Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amewataka Wazanzibari kuimarisha amani na umoja walionao ili kuleta maendeleo.

Akizungumza katika Msikiti wa Ijumaa wa Bweleo, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi baada ya Sala ya Ijumaa, Dk. Mwinyi amesema wananchi wote wanapaswa kuungana katika kuendeleza amani na umoja.

“Kukosekana kwa amani husababisha kutofanyika mambo muhimu katika maisha ya wananchi hata kushindwa kutekeleza ibada. Kila mmoja ana wajibu wa kuendeleza na kuimarisha amani,” anasema.

Anasema wananchi wana matumaini makubwa ya kupiga hatua mbele na kubadili maisha yao kwa sababu ya amani.

Anasema amani na umoja ni muhimu katika kuleta maendeleo kwani mifarakano haina tija.

“Kwa upande wangu nina jukumu kubwa la kuwahudumia wananchi na kutekeleza ahadi tulizoahidi wakati wa kampeni, kuhakikisha nchi inapata maendeleo ya haraka na maisha ya wananchi yanaimarika,” anasema.

Kwa kutekeleza hayo, Dk. Mwinyi anasema kuna hitaji msaada wa mawazo, dua na watu kuwajibika katika kufanya kazi.

Amewataka waumini kumuombea dua ili atimize majukumu yake na atende haki kwa kila mmoja kutokana na dhima aliyonayo mbele ya Mwenyezi Mungu na wananchi.

“Katika utekekezaji kuna mamabo yatawakuta watu, kwani ambao hawatawajibika, watawajibishwa. Lengo ni kujenga wala si kulipa visasi,” anasema.

Kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, ubadhilifu, wizi na uzembe, Dk. Mwinyi anasema hayo hukwaza maendeleo iwapo yataachwa bila kudhibitiwa.

Akisoma hotuba ya sala ya Ijumaa, katibu wa msikiti huo, Sheikh Mussa Ali Kirobo, ameeleza haja kwa waumini kushikamana na maamrisho ya Allah na wala wasifarakiane na kuwataka kuwa kitu kimoja.

Naye Katibu wa Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amesisitiza haja kwa wananchi kumuombea dua Dk. Mwinyi kutokana na mambo makubwa anayoyafanya na kuwataka kuithamini neema hiyo ya kupata kiongozi huyo bora. 

Baada ya sala ya Ijumaa, Dk. Mwinyi alikwenda kumtembelea Rais wa Awamu ya Saba, Dk. Ali Mohamed Shein, nyumbani kwake Kibele, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.