Vita dhidi ya corona ni zaidi ya masuala ya utabibu. Ni vita ya kuunusuru uhai wa watu na uchumi.
Tangu mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) uliporipotiwa kwa mara ya kwanza Desemba 2019 huko Wuhan, China, sote tu mashuhuda wa hatari iliyopo.
Inatisha. Dunia imetangaza vita. Ni vita ya afya na kuokoa uhai wa watu. Kila mmoja wetu ni askari katika vita hii. Mchango wa kila mmoja wetu utaokoa maisha.
Tunapaswa kufahamu kwamba vita hii imeambatana na vita nyingine kubwa — ya kunusuru uchumi usiporomoke, kwa sababu ya kusimama kwa shughuli za uzalishaji mali.
Tukumbuke kwamba uchumi wowote ule duniani unajengwa/unaundwa na makundi mawili – mzalishaji na mlaji au muujazi na mnunuaji. Mzunguko wa uchumi uko hivyo. Corona si tatizo la afya peke yake.
Corona inaathiri mzunguko huu wa uzalishaji mali katika uchumi kwa kuifunga na kuivunjavunja nguvu kazi ya rasilimali watu isizalishe mazao, bidhaa na huduma ambazo ni chachu ya kukua na kuimarika kwa uchumi.
Uchumi ni watu — kumbe uchumi ni nini? Bila watu hakuna uchumi, kwani watu ndio wazalishaji na watu hao hao ndio walaji au watumiaji wa mazao, bidhaa na huduma za kiuchumi.
Kwa hiyo niweke msisitizo kwamba corona inaambatana na tatizo la kuua uchumi kwa kusababisha baa la njaa, zilizala la mfumuko wa bei na uvunjifu wa amani.
Hivyo basi, jitihada za makusudi zinahitajika katika kuwanusuru watu na makali ya athari za kuanguka kwa uchumi wa dunia kwa sababu ya corona.
Kwa kuwa ugonjwa huu unasambaa kwa kasi kubwa sana, hivyo basi tutambue fika kwamba ni hatari na ni tishio la usalama wa taifa, usalama wa chakula (uhakika wa mtu kupata chakula na kuepuka kufa kwa njaa) na ustawi wetu kwa sababu utatuletea baa la njaa na mfumuko wa bei.
Ukosefu wa chakula na mfumuko wa bei utatokana na ukweli kwamba watu watakuwa hawazalishi chakula na chakula kilichopo hakipelekwi sokoni iwapo maambukizi ya ugonjwa yataendelea kwa kasi yaliyonayo sasa.
Ukosefu huu wa chakula utasababisha bei za chakula kuzidi kupanda bila kushuka na kusababisha mfumuko wa bei (hyperinflation) ambapo bei ya kilo moja ya unga wa sembe inaweza kuuzwa kwa Sh 10,000 au zaidi.
Na kwa kuwa watu wanaotegemea chakula cha kununua wengi wao wanaishi mijini na watakuwa hawaendi kazini (viwandani, maofisini au, sokoni kuuza bidhaa zao) na hawazalishi chochote, basi hawatakuwa na uwezo wa kununua chakula katika soko lenye mfumuko wa bei. Hali hii husababisha majanga na uvunjifu wa amani (rejea hali ya mfumuko wa bei huko Zimbabwe na Venezuela).
Corona imeiteka dunia. Dunia imefunikwa na taharuki. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema (Machi 24, 2020) kwamba maambukizi ya corona Ulaya na Marekani yanaongezeka kwa asilimia 85 katika muda wa saa 24. Nchi hizi ni zenye nguvu na nyenzo bora lakini zinashindwa kuidhibiti corona. Je, katika nchi zetu za Kiafrika hali itakuwaje?
Hakuna nchi iliyo salama na athari za kiafya na kiuchumi za corona. Katika nchi zilizoendelea za Ulaya (kama Italia, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Hispania) hakuna vifaa vya kutosha hospitalini huku zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa wauguzi na madaktari. Hispania kwa sasa (Machi 24, 2020) hawana mahali pa kuweka maiti.
Wazee wanaotunzwa katika nyumba za wazee wametelekezwa na wanakufa kwa kasi kubwa sana. Leo (Machi 24, 2020) Japan imeamua kuahirisha michezo ya Olympic hadi mwakani. Uingereza imeanza kipindi cha wiki tatu (huenda zitaongezwa) za watu kukaa majumbani mwao bila kutoka isipokuwa kwenda kununua chakula, dawa au kwenda kazini kwa ambao hawawezi kufanya kazi wakiwa majumbani kama madaktari na wauguzi.
Huko Italia (Machi 23, 2020) mtu mmoja anafariki dunia kila baada ya dakika mbili kwa sababu ya corona. Kote duniani shule zimefungwa. Huduma nyingi za kiuchumi zimefungwa. Maisha tuyajuayo ya uhuru wa kutembea na kwenda unakotaka, wakati unaotaka, hayapo tena. Dunia imo kizuizini. Dunia si ile tuijuayo. Hofu kuu imetanda. Je, katika nchi zetu za Kiafrika tumejiandaa vipi kukabiliana na mlipuko huu wa corona na athari zake?
