Wakati dunia ikizizima kutokana na kusambaa kwa ugonjwa wa corona, kamati za maafa katika mikoa mbalimbali nchini zimekuwa katika kipindi cha tahadhari zikisimamia kanuni na maelekezo yanayotolewa na Serikali Kuu za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.

Hadi tunakwenda mitamboni, ni mikoa mitatu tu ya Tanzania Bara; Dar es Salaam, Arusha na Kagera ndiyo imeripotiwa kuwa na wagonjwa wa corona, ingawa kwa hakika mgonjwa aliyekuwapo Arusha amekwisha kupona. Wagonjwa wengine wawili wapo Zanzibar.

Miongoni mwa majukumu ya kamati za maafa kwa sasa ni kuhakikisha vifaa tiba kwa ajili ya kuzuia maambukizi hayo vinapatikana kwa urahisi na kwa bei halali anayoimudu Mtanzania wa kawaida.

Wafanyabiashara waliopandisha bei ya vifaa hivyo vikiwamo vitakasa mikono, sabuni na barakoa jijini Arusha, wamekamatwa na kamati hizo zinazosimamiwa na wakuu wa mikoa na wa wilaya na sasa wanasubiri kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mpaka wa Namanga unaoitenganisha Tanzania na Kenya umefungwa isipokuwa kwa magari makubwa pekee, hata watu wachache waliokuwa wakiingia kutokea Kenya sasa hawapiti tena baada ya serikali kutangaza sheria ya kuwaweka wageni wote katika karantini ya siku 14.

Jijini Arusha JAMHURI limeshuhudia maisha yakiendelea kama kawaida lakini kwa tahadhari kubwa, wananchi wakisafisha mikono mara kwa mara na kubadili mazoea ya kupeana mikono.

“Watalii ndiyo hakuna kabisa. Mjini hakuna Wazungu tena,” anasema kwa utani mwananchi mmoja mjini humo na kuongeza kuwa magari mengi ya watalii kwa sasa yameegeshwa tu kwa kuwa safari za kwenda kwenye hifadhi za taifa hazipo kabisa.

JAMHURI lina taarifa kuwa asilimia 95 ya safari za watalii au nafasi zilizokuwa zimeombwa (booked) zimefutwa; ndege ya KLM iliyokuwa ikitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kuleta watalii kati ya 300 hadi 400 kila wiki sasa haiji tena. Bei ya chakula jijini humo nayo imeshuka. 

“Ni kwa kuwa chakula kilichokuwa kikinunuliwa kwa wingi kupelekwa kwenye makambi ya watalii kinabaki hapa hapa mjini. Watalii hawapo.”

Hali hiyo inaripotiwa kuwa sawa na Zanzibar, kituo maarufu cha utalii duniani, ambapo kwa sasa hakuna watalii kutoka nje hasa baada ya kufutwa kwa safari za ndege kubwa kutoka Italia iliyokuwa ikileta watalii 300 mara mbili kwa wiki.

Katika kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano chidi ya ugonjwa huo, kampuni na taasisi kadhaa binafsi zimechangia mabilioni ya fedha katika mfuko wa serikali.

Msaada huo wa Sh bilioni 1.185 ulipokewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu iliyopo jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae zaidi nchini.

“Hii ni vita kubwa inahitaji tupigane kwa lengo la kuzuia janga hili lisisambae zaidi nchini, hivyo tuzingatie maagizo ya Rais Dk. John Magufuli ya kumtaka kila Mtanzania ashiriki kwenye vita hii,” anasema. 

Waziri Mkuu amewashukuru wadau waliotoa msaada huo na kuwataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika hatua zinazochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo. 

Miongoni mwa wadau hao ni Benki ya UBA Tanzania iliyotoa Sh milioni 230, CRDB (Sh milioni 150) na NMB (Sh milioni 100). 

Wengine ni Karimjee Jivanjee Ltd na kampuni zake tanzu waliotoa Sh milioni 200 pamoja na kuahidi kufanyia matengenezo magari yote ya Toyota yanayotumika katika kukabiliana na COVID-19 kwa muda wa siku saba bure. Familia ya Karimjee imetoa jenereta yenye thamani ya Sh milioni 75. 

