseni la Barrick kwa sasa lina mandhari nzuri ya msitu wa asili tofauti na eneo la nje.
Shughuli hii inafanywa na Barrick kwa kufuata mpango uliopitiwa na kuidhinishwa na kamati ya wataalamu kutoka idara mbalimbali za serikali (National Mine Closure Committee).
Mashimo ya Buzwagi kufukiwa? Dhahabu imekwisha?
“Hapana. Buzwagi haifukiwi. Lile eneo la ‘open pit’ (mgodi wa wazi) tulilokuwa tukichimba dhahabu litabaki kama lilivyo, lakini tutahakikisha lipo salama.
“Hii ni kwa kuwa ukuta imara uliojengwa kuzunguka eneo letu la uchimbaji utabaki kama ulivyo kuzuia watu na wanyama kuingia katika eneo hili,” anasema Rebecca.
Eneo la leseni la mgodi huo lina ukubwa wa kilomita za mraba 35.32, wakati eneo lililozungushiwa ukuta likiwa ni la kilomita za mraba 10.2.
Mbali na gharama kubwa ya kurejesha mawe-taka na udongo katika shimo hilo, Rebecca anasema kubaki kwake wazi kutatoa nafasi ya kufanyika kwa shughuli za uchimbaji katika siku za baadaye, pia kutawapa nafasi watafiti na wanafunzi wa jiolojia kujifunza aina ya miamba na miundo yake.
Shimo hilo lenye upana mkubwa (kilomita za mraba 0.78) lina urefu (kina) wa mita 340 kwenda chini.
Rebecca anasema eneo pekee litakalofukiwa ni bwawa la kutunzia tope na maji yanayotoka baada ya kuchenjua dhahabu (tailings) ambayo yana mabaki ya kemikali aina ya ‘cyanide’, ambayo ni sumu; na kwamba utaalamu wa hali ya juu utatumika kutekeleza shughuli hiyo ili kuzuia madhara kwa binadamu na viumbe hai wengine.
Kuhusu sababu za Barrick kufunga au kusitisha uzalishaji wa dhahabu Buzwagi, Rebecca anasema: “Si kwamba dhahabu imekwisha, hapana. Ipo. Ila kwa mfumo wetu wa uendeshaji biashara, gharama ya uzalishaji kwa mitambo mikubwa kama hii tuliyo nayo inakuwa kubwa, hivyo ni hasara.
“Uchimbaji unaweza kuendelezwa (na kampuni nyingine) kwa kutumia mfumo tofauti na mashine ndogo. Si kama hizi za kwetu.”
Wakati kazi hiyo ikiendelea, uongozi wa Barrick unajiandaa pia kukabidhi ama serikalini au kwa mamlaka zilizopo eneo hilo miundombinu mbalimbali iliyopo kama majengo, karakana, magodauni na miundombinu na mabwawa makubwa ya kuvuna maji yaliyokuwa yakitumiwa na mgodi.
“Huku mvua si nyingi na sisi tunatumia hadi lita milioni 10 za maji kwa siku. Kwa hiyo tumelazimika kuvuna maji ya mvua na kuyatunza. Tunaamini mabwawa haya ya kuvuna maji ya mvua yataisaidia sana Manispaa ya Kahama na kuwa chanzo kingine cha maji mbali na yale ya Ziwa Victoria, hasa kwa vijiji jirani na hapa,” anasema Rebecca, mhandisi wa mazingira aliyehitimu Chuo Kikuu cha Ardhi cha Dar es Salaam mwaka 2002 (wakati huo kikifahamika kama UCLAS).
Uvunaji wa maji hayo unafanyika kwa utaalamu wa hali ya juu, kwani chini ya bwawa kumewekwa ‘carpet’ maalumu kuzuia maji yasipotee.
Wakati mitambo mingine itahamishiwa kwenye migodi ya Barrick ya North Mara na Bulyanhulu kufuatana na taratibu za kisheria, majengo yaliyopo ndani ya Buzwagi yatabaki na yanaweza kutumiwa kama chuo, hoteli au viwanda vidogo vidogo kwa namna yoyote ambayo mamlaka husika itaona inafaa kwa wakati huo.
Majirani kunufaika
Akizungumzia namna Barrick inavyoachana na jamii inayouzunguka mgodi wa Buzwagi, Meneja Uhusiano wa Jamii, Siama Paul, anakiri kuwapo madhara yatokanayo na kufungwa kwa mgodi wa Buzwagi.
“Kuondoka kuna madhara hata sisi tunafahamu, lakini ni lazima jamii ibaki ikiwa bora kuliko awali. Na hili tunalisimamia kikamilifu.
“Hatutawaacha mikono mitupu. Tunafahamu kwamba wengi walikuwa wakitegemea Buzwagi kwa kujipatia riziki, ndiyo maana tumefanya tafiti na kubaini nini kinahitajika kwa ajili ya jamii hii,” anasema Siama.
“Mbali na masuala ya kushirikiana na halmashauri katika kujenga miradi ya elimu na afya, sisi Buzwagi tunafahamu kuwa shughuli kubwa ya jamii inayotuzunguka hapa ni kilimo.
“Lakini je, kilimo hicho kina tija kwao na kwa taifa? Maswali kama hayo ndiyo yalitufanya kufikia uamuzi wa kutafiti na kugundua kuwa kuna haja ya kuwasaidia wananchi ili kuwa na kilimo endelevu,” anasema.
Siama anasema kwa sasa wameanzisha vituo katika kata za Mwendakulima na Mondo.
Ni vituo viwili vyenye jumla ya vikundi tisa vya kilimo-biashara ambako kuna wataalamu wanaotoa elimu ya kilimo kwa wanachamna wa vikundi hivyo.
Vituo hivi vina mashamba darasa ya umwagiliaji (drip irrigation) na ‘greenhouse’. Pia kutakuwapo na duka la pembejeo za kilimo, maghala ya nafaka, mashine za kukoboa mpunga na nyumba za ukaushaji matunda hasa maembe.
Anasema kabla ya mwaka 2017 kumekuwa na tafiti mbalimbali kuangalia jamii inahitaji nini baada ya mgodi kufungwa.
“Mwaka huo tukatafuta wataalamu na kuanza uboreshaji wa mazao makuu ya mpunga na mahindi. Hadi kufikia mwaka huu tumeona tofauti kubwa.
“Kwa mfano, kabla ya mafunzo mkulima alikuwa anavuna magunia matano hadi 12 kwa ekari moja. Lakini sasa hivi mkulima huyo huyo katika eneo lile lile, anavuna kati ya magunia 30 na 45!” anasema Siama, kauli iliyothibitishwa baadaye na wakulima waliozungumza na wahariri katika kituo cha ushauri wa kilimo biashara cha Mondo.
Siama anatoa mfano wa kilimo cha miembe ambacho ni zao la asali akisema: “Wakulima wamekuwa wakivuna maembe kwa miaka mingi. Wakati wa msimu wa mavuno maembe haya huwa mengi kiasi cha mengine kuoza. Miundombinu ya ukaushaji tuliyosaidia kuiweka itaongeza tija katika hili.”
Hata kabla wahariri hawajaondoka Kahama, Rais John Magufuli, alizindua kiwanda cha juisi kinachotarajiwa kuwa mkombozi wa wakulima wa maembe wa eneo hilo.
Kwa miaka kadhaa sasa Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi umekuwa ukiongozwa na wazawa watupu.