Tukumbuke kwamba katika kipindi hiki kila nchi inajiangalia yenyewe. Hakuna wa kumsaidia mwenzake isipokuwa Cuba na China zilizopeleka Italia madaktari, dawa na vifaa. Je, zitasaidia nchi ngapi? Hapa ndipo tunauona umuhimu wa kujitegemea.
Naipongeza serikali kuchukua hatua zote za haraka na muhimu katika vita hii kubwa dhidi ya corona, ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma, kutenga maeneo ya karantini na kuziandaa hospitali kukabiliana na ugonjwa huu.
Lakini kazi ya kupambana na corona ni kubwa zaidi, kwani corona ni tishio dhidi ya afya na uhai wa watu ambao ndio wazalishaji mali. Tukumbuke kwamba afya ndiyo msingi wa uchumi imara. Msemo wa ‘mtaji wa maskini ni nguvu zake (afya) mwenyewe’ unatukumbusha umuhimu wa afya imara katika kukusanya mtaji tuweze kuinuka kiuchumi.
Kwa hiyo kwa mikakati mizuri na umakini tupambane wenyewe na in shaa Allah tutashinda. Penye nia pana njia.
Nami ninaomba kwa heshima na taadhima kuwasilisha maoni yangu ya nini kifanyike katika jitihada za makusudi za kupunguza, kuondoa na hata kuepuka athari za corona katika maisha ya watu na uchumi wa Tanzania.
Nini kifanyike?
Serikali iwahamasishe wakulima kote nchini kuzitumia mvua zinazoendelea kulima na kupanda mazao ya nafaka na mengine ya chakula yanayokomaa katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne au hata sita.
Zifanyike jitahada za makusudi za kulima mahindi, maharage, mchele, mtama, uwele, ulezi, viazi vitamu, viazi vikuu, muhogo, nyanya, vitunguu na mengineyo kuhakikisha kwamba tuna chakula cha kutosha mashambani.
Na ikitokea shughuli zote zikasimamishwa na watu kuzuiwa kutoka majumbani basi wawe na uhakika wa usalama wa chakula. Njaa haitawaathiri.
Serikali ipeleke muswada bungeni ili itungwe sheria ya kuhusu namna ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa corona na magonjwa mengi ya milipuko yenye athari kama corona.
Sheria hii ambayo naiita ‘Sheria ya Corona’ itoe mwongozo wa namna ya kuendesha shughuli mbalimbali za kuokoa maisha, kutokomeza ugonjwa wa mlipuko, kuulinda uchumi usiporomoke kwa sababu ya njaa na ukosefu wa chakula na mfumuko wa bei katika kipindi kigumu ambacho watu hawazalishi na hawana uwezo wa kifedha wa kukidhi mahitaji yao.
Sheria hii itupe mwelekeo na dira ya nini kifanyike, kwa nini kifanyike, kifanyike kwa namna gani, kifanyike wapi, kifanyike kwa nani na kifanyike katika muda gani. Sheria hii izingatie misingi ya utu, ambayo ni moyo wa amani, umoja, udugu na mshikamano wetu bila kuathiri haki za watu.
Bila ya uwepo wa sheria ya kutuongoza katika vita dhidi ya corona upo uwezekano mkubwa wa mambo kwenda shaghalabaghala na tutajikuta katika hali ngumu, kwani baadhi ya watu wanaweza kufanya au kutoa uamuzi juu ya mambo yanayoweza kuhatarisha usalama wa wananchi wengine na ustawi wa nchi yetu.
Sambamba na Sheria ya Corona, serikali ipeleke muswada mwingine bungeni wa kuiruhusu serikali kukopa pesa kutoka Benki Kuu (BoT) ili kununua nafaka. Nitafafanua.
Muswada huu utaiwezesha serikali kupata pesa za kuendesha shughuli zote za kuhakikisha nchi ina akiba ya kutosha ya chakula na watu wanapata chakula kwa bei nafuu au bure kutugemea na vigezo ili kuzuia watu wasife njaa na mfumko wa bei usivuruge uchumi.
Mtu anaweza kusema serikali kukopeshwa na BoT kutasababisha ichapishe pesa zaidi na kuziingiza katika mzunguko wa uchumi jambo ambalo linajulikana kama Uzaji wa Pesa (Quantitative Easing) hivyo kusababisha mfumuko wa bei mbele ya safari.
Jambo ambalo ninaliongelea hapa ni tofauti kabisa na Quantitative Easing. Katika Quantitative Easing ambayo inafanywa na Benki Kuu za nchi za Ulaya na Marekani, pesa huingizwa katika mzunguko wa uchumi bila uwepo wa dhamana yenye thamani inayolingana na pesa iliyoingizwa katika mzunguko wa uchumi — wanachapisha pesa (makaratasi au stationery) na kuyaingiza katika mzunguko wa uchumi.
Pesa hizi ambazo hazijatokana na shughuli yoyote ya uzalishaji mali (bidhaa au huduma) hupelekwa kwenye mabenki ya biashara kwa riba nafuu na watu hupewa fursa na kukopeshwa.