Tanzania imetajwa kama nchi ya mfano katika mapambano dhidi ya rushwa katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ripoti ya kiwango cha rushwa kwa mwaka 2020 iliyotolewa hivi karibuni na Transparency International imebainisha kuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Tanzania imeweza kupanda kwa nafasi saba katika orodha inayopima jinsi nchi zinavyopambana na rushwa.

Mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache sana ambazo zinafanya vizuri katika mapambao dhidi ya rushwa katika eneo hilo.

Kwa ujumla, ripoti hiyo imeonyesha kuwa kiasi cha rushwa duniani kinazidi kuongezeka huku nchi nyingi zikishindwa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hilo.

“Wakati nchi nyingi hazijachukua hatua kabisa au zimechukua hatua kidogo kupambana na rushwa katika muongo mmoja uliopita, zaidi ya nchi theluthi mbili za dunia zimepata alama chini ya 50,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania imeibuka nchi ya pili kwa kupambana na rushwa nyuma ya Rwanda iliyopata alama 54 kati ya alama 100 na kushika nafasi ya 49 duniani. Tanzania ina alama 38 na imekuwa ya 94 duniani.

Katika eneo la Afrika Mashariki, Kenya imepata alama 31 huku ikishika nafasi ya 124 duniani, ikifuatiwa na Uganda iliyopata alama 27 na kushika nafasi ya 142.

Burundi, ambayo ina alama 19 inashika nafasi ya 165 duniani, huku Sudan Kusini ikipata alama 12 na kushika nafasi ya 179, ambayo ni ya mwisho katika orodha ya jinsi nchi inavyopambana na rushwa.

Transparency International inasema katika ripoti hiyo kuwa janga na COVID-19 limefanya kazi ya kupambana na rushwa kuwa ngumu kwa baadhi ya nchi, hasa zile ambazo hazina mifumo imara ya huduma za afya.

“Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa janga la COVID-19 limeyafanya mapambano dhidi ya rushwa kuwa magumu lakini pia rushwa imeendelea kudhoofisha demokrasia,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti inaonyesha kuwa COVID-19 si tu ni janga la kiafya na kiuchumi, bali pia imeongeza ugumu katika mapambano dhidi ya rushwa.

TI inasema kuwa kuna watu katika baadhi ya nchi wamepoteza maisha kutokana na COVID-19 kwa sababu ya rushwa iliyosababisha wahusika kutochukua hatua zinazotakiwa kwa wakati.

“Ripoti kuhusu rushwa kuhusiana na COVID-19 zilikuwa ni za kawaida duniani kote. Kuanzia hongo na wizi hadi upandishaji bei na upendeleo katika vituo vya kutolea huduma za afya kuliifanya rushwa kuchukua sura mpya,” inasema ripoti hiyo.