NFRA yawatoa hofu wananchi

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa, amewatoa hofu Watanzania kuhusu uwezekano wa janga la corona kusababisha janga jingine la njaa nchini.

Akizungumza na JAMHURI kuhusu hofu iliyoonyeshwa na mwanasiasa mmoja nchini aliyedai kuwa Tanzania itakumbwa na njaa iwapo wananchi watalazimika kuzuiwa majumbani mwao kutokana na kutokuwa na akiba ya kutosha ya chakula, Lupa anasema:

“Akiba iliyopo inatosha kuwalisha Watanzania hadi msimu ujao wa mavuno . Hakuna hofu. Tunafahamu umuhimu wa kujiandaa kukabiliana na majanga si corona tu, hata mengine kama ya mafuriko ndiyo maana tumepeleka chakula kwa waliokumbwa na maafa huko Lindi.

“Hivi tunavyozungumza ninaelekea Lindi kusimamia ugawaji wa chakula hicho. Tumejizatiti kiasi cha kutosha na kuanzia Mei mwaka huu tutaanza kununua chakula, si mahindi pekee, bali nafaka za kila aina kama mpunga na mtama.” 

Lupa anasema hata wakati Kenya walipokumbwa na baa la nzige, NFRA walikuwa makini wakitambua kuwa baa hilo lingeweza kuingia nchini, hivyo wakajiandaa kukabiliana nalo.

EAC yaungana dhidi ya corona

Mawaziri wenye dhamana ya afya katika nchi sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamefanya kikao kwa njia ya mtandao na kufikia makubaliano kadhaa katika kudhibiti kwa pamoja ugonjwa wa corona.

Kikao hicho cha Machi 25, mwaka huu kiliongozwa na Waziri wa Afya wa Rwanda, Dk. Daniel Ngamije na kuhudhuriwa na mawaziri wa afya katika mataifa yote sita, mawaziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki; mawazi wa biashara na mawaziri wa uchukuzi.

Maazimio yaliyofikiwa ni kuudhibiti ugonjwa huo na kuhakikisha hakuna maambukizi mapya yatakayosambaa eneo zima la Afrika Mashariki.

Katika waraka wa pamoja uliosainiwa na mawaziri wote akiwamo Ummy Mwalimu kwa upande wa Tanzania, mawaziri hao wameelekeza mataifa husika kuendelea kutekeleza karantini ya lazima ya siku 14 kwa wageni wanaoingia nchini mwao.

“Pia kuepuka kuingiza wageni wenye virusi kutoka mataifa mengine kwa kuwapima kwenye mipaka yote; kuahirisha kwa muda mikutano ya ana kwa ana ya viongozi wa EAC; kuruhusu usafirishaji wa mizigo miongoni mwa mataifa haya; kuhakikisha magari ya mizigo yanakuwa na watu wawili au watatu tu na gari litakalohisiwa kuwa mmoja wa wafanyakzi wake ana virusi, lichukuliwe hatua mahususi kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Katibu Mkuu UN azungumza 

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameyataka mataifa yaliyomo vitani kwa sasa kuweka silaha chini na kuungana katika vita dhidi ya corona.

Katika hotuba yake aliyoitoa wiki iliyopita, Guterres amesema vita huzuia misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wenye mahitaji.

“Ugonjwa wa COVID-19 haujali utaifa, rangi au tofauti zozote zilizopo kati ya watu. Hushambulia mtu yeyote wakati wowote hata kama upo vitani,” anasema.

Anasema waliomo kwenye hatari zaidi kupata matatizo wakati wa vita ni wanawake, watoto, walemavu na wakimbizi. 

“Pia mifumo ya afya sehemu zenye vita huwa dhaifu au haipo kabisa, huku wahudumu wachache waliopo nao wakilengwa na silaha nzito za kivita,” anasema Guterres.

Hadi tunakwenda mitamboni, idadi ya watu walioambukizwa corona duniani ilikuwa 678,910; vifo 31,771 na watu waliopona ni 146,319.

Kati ya watu 500,820 waliokuwa wakihudumiwa kutokana na ugonjwa huo; watu 475,443 sawa na asilimia 95 walikuwa na ugonjwa wa kawaida (mild) huku 25,377 wakiwa na hali mbaya.